Saturday , 15 June 2024
Home Gazeti Habari za Siasa Waliotekwa Pemba wapatikana, waelezea kilichowakuta
Habari za SiasaTangulizi

Waliotekwa Pemba wapatikana, waelezea kilichowakuta

Baadhi ya vijana waliotekwa baada ya kupatikana
Spread the love

VIJANA sita wa kijiji cha Mtambwe Mtambuuni, wilayani Wete Pemba, waliokuwa wametekwa mapema mwezi huu na watu wanaodhaniwa ni wa dola, wamepatikana. Anaripoti Jabir Idrissa … (endelea).

Vijana hao wamepatikana hai lakini hoi kwa uchovu na maumivu yatokanayo na kuteswa na watekaji wao.

Baada ya vijana watatu kupatikana wiki moja tangu walipotoweka kwao wakiwa wazima ingawa wanaonesha kufadhaika na kilichowakuta, wenzao watatu walipatikana jana wakiwa hawajitambui na waliojaa michubuko mgongoni inayoonesha walipigwa kwa kitu kama waya.

Taarifa kutoka kijijini Mtambwe Mtambuuni, zinasema hawa wa jana walikutwa maeneo tofauti msituni; wapo waliokutwa eneo la Mzambarauni, kilomita tano hivi kufika njiapanda ya Piki yalipo makutano ya barabara ya Chake-Wete na njia kuu ya kwendea Mtambwe.

Kiongozi wa Vijana wa Chama cha Wananchi (CUF) jimboni Mtambwe, Mohammed Khatib amesema vijana wawili ambao ni Thuweni Nassor Hemed na Khamis Abdalla Mattar walikutwa Mzambarauni.

Mwenzao aitwaye Khalid Khamis Hassan alikutwa Likoni, kando ya barabara I iendayo kisiwa kidogo cha Kojani, kilichoko kaskazini mashariki mwa kisiwa kikuu cha Pemba.

“Tumewapata hai lakini hali zao zi taabani, bila ya shaka, kutokana na mateso. Wamevimba miguu na mgongoni wana mavilio ya damu yatokanayo na kupigwa kitu kama waya,” alisema Khatibu.

“Tumewapeleka Hospitali ya Wete kwa uchunguzi na matibabu,” alisema.Taarifa za kupatikana vijana hao zimethibitishwa na Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kaskazini Pemba, ACP Haji Khamis Haji.

“Ninazo taarifa kuwa wamepatikana lakini kwa sasa wanafanyiwa uchunguzi hospitali ya Wete. Nitakuwa na taarifa zaidi kuhusu hali zao tukionana nao na kupata maelezo yao,” alisema.

Hospitali hiyo iliyopo mjini Wete, ni ya hadhi ya mkoa na inamilikiwa na Serikali ya Mapinduzi Zanzibar.

Mafanikio ya kuwapata yamekuja kwa ufuatiliaji uliofanywa na kikosi maalum cha vijana wa CUF.

“Tukiwa kwenye mizunguko ya kuwatafuta majira ya saa 8 usiku kuamkia Jumapili, tulimuona mtu kapanda baiskeli amepita kwa kasi na ghafla akatoweka tusimuone alikoelekea.

“Tulipofuata upande aliokimbilia ndipo tukakuta watu wawili wamelala kwenye majani kama wametupwa hivi. Kumbe ndio wenzetu waliotekwa,” alisema Khatibu kwa lugha nyepesi akionesha huzuni.

“Wamechoka na wamejeruhiwa na kudhoofika miili. Hawawezi kuzungumza kitu na miguu yao imevimba kiasi cha kutoweza kusimama,” alisema.

Thuweni Nassor Hemed, alikutwa Likoni, karibu na njia ya kwenda Kojani kisiwani.Kaka yake, Said Nassor Hemed, amesema haki ya ndugu yake “si nzuri. Hawezi kuongea; amepoteza uzito na mgongoni amejaa michubuko ya kupigwa kwa kutumia waya.”

“Yeye na wenzake wanatoka damu wanapojisaidia haja kubwa na ndogo. Hatujajua hasa kilichowasibu,” alisema.

Watu waliodhaniwa ni askari wa Usalama wa Taifa wakitumia gari mahsusi za serikali walifika Mtambwe Mtambuuni usiku wa saa 4 tarehe 4 Aprili mwaka huu na baada ya kuufunga mtaa na kupekua nyumba baada ya nyumba walitoweka na vijana sita wenye umri wa kati ya miaka 16 na 31.

Vijana watatu walipatikana pamoja siku nne baadaye kwenye kijiji cha Kengeja, Wilaya ya Mkoani, Kusini Pemba. Hali za vijana hao ambao wadogo kwa umri kuliko wenzao watatu, si mbaya.

“Hatukuteswa mwilini lakini tulihojiwa mara kwa mara masuala yasotuhusu kabisa. Waliotuhoji walijificha usoni na wakati mwengine sisi tulifungwa vitambaa usoni ili tusi wajumbe,” alinukuliwa mmoja wao akisema.

Hili ni tukio la kwanza la utekaji wa staili hiyo kwa Zanzibar katika kipindi cha karibuni cha kushamiri kwa matukio kama hayo Tanzania Bara. Matukio maarufu kwa Zanzibar ni yale yanayohusu askari wa vikosi vya SMZ kushambulia kqa vipigo wananchi nyakati za usiku.

Katikati ya mwaka jana, askari hao waliopachikwa jina la mazombi, walimuua Ali Juma, aliyekuwa ofisa habari na uenezi wa CUF wilaya ya Magharibi B.

Mazombi walimchukua baba huyo wa watoto 19 mkaazi wa Maoni Kidatu mjini Zanzibar chumbani kwake baada ya kuvunja mlango wa nyumba yake na kuingia ndani usiku.

Walimshambulia mbele ya familia yake na kuondoka naye huku wakimtupia matusi. Ali alipata fahamu alfajiri akiwa msitu wa Masingini, nje kidogo ya mji. Alipata msaada kwa kuchukuliwa na wachunga ng’ombe waliomkuta akilalama kwa maumivu.

Alifariki dunia siku iliyofuata kutokana na majeraha. Alipata kujieleza akisema alihujumiwa makusudi kwa sababu za kisiasa. “Tunadhulumiwa kwa kweli lakini nawaambia wenzangu tusikubali dhulma namna hii,” ilikuwa kauli ya mwisho akiwaeleza viongozi wa CUF waliofika nyumbani kwake kumkagua.

Polisi walisema hawakuripotiwa rasmi tukio hilo.

Written by
Jabir Idrissa

+255 774 226248

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Articles

BiasharaHabari za Siasa

Tanesco yawasha mtambo namba 8 Bwawa Julius Nyerere

Spread the loveNaibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dk. Doto Biteko...

Habari MchanganyikoHabari za SiasaTangulizi

Samia: Wakuu wa mikoa, wilaya wanaendeleza ubabe

Spread the loveRAIS Samia Suluhu Hassan amesema bado wakuu wa wilaya na...

Habari za SiasaKimataifaTangulizi

Ramaphosa achaguliwa tena kuwa rais Afrika Kusini

Spread the loveRais wa Afrika Kusini, Cyril Ramaphosa amechaguliwa na wabunge wa...

Habari za SiasaKimataifaTangulizi

DA, ANC waridhia kuunda serikali ya mseto Afrika Kusini

Spread the loveChama tawala nchini Afrika Kusini cha African National Congress, ANC,...

error: Content is protected !!