January 19, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Wanafahamiana tena wamoja

Spread the love

RAISI anajidhalilisha kwa kukithiri mizaha. Anajisahau akidhania Saigoni – kijiwe cha maalwatan wa Da’Salama, wehu kwa utani wa Simba na Yanga.

Alikuwa maarufu miaka ile ya 1980. Niliwahi kumsikia akisema enzi za kusakata rumba usiku wakienda Mnazimmoja kwa miguu kutoka Magomeni.

Sasa hajui angali rais wa watu milioni khamsini, ambao zaidi ya asilimia 99.01 wana akili za kuambiwa na wanatia za kuzaliwa. Wanamjua ni kiongozi mkubwa kama mfalme vile. Anaajiri, kuadhibu na kufukuza. Siku ile akafukuza mfanyakazi kizembe, majuto hadi leo.

Haachi maskhara ya Saigoni hata kwa masuala ya maslahi na Watanzania. Kwanza niseme ananikosha kwa baadhi ya vitu, k.mf anapenda wanyonge, sema hawatetei kwa moyo anowapendea.

Pili, simchukii Luwasa, mwanasiasa ambaye hawakukutana barabarani. Wakiitwa Boys Two Men tangu ujanani walipokuwa vijana watiifu kinoma wa itikadi ya Ujamaa na Kujitegemea alioupandikiza mwalimu.

Amini usiamini, JMKhK na ENL marafiki kuliko marafiki uwajuao. Wanafahamiana na mpaka sasa wangali wamoja. Wanafanyia ishtizai wananchi.

Kiongozi alisema Luwasa alipata tu ajali ya kisiasa. Akamuinua mkono alipokwenda Munduli akimsifia “mnaye kiongozi makini.”

Fikiria wewe rais ukurupuke umteue Jabir Idrissa usiyemjua awe waziri mkuu wako. Inakwenda? Walikuwa na bado wamoja. Tusidanganywe.

Kweli, amekumbuka Saigoni akidhani maisha yalivyo leo sawa na miaka ile na kina mzee Khamis Kilomoni, Yusuph Mzimba, Amijee, Mangara Tabu, Amiri Bamchawi, ukienda pale mkavu unakula, unakunywa Potelo(?) na pakiti ya sigara nyota, vyote bure. Wapi leo?

Leo unavochuma ndo uishivo – mbuzi hula kutokana na urefu wa kamba yake. Ukichuma hulali njaa labda uzembee wakupige kitapeli mjini. Wakubwa wajue Richimondi wanavyoileta tena wanajipalia makaa wenyewe. Utapeli utapeli tu hata ukiutia udi.

Nchi zinatapeliwa vilevile, la muhimu hatua inayofuata kutapeliwa. Zinaridhia, kunyamazia au zinadhibiti matapeli? Mawili ya kwanza ni kudhulumu mali ya wananchi.

Richimondi rais alisema amekutana naye Amerika, nchi aloizoea kabla hajawa rais. Aliwaambia mawaziri Richimondi anaweza kuleta umeme mwingi.

Nini? Ndo wa kwanza kumjua Richimondi. Hapo tena, kila kitu mbelembele, si ndio utamaduni wa chama chetu kinacholea demokrasia(?). Wamechukia Luwasa kachomoka.

Richimondi kaleta karatasi zake za kontrakti, Taanesiko wakabaini ninihii, wakadharauliwa. Luwasa keshasema kasema, akamshika Balozi Seeyafue kuulizia vizuri jikoni – ona wa Kaayaratu ahoji “mzee nani hapa (hamjui nani)?” Chezea wanaume baba; yuwapi padre-mwanasiasa-mtakaurais-mstaafusiasa – kizani kama Richimondi.

Majibu si yamekuja; halafu… kuona Luwasa kahisi utapeli, mgeuko. Kontrakti akauizwa Duwansi, akaja Mwarabu wa kuchonga mmiliki wao. Yaelezwa waliteta kama Sethiyi alivopelekwa, Duwansi kapelekwa. Tusidanganywe.

Richimondi, Duwansi na Dipugrini yote kama EPA na Esikroo. Michongo ya kileleni. Hawa wengine wanatajwa tu mbuzi wa kafara. Mtindo ule wa sebuleni, kajamba baba kukaripiwa mwana, we nanihii umeja….

Na Tototundu naye, Rais ana chamache kinokufa maana hawakumsikiliza na kumzingatia alivowaonya waache fitina, rushwa na kutegemea Polisi. Anakupeleka kubishana ili usichambue sera ya Ukawa wanayoiita Ukiwa huku ikiwabana hoi. Anakuzoea Rais. Hukumbuki mlipokwenda Ikulu akakutania eti ndo ulivuruga sheria ya Katiba. Muwache anaaga rais. Ukipanda jukwaani muuze zaidi Luwasa, mizaha ya Richimondi kamuachia Rais na Sam6, na Mwakyi wababaike nayo.

Ama, lakini nakumbuka mradi wa windipawa Kisasida (Singida), wapi Isango mjanja? Mradi ulozua sakata hata kumtengenezea mkosi Luwasa. Ah, wanasema nafasi imekwisha. Nisalimieni Saigoni. Idi njema!

Nawaachia habari motomoto:

Wakati Ethiopia imezindua treni ya umeme na Kenya imeshanunua vichwa vya treni ya umeme, Tanzania imenunua mabehewa feki kwa mkupuo wa shilingi bilioni 650 chini ya uwaziri wa daktari wa sheria, Mwakyiii.

error: Content is protected !!