Spread the love

 

WALIOKUWA wajumbe wa Baraza Kuu la Chama cha Wananchi (CUF), wamehoji ukimya wa Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa, juu ya majibu ya malalamiko yao ya kupinga kutimuliwa ndani ya chama hicho. Anaripoti Mwandishi Wetu, Dar es Salaam…(endelea).

Maswali hayo yamehojiwa leo Jumatano, tarehe 29 Desemba 2021 na Abdul Kambaya, akizungumza na MwaanHALISI Online kwa niaba ya wanachama hao waliofukuzwa CUF na Baraza Kuu la Uongozi wa chama hicho, Novemba 2021.

Mbali na Kambaya, wanachama wengine wa CUF waliofukuzwa kwa tuhuma za kukiuka maadili ya chama hicho ni, Ahmed Hamis, Mohamed Vuai, Ali Makame, Mtumwa Ambari, Dhifaa Mohamed Bakari na Chande Jidawi.

Kambaya aliyewahi kuwa Naibu Mkurugenzi wa Habari, Uenezi, Uhusiano na Umma, amedai majibu yao yamekawia kwani walitarajia yatachukua muda mfupi.

Kama ofisi hiyo ilivyoshughulikia malalamiko yao dhidi ya aliyekuwa Katibu Mkuu wa CUF, Hayati Maalim Seif Shariff Hamad, ambapo anadai iliyajibu ndani ya mwezi mmoja na nusu.

Mwaka 2016, Kambaya pamoja na Mwenyekiti wa CUF, Prof. Ibrahim Lipumba, walitinga katika Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa, kupinga kufukuzwa na Baraza Kuu la Uongozi la chama hicho, chini ya Maalim Seif.

Ambapo ofisi hiyo ilibatilisha maamuzi hayo na kuendelea kumtambua Prof. Lipumba kama mwenyekiti wa chama hicho.

“Bado hatujapata majibu, maana kwa uzoefu wetu katika tukio lile la Maalim Seif, ametoa majibu ndani ya mwezi mmoja na nusu, lakini letu limeenda takribani miezi miwili, tumeandika barua tarehe 12 Novemba mpaka tarehe 12 Desemba na tarehe ya leo tunamaliza kama mwezi mmoja na nusu,” amedai Kambaya.

Alipoulizwa kama kuna jitihada zozote wamezifanya kutafuta suluhu na uongozi wa CUF, Kambaya amejibu akidai hakuna dalili za jambo hilo kutokea.

MwanaHALISI Online, imemtafuta kwa simu Naibu Msajili wa Vyama vya Siasa, Sixty Nyahoza, ili kufahamu suala hilo limefikia wapi, ambapo amejibu akisema linafanyiwa kazi.

Naibu Msajili wa Vyama vya Siasa, Sixty Nyahoza,

“ Malalamiko yako mengi, tunayashughulikia yote. Unajua kuyashughulikia ni mchakato, inaenda kwa mchakato na siwezi kukwambia lini litamalizika sababu watu wanajibu na msajili akiona kuna umuhimu awaite apate maelezo ya ziada,” amesema Nyahoza na kuongeza:

“Tunaomba mtuvumilie, jibu la msingi ni kwamba malalamiko yote yanafanyiwa kazi.”

Kambaya na wenzake waliwasilisha malalamiko yao katika ofisi hiyo, kupinga kutimuliwa CUF, wakidai mchakato uliotumika kuwafukuza haukuwa halali kwa kuwa katiba ya chama hicho ilikiukwa.

Katika malalamiko yao wanadai, hawakupewa nafasi ya kushiriki mchakato uliotumika kuwafukuza, ikiwemo kutoruhusiwa kupiga kura katika mkutano wa Baraza Kuu la Uongozi la chama hicho.

Pia, wanadai Kamati ya Nidhamu na Maadili ya CUF, iliyoandaa tuhuma dhidi yao haikuwa halali kwa kuwa haikutimiza akidi.

2 Responses

  1. Wanapo subiri wajue kuna mawili kuna kheli na shari lakini watakolo bahati kulipata ndio haki yao

  2. Wakati mwingine unahamia chama kingine.
    Kwa sasa mnasubiria migogoro yenu. CUF kimekuwa Chama cha Ufanyaji Fujo.
    Msajili, wakati umefika wa kukata zile pesa.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *