August 17, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Waliotesa machinga Mwanza kukiona

Stanslaus Mabula, Mbunge wa Jimbo la Nyamagana (CCM)

Spread the love

STANSLAUS Mabula, Mbunge wa Jimbo la Nyamagana (CCM) amesema kuwa, atawatafutia wanasheria wafanyabiashara ndogo ndogo (Machinga) kuwashitaki wakuu wa Wilaya za Nyamagana na Ilemela, anaandika Moses Mseti.

Wakuu hao ni Marry Tesha (Nyamagana) na Dk. Leonard Masale (Ilemela), mwingine atakayeunganishwa kwenye kesi hiyo anatajwa kuwa Kiomoni Kibamba, Mkurugenzi wa Jiji hilo kwa madai ya kuharibu bidhaa za machinga na kuvunja mabanda yao ya biashara.

Tarehe 3 Desemba mwaka huu, wakuu wa wilaya hizo na mkurugenzi huyo walifanya oparesheni ya kuwaondoa machinga mjini, kabla ya Rais John Magufuli kuagiza warejeshwe kuendelea na shughuli zao kama kawaida.

Mabula ametoa kauli hiyo leo wakati akihutumbia Wananchi katika mkutano wa hadhara uliofanyika kwenye Stendi ya gari ndogo ‘hiace’ Igoma Kata ya Igoma Wilaya ya Nyamagana jijini humo.

Mabula amesema kuwa, uamuzi wa kuwaondoa machinga hao kutoka katikati ya jiji ulichukuliwa na viongozi hao kwa kukurupuka huku akidai kuwa, hayupo tayari kuona machinga hao wakionewa akiangalia.

Pia amewataka Machinga kukaa na kuangalia ni athari ya bidhaa zao zilizoharibiwa pamoja na mabanda yao ili awatafutie wanasheria watakaowasaidia kufungua kesi mahakamani ili haki ipatikane.

“Machinga bidhaa zao zimeharibiwa sana, tunaomba Mwenyekiti wa Machinga (Said Tembo) mkae na mfanye tathimini ya bidhaa zenu zilizoharibiwa na baada ya hapo nitawatafutia wanasheria.

“Msimamo wangu ni kuhakikisha machinga wanatengewa maeneo yaliopo katikati ya jiji na sehemu ambayo ni rahisi kufikika na sio kuwapeleka kiloleli ambako hakufikiki,”amesema Mabula.

Hata hivyo, Mabula amesema kuwa baadhi ya viongozi wa serikali hususani wakuu wa wilaya wamemchukia kwa kuwatetea machinga hao huku akidai kwamba, (machinga) ndio waliomchagua.

Said Tembo, Mwenyekiti wa Machinga mkoani Mwanza amesema kuwa, baada ya Rais Magufuli kuwarudisha mjini, kilichobaki hivi sasa wanataka kulipwa mali zao na hawatakubali kuona wakidhulumiwa.

“Machinga wengi wamekopa fedha benki, lakini tukashangaa kuona Mkuu wa Wilaya (Marry Tesha) anakuja usiku wa manane kubomoa vibanda vyetu huku akidai kwamba, hataki kuona uchafu wa machinga mjini,” amesema Tembo.

Tembo amesema kuwa, kutokana na dharau zilizooneshwa na mkuu huyo wa wilaya, hivi sasa na wao wanaomba kurudishiwa mali zao na bidhaa zao huku akiunga mkono hatua za mbunge huyo kuwatafutia wanasheria kuwafikisha viongozi hao kortini.

error: Content is protected !!