March 6, 2021

Uhuru hauna Mipaka

Wamiliki Simba kufanya maamuzi magumu

Spread the love

BAADA ya kutokuwa na mwenendo mzuri wa matokeo katika michezo miwili ya Ligi kuu Tanzania Bara, Bodi ya Wakurugenzi ndani ya Simba inatarajia kufanya maamuzi magumu katika kuamua hatma ya kibarua cha kocha mkuu wa klabu hiyo, Patrick  Aussems na msaidizi wake Masoud Djuma. Anaripoti Kelvin Mwaipungu  … (endelea).

Maamuzi hayo yanaweza kumuondoa mmoja wapo kati yao au wote kwa pamoja ili kuinusuru timu na matokeo mabovu baada ya kuonekana wawili hao kutokuwa na maelewano kiasi cha kusahindwa kufanya kazi pamoja.

Djuma ambaye ameachwa Dar es Salaam wakati kikosi hicho kiliposafiri kwenda kucheza michezo miwili ya ugenini dhidi ya Ndanda FC waliokwenda sare katika uwanja wa Nangwanda, Mtwara, na mwingine wa Mbao FC waliofungwa kwenye Uwanja wa CCM Kirumba, Mwanza.

Katika taarifa iliyotolewa na Mkuu wa kitengo cha Habari na Mawasiliano ya Simba, Haji Manara kupindia ukurasa wake kwenye mtandao wa kijamii wa Instagram alituma ujumbe wa kuomba radhi kwa mashabiki pamoja na wanachama wa klabu hiyo kutoka kwa bodi ya Wakurugenzi, Sekretalieti, wachezaji pamoja na benchi la ufundi huku wakitarajia kufanya maamuzi sahihi bila shinikizo lolote.

“Bodi ya wakurugenzi, sekretarieti, benchi la ufundi na wachezaji wa Simba wanaomba radhi mashabiki na wanachama wetu kwa matokeo ya leo. Tumeumia sote na tunawaomba mjue hii ni mechi ya nne tu. Tutafanya maamuzi sahihi bila pressure kwa maslahi makubwa ya timu na klabu nawaomba mtulie katika kipindi hiki.”

Simba ambayo mpaka sasa imecheza michezo minne na kupata alama saba na kushika nafasi ya tano kwenye msimamo wa Ligi Kuu Tanzania Bara inatarajia kusafiri kwenda Shinyanga kwenye mechi nyingine ya ugenini dhidi ya Mwadui inayotarajia kuchezwa siku ya Jumapili kwenye dimba la Mwadui Complex.

error: Content is protected !!