WATU wanne wanashikiliwa na Jeshi la Polisi kwa kupendekeza majina ya viongozi wa serikali wanaotamani wafe kwa virusi vya corona (COVID-19). Anaripoti Mwandishi Wetu, Pwani…(endelea).
Taarifa hiyo imetolewa leo Jumatatu tarehe 22 Februari 2021 na Kamanda wa Polisi Mkoa wa Pwani, Wankyo Nyigesa wakati akizungumza na wanahabari.
Kamanda Nyigesa amewataja watuhumiwa hao kuwa ni Frank Nyange (47), Moses Mgao (34), Mohamed Lutambi (47) na Bumija Senkondo (54).
Nje ya kutuhumiwa kupendekeza majina ya viongozi wanaotamani wafe kwa Covid-19, watuhumiwa hao wanadaiwa kutumia mitandao ya kijamii kusambaza taarifa za uongo juu ya vifo vya baadhi ya watu, waliodai wamekufa kwa Covid-19.
Kamanda Nyigesa amesema, Jeshi la Polisi linaendelea kuwasaka watuhumiwa wengine wanaodaiwa kusambaza taarifa za uongo juu ya Covid-19.
“Watuhumiwa hawa wanne tuliowakamata na wengine ambao tunaendelea kuwatafuta, wanasambaza taarifa za uvumi juu ya vifo vya watu wanaodai wamekufa kwa Corona.
“Pia wanapendekeza majina ya viongozi wa serikali ambao walitamani wafe haraka kwa corona,” amesema Kamanda Nyigesa.
Kamanda huyo amewataka wananchi kujiepusha na matumizi mabaya ya mitandao ya kijamii, kwa kusambaza taarifa za uvumi kuhusu vifo vya watu.
Leave a comment