Friday , 29 March 2024
Home Gazeti Habari za Siasa Wanachama 11 kuchuana uchaguzi ACT-Wazalendo
Habari za Siasa

Wanachama 11 kuchuana uchaguzi ACT-Wazalendo

Juma Duni Haji, Naibu Kiongozi wa chama cha ACT-Wazalendo
Spread the love

 

WANACHAMA 11 wa chama cha siasa cha upinzania, ACT-Wazalendo, wamechukua fomu kuomba nafasi za uongpzi, wawili wakiwania uenyekiti. Anaripoti Selemani Msuya, Dar es Salaam … (endelea).

Wawili hao Juma Duni Haji na Hamad Masoud Hamad wanawania kuziba pengo lilioloachwa wazi kwa kifo cha Maalim Seif Sharif Hamad kilichotokea tarehe 17 Februari 2021.

Duni na Hamad wanatajwa kuwa na ushindani mkubwa hali ambayo inahofiwa kusababisha mpasuko ndani ya chama.

Hayo yalisemwa na Mwenyekiti wa Kamati ya Uchaguzi ya chama hicho, Joram Bashange akizungumza na waandishi wa habari makao makuu ya chama hicho, Kijitonyama, Kinondoni, Dar es Salaam.

Bashange alisema uchaguzi huo mdogo unafanyika kuziba nafasi zilizoachwa wazi ikiwamo ya Maalim Seif aliyefariki dunia kwa Uviko-19.

“Kwa mujibu wa ibara za 84(4) na 116(4) za Katiba ya ACT Wazalendo (toleo la 2020) nafasi hiyo inapaswa kujazwa ndani ya miezi 12.

“Halmashauri Kuu ya Taifa kupitia kikao chake cha Oktoba 31, mwaka jana na kwa kuzingatia mamlaka yake chini ya ibara za 69(2) na 84(4) za Katiba ya Chama, ilipitisha azimio la kuitishwa mkutano mkuu maalumu wa uchaguzi.

“Lengo ni kujaza nafasi ya Mwenyekiti Taifa, Makamu Mwenyekiti Zanzibar na mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa kutoka Tanzania Bara Januari 29 mwaka huu,” alisema.

Alisema Kamati ya Uchaguzi ilitangaza kalenda ya kuchukua na kurejesha fomu kwa wanachama wenye nia, kuanzia tarehe 4 hadi 17 Januari 2022, ambapo hadi jumla ya wanachama 11 walitia nia ya kugombea nafasi tatu zilizotangazwa.

Mwenyekiti huyo, alitaja waliochukua fomu kugombea uenyekiti kuwa ni Duni kutoka Mjini Magharibi, Unguja na Hamad kutoka Ole, Kaskazini Pemba.

Bashange alisema katika nafasi ya Makamu Mwenyekiti, Zanzibar, waliochukua fomu ni Makamu wa Kwanza wa Rais wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ), Othman Masoud Othman kutoka jimbo la Pandani, Kaskazini Pemba na Juma Said Sanani wa Mjini Magharibi, Unguja.

Mwenyekiti huyo alitaja wanachama waliojitokeza kugombea ujumbe Halmashauri Kuu ya Taifa, Tanzania Bara, kuwa ni Chrisant Msipi wa Shinyanga, Ester Thomas, Fungo Godlove wa Dar es Salaam na Johnson Mauma wa Arusha.

Wengine ni Msafiri Mtemelwa wa Tabora, Jafet Masawe wa Kilimanjaro na Fidel Hemed wa Tabora.

Alisema baada ya uchukuaji fomu kukamilika, leo Kamati ya Uchaguzi itaandaa taarifa ya mchakato wote kwa ajili ya kikao cha Sekretarieti ya Kamati Kuu.

“Sekretarieti itakaa tarehe 22 Januari 2022 kupokea taarifa ya watia nia kutoka Kamati ya Uchaguzi na kuandaa kikao cha Kamati Kuu ambayo itakutana Januari 27 kuandaa mapendekezo ya uteuzi kwa Halmashauri Kuu ya Taifa,” alisema.

Bashange alisema Halmashauri Kuu ya Taifa itakutaka 28 Januari 2022 kufanya uteuzi wa mwisho wa wagombea uenyekiti, makamu uenyekiti na ujumbe wa Halmashauri Kuu Taifa.

“Kamati ya Uchaguzi baada ya kupata majina rasmi, itawatangaza kupitia mdahalo wa wazi siku hiyohiyo, na wagombea watajieleza, wataulizwa maswali na kuelezea madhumuni ya kugombea nafasi hizo,” alisema.

Mwenyekiti huyo alisema tarehe 29 Januari 2022 Mkutano Mkuu Maalumu wa Uchaguzi utafanyika katika ukumbi wa Mlimani City, Dar es Salaam na kufanya uchaguzi.

Alisema Kamati ya Uchaguzi imejizatiti kuhakikisha uchaguzi unaendeshwa kwa uhuru, haki, uwazi na kuaminika.

“Kamati ya Uchaguzi inatoa mwito kwa viongozi, wajumbe wa mkutano mkuu, watia nia wote na wanachama kwa ujumla, kutunza maadili ili kupatikana viongozi watakaojenga na kuimarisha ACT-Wazalendo kwa mustakabli mwema wa demokrasia nchini,” alisema.

Akizungumzia kauli hizo za ushindani wao kuleta mpasuko ndani ya chama, Hamad alisema anaamini katika haki na demokrasia, hivyo hatarajii kuona wakigawanyika kisa uchaguzi.

“Uchaguzi una matokeo mawili; kushinda na kushindwa, naamini kama mifumo ya haki na demokrasia itafuatwa, hakuna kitakachoharibika. Lakini pia hata mchakato wa kupitishwa kugombea bado,” alisema.

Duni alisema hafikirii kushindwa au kushinda kwake, kunaweza kusababisha mpasuko, akitolea mfano uchaguzi wa kumpata Maalim Seif, alishindana na Jeremia Maganja na hakuna mpasuko uliotokea.

“Kwenye nafasi ya kiongozi wa chama, Zitto Kabwe alishindana na Ismail Jussa, na mpaka sasa chama kina umoja na upendo, hivyo wanaofikiria kutokea mpasuko wameishiwa hoja,” alisema.

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Articles

Habari za SiasaMakala & Uchambuzi

Nani anasema kuna hasara ATCL?

Spread the loveRIPOTI za makusanyo na matumizi ya fedha katika Kampuni ya...

Habari za SiasaTangulizi

CAG: Wastaafu, wenza wao chanzo NHIF kufilisika

Spread the loveRIPOTI ya ukaguzi ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu...

Habari za SiasaTangulizi

Vikundi hewa 851 vyalamba bilioni 2.6 mikopo ya halmashauri

Spread the loveVIKUNDI hewa vya wajasirimali wadogo 851 kutoka katika halmashauri 19...

Habari za SiasaTangulizi

Mashirika matano yapata hasara mabilioni ya fedha

Spread the loveMASHIRIKA matano ya Serikali yanayojiendesha kibiashara, yamepata hasara ya mabilioni...

error: Content is protected !!