August 13, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Wanafunzi hewa ‘wakwapua’ bilioni 3.8

Spread the love

TIMU ya uhakiki wa wanafunzi wanaonufaika na mikopo ya elimu ya juu hapa nchini imebaini kuwa, Vyuo Vikuu 29 vimeitia hasara ya Sh. 3.8 bilioni Serikali kutokana na kuwalipa fedha wanafunzi 2,192 wasiokuwepo vyuoni, anaandika Pendo Omary.

Kufuatia upotevu huo wa fedha za serikali, Profesa Joyce Ndalichako, Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia amevitaka vyuo vikuu ambavyo vimepokea na kulipa fedha wanafunzi ambao hawapo vyuoni kurejesha fedha hizo ndani ya siku saba kuanzia leo.

Prof. Ndalichako amesema, Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu (HESLB), imeshirikiana na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) kati ya mwezi Mei hadi Julai mwaka huu na kufanya uhakiki wa wanufaikaji wa mikopo ya elimu ya juu kwa vyuo 31 kati ya 81.

“Timu ya uhakiki imebaini wanafunzi 2,192 walinufaika na mikopo katika vyuo 31 hata hivyo uwepo wa wanafunzi hao haukuwahi kuthibitishwa,” amesema.

Vyuo vilivyoongoza kwa kuwapatia fedha wanafunzi hewa ni, Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), wanafunzi 350 ambapo fedha zilizopotea ni Sh. 703.4 milioni, Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM) wanafunzi 364 fedha zilizopotea- Sh. 460.9 milioni na Chuo Kikuu cha Sokoine (SUA) wanafunzi 235 waliogharimu jumla ya Sh. 387.6 milioni.

Vyuo vingine ni; Chuo Kikuu cha Mtakatifu Joseph wanafunzi 200 gharama zao zikiwa ni Sh. 408.8 milioni na Chuo Kikuu cha Mtakatifu Yohana Dodoma (SJUT) wanafunzi 164 ambao jumla ya fedha zao ni Sh. 29.4 milioni.

“Uhakiki wa malipo hayo unaonesha kuwa wanafunzi hao 2.192 ambao hawakuonekana kuwa wapo vyuoni katika zoezi la uhakiki lililofanyika wameigharimu serikali shilingi bilioni tatu, milioni mia nane hamsini na saba na laki saba hamsini na nne elfu, mia nne sitini na nane (3,857,754,468).

Hivyo naagiza vyuo vikuu vyote ambavyo vimepokea fedha za wanafunzi wasiokuwepo vyuoni virejeshe fedha hizo ndani ya siku saba kuanzia leo,” amesema Prof. Ndalichako.

Mbali na kutakiwa kurejesha fedha hizo, vyuo hivyo vimetakiwa kuwasilisha Bodi ya Mikopo taarifa zote za kitaalam na kibenki, kuchambua na kuingiza taarifa ya mabadiliko ya wanafunzi na bodi hiyo imetakiwa kuchukua hatua kwa wote waliofanikisha malipo ya wanafunzi hewa.

Kati ya Vyuo Vikuu 31 vilivyofanyiwa uhakiki huo, ni vyuo viwili tu ambavyo havikupatikana na wanafunzi hewa, vyuo hivyo ni; Chuo Kikuu cha Mtakatifu Agustino (SAUT, Mbeya) na Chuo cha Elimu ya Biashara (CBE, Dodoma).

 

error: Content is protected !!