SERIKALI imesema kwa kipindi cha miaka saba kumekuwepo na ongezeko kubwa la walipa kodi kutoka milioni 2.2 mwaka 2015/16 hadi milioni 4.4 mwaka 2021/22. Anaripoti Mwandishi Wetu, Dar es Salaam … (endelea).
Hayo yameelezwa leo Jumatano tarehe 11 Januari, 2023 na Emmanuel Ezron Kaimu Mkurugenzi wa Sera na Utafiti kutoka Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) wakati akiwasilisha mada katika Kongamano la Kodi la Kitaifa lililofanyika jijini Dar es Salaam.
Amesema ulipaji kodi wa hiari unaangaliwa katika maeneo makuu manne ikiwemo usajili wa biashara, uwasilishaji wa returns, ulipaji wa kodi na kutoa taarifa sahihi za kodi.
“Kwa sasa hivi kumekuwa na mwenendo mzuri wa kuandikisha walipa kodi kuanzia mwaka 2015/16 tulikuwa na walipa kodi 2.2 Milioni ambao kufikia 2021/22 wamefikia 4.4 milioni,” amesema Ezron.
Amebainisha kuwa ongezeko hilo la walipa kodi lilienda sambamba na ongezeko la makusanyo ambapo Mamlaka hiyo iliweza kuongeza kutoka Sh 12.5 Trilioni mwaka 2015/16 na kufikia Sh 20.9 trilioni mwaka 2020/21.
Katika mwendelezo wa kuonyesha ulipaji kodi wa hiari amesema kwa kipindi cha miezi sita cha Julai hadi Desemba 2022 Mamlaka hiyo ilik usanya Sh 12.6 trilioni ambao ni ongezeko la asilimia 12.1 ikilinganishwa na mwaka uliopita.
“Matokeo yanatokana na uboreshaji wa mifumo ya TRA ya kielekroniki, uboreshaji wa mazingira ya biashara nchini, uboreshaji wa ulipaji kodi wa hiari, utatuzi wa migogoro ya kodi nje ya mahakama na kushughulikia kwa wakati malalamiko ya walipa kodi na kutoa elimu kwa walipa kodi,” amesema Ezron.
Amesema katika utendaji kazi huo kuna fursa na changamoto ambapo ametaja fursa kuwa ni pamoja na ukuaji mzuri wa uchumi unaotokana na biashara mtandao, utalii na shughuli za viwandani.
Pia amesema kumekuwepo na ushirikiano mzuri kati ya TRA na walipa kodi ambao umeongeza uhiari wa walipa kodi na kuongezeka kwa shughuli za uwekezaji kutoka nje na ndani na kuwezesha utekelezaji wa miradi mikubwa ya kimkakati kama vile Bwawa la Julius Nyerere.
Ametaja changamoto zilizopo kuwa ni uhiari mdogo wa kulipa kodi kwa baadhi ya wafanyabiashara na kuendelea kuwepo shughuli za magendo na ukwepaji kodi.
Walipa kodi kwa hiyari ni kina nani – ni pamoja na tozo kupitia miamala, akaunti za benki, vifurushi, LUKU, PAYE na kadhalika? Ni hiyari kweli??
Biashara za mamilioni zinafanyika kupitia sekta isiyo rasmi kama wamachinga na wakulima. Je hawa wanalipa kodi kweli?
Nyinyi TRA hebu tembeleeni kituo cha Azam pale Kariakoo muone je kuna risiti hapo?