Friday , 19 April 2024
Home Habari Mchanganyiko Waliovamia Msitu wa Morogoro kupangwa
Habari Mchanganyiko

Waliovamia Msitu wa Morogoro kupangwa

Spread the love

 

ZAIDI ya makazi 1214 ya watu waliovamia Msitu wa Morogoro uliopo chini ya Wakala wa Huduma za Misitu maarufu msitu wa kuni, yatalazimika kupangwa upya baada ya Serikali kuridhia kuwaachia kwa kuchangia gharama kidogo. Anaripoti Mwandishi Wetu, Morogoro … (endelea).

Makazi hayo ambayo yapo kwenye eneo la hekta 2000 yamejengwa na wananchi waliovamia eneo halali la msitu ulioanzishwa tangu mwaka 1953 ambao upo chini ya Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS).

Hata hivyo baada ya Serikali kupitia timu ya mawaziri nane kufanya tathimini ya eneo hilo walifanya uamuzi wa busara wa kutobomoa makazi hayo na badala yake yapangwe upya.

Akizungumza na wananchi wa eneo hilo hivi karibuni Mkuu wa Mkoa wa Morogoro, Fatma Mwassa, alisema msitu wa kuni ni eneo halali linalomilikiwa na TFS.

Alisema kipindi akiwa Mkuu wa wilaya ya Mvomero alilinda eneo hilo na hadi anaondoka mwaka 2011 eneo lilikuwa salama na halikuwa na nyumba hata moja.

Alisema hivi sasa eneo hilo limejengwa nyumba 1,214 na kusababisha ya mgogoro kuwa mkubwa uliofanya timu ya mawaziri nane kufika eneo hilo tarehe 26 Mei, 2022 kulikagua pamoja na maeneo mengine ya Morogoro ikiwemo safu ya Milima ya Uluguru.

“Wakaona hali ilivyokuwa mbaya na hifadhi ilivyovamiwa na walikwenda kumwelezea Rais (Rais Samia Suluhu Hassan) hali ilivyo.

“Walichukua kila kitu hadi picha za nyumba, picha za wamiliki pamoja na majira nukta,” alisema.

Alisema baada ya kumfikishia Rais Samia aliona si busara kuvunja nyumba hizo lakini waliokwisha kujenga tuwaache waendelee kuishi humo lakini eneo lipangwe.

Alisema maelekezo mengine yaliyotolewa na timu hiyo ni kwamba waliomo humo watakatiwa eneo la nyuma yake na atalipishwa kila mita ya mraba Sh 2,000.

“Wakati huo tayari majira nukta yameshachukuliwa lakini timu ikaja na maelekezo kwamba eneo wanalolitoa kutoka kwenye msitu wa hekta 32,000 ni hekta 5000 wanabakisha 27,000 na nusu watapewa wale waliokwisha kujenga na nusu watapewa wale wa milimani ili watoke milimani miti iweze kupandwa,” alisema.

Hata hivyo alisema jambo la kusikitisha baada ya kusikia hekta 5000 zinarudishwa, watu waliaanza kuuzia kwa kasi tena wakati mwingine kwa kutumia watendaji wa mjini ilihali eneo ni la Wilaya ya Mvomero.

“Watendaji hao wa mjini ni matapeli tu,” alisema.

Mwassa alisema barua ya maelekezo ya timu hiyo ilifika tarehe 18 Septemba, 2022 lakini cha kusikitisha zaidi kati ya Septemba hadi sasa eneo lile limeshajengwa nyumba 500.

“Unajua sasa msipojua ukweli wa haya mambo mkasikiliza tu manenoya mtaani na vyombo vya habari mtaona wananchi wameonewa,” alisema.

Alisema uvamizi ukiendelea Serikali itapata hasara kwa kutopata mapato ya mauzo ya eneo na pia eneo hilo litakuwa halijapangwa.

“Wananchi wa sasa wanajitambua wanataka ukweli na wanataka maendeleo, hizo pesa tutakazouza maeneo kule ndiyo zitatumika kupima na kupanga,” alisema.

Alisema hakuna mtu aliyeonewa, “wenyewe wanajua wamefanya uvamizi bila aibu nani atarudi kwa Rais kumwambia wamevamia tena.”

“Wale mnaonisakama Mkuu wa mkoa mnionee huruma, watu mmefanya uvamizi mimi sikuwepo na nimeambiwa niwaondoe.

“Tunakwenda kuwaonesha mpaka mpya ikiwa umeangukia upande ambao ndiyo tumeruhusiwa kuutumia, jua tutakupimia, tutakumilikisha lakini kwa kulipia. Ukiwa umeangukia kwenye hifadhi anza kuvunja mwenyewe chukua tofali lako moja moja tutii sheria bila shuruti,” alisema Mwassa.

Mkuu huyo wa mkoa alikemea vitendo vya kuvamia maeneo na kujenga bila kufuata sheria na utaratibu na kubainisha kuwa wengine wanaofanya hivyo ni maofisa wa Serikali amabao wana uelewa.

“Morogoro tuache mambo tunayofanya yanatia aibu, msifanye mambo ya hovyo halafu mkasingizia watu ubaya. Na kwenye ule msitu wengine ni maafisa wakubwa wa Serikali na wanajenga usiku sasa hao hawajui wanachofanya,” alisema.

Alibainisha kuwa ili kujenga nyumba ni lazima mwananchi awe na hati miliki ya Ardhi na pili kuwa kupata kibali cha ujenzi wa nyumba anayotaka kujenga na vyote hivyo vinapatikana Ofisi za Ardhi za Halmashauri husika na sio kwa Mtendaji wa Kijiji wala Mtaa.

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Articles

Habari Mchanganyiko

NEMC yaonya wanaojenga bila tathmini ya mazingira

Spread the loveBARAZA la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC),...

BiasharaHabari Mchanganyiko

NMB Pesa Akaunti yawavutia wakaguzi wa ndani Afrika

Spread the loveUbunifu wa bidhaa bora wa Benki ya NMB pamoja na...

Habari Mchanganyiko

Carbon First, Ruangwa wasaini makubaliano ya biashara ya hewa ukaa

Spread the love  KAMPUNI ya Carbon First Tanzania Limited na Halmashauri ya...

Habari Mchanganyiko

CBE yawakumbuka wenye mahitaji maalum Jangwani

Spread the loveCHUO cha Elimu ya Biashara (CBE), kimetoa msaada mbalimbali na...

error: Content is protected !!