August 10, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Waliotakiwa kumrithi Mukandala hawa hapa

Profesa Allen Mushi Mkurugenzi wa Shahada za awali katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM)

Spread the love

PROFESA David Mfinanga, Prof. Allen Mushi na Prof. Bernadeta Kilian watalazimika kusubiri kwa mwaka mmoja zaidi ili kujua iwapo watavivaa viatu vya Prof. Rwekaza Mukandala katika nafasi ya Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) au la, anaandika Charles William.

Maprofesa hao watatu ndiyo waliopitishwa katika mchujo wa kurithi nafasi ya Prof. Mukandala kabla ya Dk. Jakaya Kikwete ambaye ni Mkuu wa UDSM kwa kushauriana na Rais John Magufuli kuamua kumuongezea Prof. Mukandala mkataba wa mwaka mmoja zaidi wa kutumikia nafasi hiyo mpaka tarehe 5 Desemba 2017.

“Mchujo ulianza mapema mwaka jana kabla hata serikali ya awamu ya nne kumaliza kipindi chake hata hivyo, tuliukamilisha mwaka huu na majina matatu ndiyo yalipitishwa katika hatua ya mwisho ambapo Mkuu wa Chuo (Dk. Kikwete) alikabidhiwa ili kumpelekea rais Magufuli,” kimeeleza chanzo cha kuaminika kutoka menejimenti ya chuo hicho.

MwanaHALISI Online imebaini kuwa kulikuwa na makundi makubwa mawili, yakiwapigia chapuo zaidi Prof. Mfinanga na Prof. Mushi katika nafasi ya Makamu Mkuu wa Chuo hicho huku Prof. Kiliani akipigiwa chapuo na kundi lililoonekana kuwa la ‘wapenda usawa wa kijinsia.’

Prof. Mfinanga ambaye kwa sasa ni Naibu Makamu Mkuu wa chuo – Utawala,  ndiye alikuwa akipewa nafasi kubwa zaidi kutokana na wasifu wake ‘kumbeba’,  huku wakosoaji wake wakitaja “uvumilivu na utatuzi wa migogoro kwa njia ya kidiplomasia zaidi” kama sifa inayomuweka rehani katika kurithi nafasi hiyo.

Ingawa mmoja kati ya wahadhiri chuoni hapo aliyekuwa akimpigia chapuo Prof. Mfinanga amesema, “Si mkali sana kama wengi wanavyosema ila hapendi mambo yakwame bila sababu. na huyu ndiye mtu anayehitajika.”

Ni sifa hiyo ya ‘ukali’ ndiyo ilichokuwa ikifanya baadhi kumpigia chapuo Prof. Mushi, ambaye ni Mkurugenzi wa Shahada za Awali chuoni hapo – akitajwa kama “mtulivu, msikilizaji mzuri na muumini wa maridhiano.”

Ingawa imeelezwa kuwa, “Prof. Mushi anadhaniwa kuwa mpole kwasababu nafasi yake si ya kiutawala zaidi.”

Prof. Bernadeta Kiliian ambaye kwa sasa ndiye Mkuu wa Chuo Kikuu kishiriki cha Elimu cha Mkwawa (MUCE), nafasi yake ilionekana kubebwa zaidi na uzoefu pamoja na shauku ya kuona usawa wa kijinsia katika nafasi za juu chuoni hapo.

Amewahi kushika nafasi mbalimbali chuoni hapo ikiwemo kuwa Mkuu wa Shule Kuu ya Habari na Mawasiliano kwa Umma (SJMC) na kwa kipindi kirefu amekuwa Mhadhiri katika Shule ya Elimu (SoED) iliyopo chuoni hapo.

Ni mwanaharakati wa masuala ya usawa wa kijinsia, akiwa kielelezo cha wanawake kuweza kusoma mpaka katika ngazi ya juu na kushika nafasi mbalimbali za uongozi.

error: Content is protected !!