August 10, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Waliotumbuliwa majibu wafikishwa kortini

Spread the love

VIGOGO watatu waliowahi kutumbuliwa ‘majipu’ na Rais John Magufuli katika Kampuni Hodhi ya Rasilimali za Reli Tanzania (RAHCO), wamepandishwa kizimbani kwenye Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu wakikabiliwa na mashitaka manane likiwemo la kusababisha hasara ya Dola za Marekani 527,540, anaandika Hamisi Mguta.

Vigogo hao ni Mhandisi Benhard Tito aliyekuwa Mkurugenzi Mkuu wa RAHCO; Kanji Myinyijuma, Raia wa Kenya anayedaiwa kuwa dalali wa zabuni Emmanuel Massawe ambaye yupo ndani ya bodi hiyo.

Vigogo hao waliotumbuliwa mwishoni mwa mwaka 2015 wamefikishwa mahakamani hapo leo wakiwa chini ya ulinzi mkali, kwa ajili ya kusomewa mashtaka yao nane yanayowakabili.

Kwa pamoja walisomewa mashtaka yao leo mbele ya Thomas Simba, Hakimu Mkazi Kisutu ambapo Thimos Vitalis, Wakili wa Serikali alidai kuwa shauri hilo ni jipya.

Alidai kuwa, shitaka la kwanza la kula njama kwa ajili ya kutenda kosa linawakabili washtakiwa wote, ambapo inadaiwa kati ya Septemba Mosi 2014 na Septemba 30, 2015 jijini Dar es Salaam walikula njama ya kutenda kosa kinyume cha sheria ya rushwa ya mwaka 2007.

Kosa la pili linalomkabili mshtakiwa wa kwanza Tito ni matumizi mabaya ya madaraka.

Mwanasheria Vitalis alidai kuwa kosa hilo lilitendwa Februari 27, 2015 katika ofisi za RAHCO zilizopo Ilala jijini Dar es Salaam baada ya kuidhinisha Kampuni ya Rothschild (South Africa) Property kuwa mshauri katika mpango wa ujenzi wa reli ya kati bila kuidhinishwa na Bodi ya Zabuni ya Kamapuni hiyo.

Mbali na hilo, shitaka la tatu linamkabili Tito na Massawe kutumia madaraka yao vibaya wakati wakiwa wanaitumikia Rahco.

Inadaiwa kwa pamoja Machi 12, 2015 katika ofisi za Rahco Ilala jijini Dar aes Salaam akiwa kama Mkurugenzi Mkuu wa Kampuni na Katibu wa RAHCO, walisaini barua ya kuhalalisha Kampuni ya Rothschild (South Africa) Property katika mchakato wa kutoa huduma ya ushauri wa kifedha katika ujenzi wa reli hiyo ya Kati bila kuidhinishwa na bodi.

Pia washitakiwa hao wanakabiliwa na shitaka la nne, ambapo inadaiwa Kati ya Machi 12 na Mei 20, 2015 wakiwa ofisini kwao Ilala Dar es Salaam waliacha majukumu yao kwa kushindwa kuwasilisha mkataba wa Kampuni ya Rothschild kwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG).

Pia wanakabiliwa na shtaka la tano, ambapo inadaiwa Mei 20, 2015 katika ofisi zao hizo zilizopo Ilala, walishindwa kutekeleza majukumu yao na kutumia vibaya madaraka kwa kusaini mkataba na kuingia makubariano na kampuni hiyo katika masuala ya ushauri.

Katika shtaka la sita Wakili Vitalis alidai kuwa, pia washtakiwa hao wanakabiliwa na kosa la matumizi mabaya ya madaraka kinyume na sheria ya kupambana na rushwa namba 11 ya mwaka 2007.

Inadaiwa kwa pamoja katika ya Mei 20 na June 20, 2015 katika ofisi zilizopo Ilala walishindwa kuwasilisha nakala za mkataba wa makubaliano wa kampuni hiyo na Kampuni ya Reli kwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG), Mkaguzi wa ndani na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA).

Mbali na hilo, shitaka la saba linawakabili washitakiwa wote ambapo inadaiwa kusababisha hasara, kosa hilo wanadaiwa kulitenda Kati ya Machi Mosi na Septemba 30, 2015 katika ofisi zao zilizopo Ilala Dar es Salaam.

Inadaiwa kuwa, wakiwa na mwakilishi wa kampuni hiyo na Katibu wa Rahco kwa pamoja walikubaliana kuidhinisha makubaliano ya kampuni hiyo katika masuala ya kiushauri na kuisababisha hasara ya dola za Kimarekani 527, 540 Kampuni ya Hodhi ya Reli Tanzania ambazo zilishalipiwa kiwango cha awali benki.

Shitaka la mwisho linamkabili mshtakiwa wa kwanza, Tito kwa matumizi mabaya ya madaraka kinyume na sheria ya kupambana na rushwa, ambapo inadaiwa Agosti 18, 2015 katika ofisi za Rahco Ilala alitumia nafasi yake vibaya kwa kutoa zabuni ya upendeleo kwa Kampuni ya Ujenzi wa Reli ya China Construction Corporation.

Inadaiwa katika zabuni hiyo kampuni ilipewe ujenzi wa reli ya Kilometa 2 yenye kiwango cha kisasa kuanzia Soga ikiwa na thamani ya dola za kimarekani 2, 312, 229.39 bila kuidhinishwa na Bodi ya Zabuni ya Reli.

Baada ya kueleza hayo, Wakili Vitalis aliieleza mahakama kuwa upelelezi wa shauri hilo bado haujakamilika hivyo anaomba kupangiwa tarehe kwa ajili ya kutajwa.

Hata hivyo, washtakiwa hao hawakutakiwa kujibu lolote kwa kuwa mahakama hiyo haina uwezo wa kusikiliza shauri hilo, jambo lililoibua mvutano wa kisheria kutoka upende wa utetezi.

Kutokana na kuibuka kwa mvutano wa kisheria, Hakimu Simba aliahirisha kesi hiyo hadi Machi 18, mwaka huu kwa ajili ya kutoa maamuzi kama washtakiwa watapewa dhamana ama kutopewa.

error: Content is protected !!