Thursday , 18 April 2024
Home Habari Mchanganyiko Wanachama 15 NMB Business Club wapaa Uturuki
Habari Mchanganyiko

Wanachama 15 NMB Business Club wapaa Uturuki

Spread the love

WAFANYABIASHARA 15 ambao ni Wanachama wa Klabu za Biashara za Benki ya NMB (NMB Business Club), wameagwa jijini Dar es Salaam leo asubuhi tarehe 17 Oktoba, 2022 na kuondoka jioni kwenda Istanbul, Uturuki kwenye ziara ya siku tisa – kutembelea Maonesho ya Biashara ya Kimataifa (Trade Fairs 2022). Anaripoti Mwandishi Wetu … (endelea).

Hafla ya kuwaaga wafanyabiashara hao imefanyika Makao Makuu ya NMB, ambako Afisa Mkuu wa Mikopo wa Benki ya NMB, Daniel Mbotto, aliwakabidhi tiketi za safari hiyo, akishuhudiwa na Afisa Mkuu wa Huduma Shirikishi NMB, Nenyuata Menjooli na Mkuu wa Idara ya Biashara wa benki hiyo, Alex Mgeni.

 

Hii ni mara ya pili kwa NMB kuratibu ziara za aina hiyo, mara ya kwanza ilikuwa mwaka 2019, ambako wafanyabiasahara 10 walitembelea na kushiriki Maonesho ya 125 ya Canton Fair 2019, yaliyofanyika mjini Guangzhou, China, kabla ya janga la corona kukwamisha safari hizo miaka miwili ya 2020 na 2021.

Akizungumza kabla ya kuwakabidhi tiketi za safari zao kwenda na kurudi katika ziara hiyo iliyogharamiwa na NMB, Mbotto alisema lengo la kusafarisha wafanyabiashara hao ni kuwapa fursa ya kupata ujuzi wa kimaendeleo yatakayowasaidia kukuza biashara zao na kufundisha wengine pia.

Afisa Mkuu wa Mikopo Benki ya NMB, Daniel Mbotto (katikati), akimkabidhi mfano wa tiketi ya ndege mwakilishi wa Wanachama 15 wa Klabu za Biashara za NMB, wanaokwenda nchini Uturuki kutembelea maonesho ya biashara ya kimataifa kwa ufadhili wa benki hiyo, Paulo Lema, katika hafla iliyofanyika jijini Dar es Salaam leo. Kushoto ni Mkuu wa Idara ya Biashara NMB, Alex Mgeni, Afisa Mkuu wa Huduma Shirikishi NMB, Nenyuata Menjooli (wa pili kulia) na kulia ni Mwenyekiti wa Klabu za Biashara za NMB Mkoa wa Dar es Salaam, Award Mpandilah.

Alivitaja vigezo vilivyotumika kupata wafanyabiashara hao kuwa ni pamoja na historia yao nzuri ya ukopaji na urejeshaji mikopo, kupitisha biashara zao kwa asilimia 95 katika benki ya NMB, kusaidia kwao kuunganisha wafanyabiashara kujiunga NMB na uwezo wa kuchangia asilimia kidogo za safari.

Aidha, aliwasihi wafanyabiashara hao kuhakikisha ziara hiyo inaleta mabadiliko yao kibiashara, wanatumia vema kila fursa watakayoiona na kurejea nyumbani wakiwa na ujuzi mkubwa, sambamba na kutanua mtandao wa kibiashara ili kukuza biashara zao na uchumi wa taifa.

Naye mwakilishi wa wafanyabiashara 15 walio katika msafara huo, Paulo Lema, aliishukuru NMB kwa fursa mbalimbali inazotoa kwa wateja wao wa kada mbalimbali katika kuwaongezea nguvu ya kukua kiuchumi na kusisitiza kuwa kadri wanavyoshikwa mkono, wanarahisishiwa ukuaji wao kibiashara.

Lakini pia, kwa niaba ya wafanyabiashara waliopata fursa kama hiyo mwaka 2019, Award Mpandila, ambaye ni Mwenyekiti wa NMB Business Club Mkoa wa Dar es Salaam, alikiri kuwa ziara yao katika Maonesho ya Canton Fair yamewasaidia kuwabadili kimfumo, kiuendeshaji na ufanyaji biashara.

 

Wafanyabiashara hao watawasili Uturuki saa 12 jioni ya Oktoba 18 na Oktoba 19 2022 kuanza ziara ya kutembelea maonesho hayo ili kuwapa mwanga kibiashara na watakuwa huko siku 9 wakijifunza mengi kutoka kwa wafanyabiashara wengine wa kimataifa.

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Articles

Habari Mchanganyiko

Carbon First, Ruangwa wasaini makubaliano ya biashara ya hewa ukaa

Spread the love  KAMPUNI ya Carbon First Tanzania Limited na Halmashauri ya...

Habari Mchanganyiko

CBE yawakumbuka wenye mahitaji maalum Jangwani

Spread the loveCHUO cha Elimu ya Biashara (CBE), kimetoa msaada mbalimbali na...

Habari Mchanganyiko

Mume auwa mke kwa kumchoma visu, ajisalimisha Polisi

Spread the loveJACKSON Kalamji (49), anashikiliwa na Jeshi la Polisi jijini Mwanza,...

Habari Mchanganyiko

Serikali yatoa ajira watumishi 46,000, yatangaza utaratibu mpya kuajiri

Spread the loveSERIKALI imetangaza nafasi za ajira za watumishi wa umma 46,000...

error: Content is protected !!