HALMASHAURI ya Wilaya ya Kilosa inatarajia kuwafikisha mahakamani watu 21 wanaodaiwa kujichukulia sheria mikononi na kujimilikisha hekari 66 za kijiji na kujenga nyumba za makazi kwenye eneo lililotengwa kwa ajili ya ujenzi wa soko, anaandika Christina Haule.
Kesi Mkambala mkurugenzi mtendaji wa halmashauri ya wilaya hiyo amekiambia kikao maalum cha baraza la madiwani kwamba tayari ameshaamuru nyumba zilizo katika eneo hilo kubomolewa huku watu waliohusika na uvamizi huowakiendelea kushikiliwa na polisi.
“Kundi dogo la watu 21 lilivamia na kujimilikisha eneo la hekari 98 lililoachwa na kijiji kilichopo kata ya Ruhembe. Kijiji kiliomba maeneo hayo na kufanikiwa kupata hekari 32 kati 98 na kufanya hekari 66 kubakia mikononi mwa kundi la watu 21,” amesema.
Mkambala amesema, watu hao wanatarajia kufikishwa mahakamani ili waachie hekari 66 zinazohusisha sehemu ya soko la kijiji na hivyo kuzuia maendeleo ya kijiji hicho.
Aidha Mkambala ameahidi kutembea kila eneo na kwamba endapo atabaini mtu kuvamia eneo lisilo lake atalivunja. “Migogoro haiishi bila kujitoa, nitaendelea kujitoa ili kumliza migogoro ya ardhi,” amesema.
Leave a comment