July 7, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Walioitosa CCM wapambisha kampeni

Spread the love

MAKADA wawili waliokihama Chama Cha Mapinduzi (CCM), mmoja akiwa waziri wa zamani na mwingine mwenyekiti wa mkoa, wamefanya kampeni ya nguvu ya kumtakia kura nyingi Edward Lowassa kwenye mkutano mkubwa wa kampeni jijini Mbeya jioni hii. Anaandika Jabir Idrissa … (endelea).

Makada hao ni Lawrence Masha aliyekuwa waziri wa Mambo ya Ndani katika serikali ya kwanza ya Rais Jakaya Kikwete kutoka Novemba 2005, na Khamis Mgeja aliyetoka akiwa mwenyekiti wa mkoa wa Shinyanga.

Wakati Mgeja amesihi Watanzania wapuuze ahadi za kilaghai za viongozi wa CCM, kwa kuwa hawana uwezo tena wakutumikia wananchi, Masha yeye alisema yeye na wenzake waliohama CCM wana akili timamu na walifuata upande wenye matumaini ya kweli kuwapatia maendeleo Watanzania.

“Sisi sio kweli kwamba hatuna akili kama wanavotuita. Yao ni jeuri tu ya madaraka yasiyoheshimu haki zenu wananchi. Tunawaambia hatukukosea kwani hatukukurupuka,” amesema Masha, ambaye katika mwaka 2010 aliangushwa katika ubunge jimbo la Nyamagana na Ezekiel Wenje.

Mgeja anayejulikana sana alivyo mfuasi mkubwa wa Lowassa, amesema CCM imeelekeza serikali ilipe madeni ya wafanyakazi wakati inadaiwa madeni makubwa haitaki kuyalipa. “Malipo ya sasa ni ulaghai wa kuwapumbaza wafanyakazi kwa ajili ya kulazimisha wawape kura. Wafanyakazi msikubali kulaghaiwa,” amesema.

Masha amesema anaijua vizuri Sheria ya Uchaguzi na haikatazi mpigakura kukaa nje ya mita 200 baada ya kupigakura yake. “Tukishapiga kura, tukae nje ya mita 200 ndivyo sheria inavyoelekeza. Msiwe na wasiwasi,” amesema.

Akichagiza kampeni, Meneja wa kampeni ya Lowassa anayeungwa mkono na Umoja wa Katiba ya Wananchi (UKAWA), John Mrema alisema serikali ya CCM imelipa askari polisi posho ya Sh. 300,000 kutoka Sh. 180,000 lakini ifikapo Novemba hawataendelea kwa kuwa hakuna bajeti hiyo.

“Katika bajeti iliyopitishwa Julai 2015, hakuna nyongeza ya posho ya Polisi. Kwa hivyo wakishafika Novemba watasema posho ile basi kwa sababu hakuna bajeti yake. Msiwasikilize kwa hivyo unganeni nasi katika kuleta mabadiliko, tuwaondoe na kutarajia serikali mpya ya UKAWA iongeze maslahi yenu mbalimbali,” amesema.

Lowassa ameanza ziara leo kwa kuhutubia mkutano wa kiporo mji mdogo wa Tunduma, ambako alishindwa kuhutubia jana kutokana na mitambo ya kupaza sauti kukorofisha. Baadaye alikwenda Kyela, Mbarali, Ileje majimbo ya mkoani Mbeya, ndipo akawasili jijini Mbeya.

error: Content is protected !!