Saturday , 20 April 2024
Home Gazeti Makala & Uchambuzi Wanachojua ni kufoka, kutisha
Makala & Uchambuzi

Wanachojua ni kufoka, kutisha

Spread the love

BABA utufundishe kusema lakini kusema sawasawa. Kusema ni kukiri na kukana kwa wakati mmoja. Serikali ya watu husema na watu wake. Anaandika Mwalimu Wetu … (endelea).

Wakati mwingine tumekuwa tukisikia serikali ikisema hata pale pasipo na lazima ya kusema huku ikikaa kimya hata pale ilipotakiwa kusema. Serikali za kiimla zote ni serikali viziwi na ni serikali bubu.

Zinajua kufoka na kutisha basi. Hakuna timamu anayependa kufokewa ama kutishwa hivyo wananchi huzidharau serikali hizo. Viongozi wakishajua kuwa wanadharauliwa na wananchi, badala ya kujiuliza ni kwanini au wapi wamekosea, wao hudhani kufoka, kutisha watu na hata kuwatesa, ndiyo suluhisho.

Wanapofanya hivyo huwa hawaelewi kuwa wanafanya hivyo kwa hasara yao wenyewe. Na mara nyingi hayo huwa siyo yao. Hutokana na kuwasikiliza wapambe na wabangaizaji wao ambao aghalabu huwa ni watu
waliopuuzwa na jamii.

Kiongozi madhubuti hana wapambe. Ukiona kiongozi hawasikilizi wale anaowaongoza jua huyo hafai kuwa kiongozi wa watu. Kiongozi mhovyo tu ndiye hudhani anajua kila kitu.

Baba kitinda mimba wa tumbo la mama yangu ni mama mwenye familia na ni mwalimu kule Iringa. Anajua kuwa kama alivyokuwa baba yetu sipendi kuchapa mtoto hivyo sipendi viboko shuleni.

Akaniambia kaka watoto bila kiboko hawafundishiki. Katika kusoma kwangu kote, mara ya mwisho nilimwona mwalimu anamchapa mtoto shuleni kwetu, ni wakati namaliza shule ya msingi darasa la nne, mwaka 1964.

Tangu nilipoingia shule ya kati (middle school) darasa la tano katika Seminari ndogo ya Mlowo mpaka nilipomaliza masomo yangu katika Seminari kuu ya Filosofia, Ntungamo, katika shule zote nilizosoma, sikuwahi kuona mwalimu awe padri au mwalimu wa kawaida akiwa ameshika fimbo mkononi; sembuse kumchapa mwanafunzi.

Na shule hizo zote kwa wakati huo zilikuwa ni shule za mfano, kinidhamu na kitaaluma. Kumbe unaweza kuwatawala watu na wakatawalika bila kuwateka wala kuwatesa hata bila kuwapoteza wala kuwaua wengine.

Anayehitaji nguvu ili atawale, hatoshi! Baba ulifurahisha sana kule Morogoro ulipowalazimisha jamaa wamchangie fedha mama wa watu. Wananchi wako walikufurahia na wakakushangilia sana.

Na baba ulipendeza! Waliotia doa ni wale walioonekana kama ni walinzi. Wananchi hawakuona kilichokuwa kinalindwa.

Walijiuliza, hivi hawa jamaa wameyaona makosa gani ambayo wanadhani mkuu ameyafanya yanayoweza kumkusanyia maadui wengi kuliko wakuu wote waliomtangulia?

Ulimwita mwenyewe lakini kila aliposogea alizuiwa na mlinzi fulani mpaka uliposema mwacheni. Aliendelea kusogea na wao waliendelea kumzuia na wewe ukaendelea kusema mwacheni. Hata alipokusogelea kabisa ulinyoosha mkono umshike, lakini aliponyosha wake alizuiwa mpaka uliposema mwacheni nimshike mkono!

Baba umefanya nini mpaka hawa jamaa wadhani uko katika hatari kubwa hivi yakushambuliwa? Furaha ya kuishi na watu wa Mungu wenzako unaipataje?

Nilipoona yale nikamrejea Muumba wangu na kumshukuru kwa kunijalia maisha ya amani na furaha tele katika moyo wangu! Furaha yakuona wengi wanakujali, wakubwa kwa wadogo.

Masikini wanakupenda na wenye ukwasi pia! Abdulrahman aliniambia, “Mayega una amani kubwa sana katika kifua chako!” Nikayakumbuka maneno ya Baba wa Taifa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, alisema, “Mtakapoona tumejizidishia ulinzi jueni kuwa tunawaibia!”

Ulinzi huu ungekuwa na maana zaidi kama mtu angekuwa anazikwa nao. Lakini kaburini mtu hafukiwi hata na kisu cha mfukoni! Nimekutana na kushikana mikono na marais wangu wote wa awamu zilizotangulia.

Na Rais Mwinyi akiwa mlezi wa chama chetu tulikuwa tunamtembelea kama Baba, Ikulu, anakaa nasi kule nyuma, ‘tunachati’. Kwa marais wote hao walinzi walikuwapo.

Lakini hakuna kati yetu aliowahisi mwilini wakati wote tulipokuwa na Rais. Lakini kwanini uwe na maisha yaliyojaa wasiwasi muda wote na hofu nyingi mpaka uogope hata na hatari isiyokuwapo?

Baba Juni mosi mwaka huu Hamida Mapunda wa Kijiji cha Mugundeni, Tarafa ya Mang’ula Wilaya ya Kilombero, akiwa katika siku zake za mwisho za ujauzito wake, alikamatwa na polisi na kutiwa ndani.

Tuhuma ni kwamba mume wake Abdallah Mrisho alinunua kitanda ambacho nacho kinatuhumiwa tu kuwa ni cha wizi! Ni unyama wa kiasi gani kumshikilia katika mahabusu ya polisi kwa siku sita mwanamke aliyetayari kwa kujifungua wakati wowote?

Siku ya sita uchungu ulipomzidia huku maji ya uzazi yakimtoka alitolewa ndani na makatili wale mpaka kwenye majani. Na kama mnyama vile, akaachwa huko ajifungue mwenyewe!

Mtanzania mpya wa awamu ya tano (kichanga chake) kikaiona anga ya nchi yake kwa mara ya kwanza kikiwa katika majani sawa na vichanga vya mafisi na manyani vinavyozaliwa huko msituni. Inauma sana!

Halafu anasimama mwanaume mtu mzima ambaye mpaka umri ule hajawahi kupatwa na uchungu wa kuzaa, hatujui huko mbele, anasema wamefungua faili. Halafu?

Kusema gani huku? Baba utufundishe kusema! Nani kasema awamu yetu imepunguza rushwa? Tumbusi wa sasa wanadaiwa kuomba rushwa kwa kupiga, galagaza, wakikataa wanawatia ndani.

Mzazi mwingine Hamida anasema, “Mwanangu alifariki Mei 12 lakini nilizuiwa kutoka hospitalini nikamzike mwanangu. Ilinibidi nilale wodini huku mwili wa mwanangu ukiwa kwenye chumba cha kuhifadhia maiti mpaka sh. 638,000 kama kikombozi zipatikane!”

Hamida ambaye alijifungua mtoto utumbo wake ukiwa nje na kulazimika kufikishwa Muhimbili anasema, “Binafsi nilishangaa kwasababu siku zote nimekuwa namsikia Waziri wa Afya anasema mtoto chini ya miaka mitano hutibiwa bure!”

Mpaka leo si Waziri si Naibu aliyesema kitu. Mkuu wa kitengo cha Mawasiliano kwa umma cha MNH, Aminiel Aligaesha amesema, “Hii haijalishi kama ni mama mjamzito au mtoto. Hiyo ndiyo sera yetu na ipo wazi kabisa.”

Kusema gani huku? Baba utufundishe kusema! Baba kama utautaka tena urais mwaka 2020 utakapofika tena pale Morogoro na kwingine ulikofanya kama vile, utapokewa na umati mkubwa zaidi ya ule!

Lakini hao wote hushangilia kwa nguvu kubwa, lakini siyo wapiga kura. Hawajiandikishi na wakijiandikisha siku ya kupiga kura hawatokei.

Hayo tumeyaona kwa mwanamwema Augustino Lyatonga Mrema alipogombea urais. Hapo ndipo watu wazima watamkumbuka Abdulrahman, lakini nyakati zitakuwa zimeishapita!

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Articles

BiasharaMakala & Uchambuzi

Kanda ya Ziwa yaonyesha NMB inavyosaidia afya ya mama na mtoto

Spread the loveMafanikio inayozidi kupata Tanzania katika kupunguza vifo vya mama na...

Habari za SiasaMakala & Uchambuzi

‘Mwanapekee’ wa Rais Samia: Atabadili nini Arusha?

Spread the loveMAPEMA wiki hii, baadhi ya viongozi walioapishwa na Rais Samia...

Habari MchanganyikoMakala & Uchambuzi

Kipunguni waihoji serikali, ziko wapi fedha za fidia?

Spread the loveWATU wanaodai kwamba serikali ya Chama Cha Mapinduzi ni sikivu,...

Habari za SiasaMakala & UchambuziTangulizi

Askofu Bagonza: Tusichonganishwe; tusichokozane na tusikufuru

Spread the loveJOTO la chaguzi linapanda kila siku hapa nchini. Upo umuhimu...

error: Content is protected !!