RAIS Samia Suluhu Hassan, amesema wanafunzi zaidi ya 3,000 walioacha masomo kwasababu mbalimbali, wamerejea masomoni baada ya Serikali yake kutoa muongozo wa namna ya kurudi shule. Anaripoti Regina Mkonde, Dar es Salaam … (endelea).
Rais Samia ametoa kauli hiyo kupitia mahojiano yake na Kituo cha Televisheni cha Azam, yaliyorushwa leo Jumatano, tarehe 4 Mei 2022.
Mkuu huyo wa nchi, amesema wanafunzi 909 wa kike na wa kiume, walioacha masomo kwa sababu mbalimbali ikiwemo kupata ujauzito wakiwa shuleni, wamerejea masomoni katika shule za kawaida, huku 3,000 wakijunga na vyuo vya ufundi stadi ikiwemo VETA.
Rais Samia amesema, Serikali yake imetoa muongozo huo ili kufuta doa lililowekwa kwa Tanzania na ulimwengu , ya kwamba inanyima haki ya wanafunzi hao kurudi shule hususan wasichana wanaokutana na changamoto ya kupata ujauzito wakiwa shule.
“Nilipokuja tukalikataa suala hili, nikaona kwa nini tugombane na ulimwengu tujitie doa. Na uzuri mimi nilisema wanafunzi wote, sababu kuna wavulana waliacha shule wako wanajutia walichokifanya nilisema wote walioacha shule warudi,” amesema Rais Samia.
Aidha, Rais Samia amesema wadau mbalimbali wanaendelea na zoezi la uchukuaji maoni kuhusu marekebisho ya vipengele vya Sheria ya Ndoa, vinavyohamasisha ndoa za utotoni.
“Maoni ya wadau yanaendelea kuchukuliwa, waangalie kwa vizuri waone njia sababu jambo hili linaangaliwa zaidi na viongozi wa taasisi za dini, kuna dini zinasema mtoto akishabalehe kama anaweza kuolewa aolewe, sasa ukitoa kauli wanaweza sema hawa wanavunja dini yetu,” amesema Rais Samia.
Leave a comment