January 23, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Walimu wavamia ofisi ya Mkurugenzi, kudai fedha zao

Spread the love

SHUGHULI katika Ofisi za Jiji la Mwanza, jana zilisimama kwa muda wa saa 6, baada ya Walimu zaidi ya 300 kuandamana hadi katika ofisi hizo, wakidai kulipwa fedha zao. Anaandika Moses Mseti, Mwanza … (endelea).

Walimu hao wanaidai Serikali Sh. 696. 2 milioni, zikiwa ni fedha za malimbikizo ya mishahara, kujikimu, likizo, posho na madai ya walimu kutopandishwa madaraja.

Hata hivyo baada ya Walimu hao kutinga katika Ofisi za Jiji la Mwanza saa 3:15 asubuhi, mgambo wa Jiji waliwazuia na kusababisha mvutano mkali uliopelekea Askari polisi kufika kuongeza nguvu.

Jitihada za uongozi wa Jiji za kuwazuia walimu wasiingie katika ofisi hizo, zilishindikana baada ya Mkurugenzi wa Jiji, Khalifa Hida, kuwataka mgambo wawaruhusu viongozi kuingia kufanya mazungumzo.

Walimu hao waliokuwa wakiimba nyimbo za ukombozi wa kubadilisha mfumo uliopo kwa sasa ambao unaonekana kuwa kandamizi, walitia `nanga` ofisini hapo hadi saa 8:00 bila mwafaka wowote.

Katika kile kilichoonekana mkurugenzi wa Jiji hilo kutojiamini ni pale alipowaita waandishi wa habari ofisini kwake, ili kuzungumza nao juu ya madai lakini Walimu hao walikataa wakishinikiza azungumze mbele yao.

Mwenyekiti wa Chama cha Walimu Wilaya ya Nyamagana (CWT), Laurence Mkamwa amesema kitendo cha Hida kushindwa kuiwapa majibu kinaonesha ni namna gani hajiamini na Serikali yake.

Mkamwa amesema mpaka sasa katika ya fedha hizo wanazoidai serikali ni Sh. 10 milioni pekee zilizolipwa kwa mwaka 2015 licha ya kuidai Sh. 696.2 milioni.

Pia Walimu hao wameilalamikia Serikali kwa kitendo chake cha Baraza la Madiwani la Jiji kuwapandisha madaraja, ambapo ni kinyume na sheria ya utumishi wa umma kwani TSD ndio yenye jukumu hilo.

“Tulipokea barua Juni 30 mwaka huu, ikionesha eti baraza la madiwani kutupandisha madaraja walimu, tukajiuliza ni lini baraza la madiwani limewapandisha Walimu madaraja ni wapi na wapi kitu kama hicho kilisha fanyika,”alihoji Mkamwa.

Mkurugenzi wa Jiji la Mwanza, Hida alikwenda kinyume na walimu hao kwa kiasi cha fedha wanachokidai akisema ni Sh. 100 milioni pekee.

Hida amesema, “Ni kweli wanaidai serikali na kiwango kinachodaiwa ni zaidi ya Sh. 100 milioni na hatua zinaendelea za kufanywa na wanahakiki ili wawezwe kulipwa.”

error: Content is protected !!