January 23, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Walimu wamshika shati Rais Magufuli

Spread the love

CHAMA cha walimu wilayani Bahi mkoani Dodoma (CWT), kimemtaka Rais Dk, John Magufuli, kuhakikisha anasimamia madeni ya walimu wanayoyadai kwa kipindi kirefu ili waweze kulipwa katika awamu hii ya tano ili waweze kusimamia kwa ufanisi dhana ya utoaji elimu bure. Anaandika Dany Tibason, Bahi … (endelea).

Rai hiyo ilitolewa na Mwenyekiti wa chama hicho wilayani Bahi, Samwel Mlugu, wakati alipokuwa akizungumza na waandhishi wa habari mjini hapa mara baada ya hafla fupi ya kuwapatia msaada wa mabati walimu wastaafu.

Mlugu amesema kuwa anatoa wito kwa Rais Dk. Magufuli kuhakikisha anatumia kipindi chake cha uongozi kuwalipa walimu madeni yao ambayo yameshindikana kulipwa katika awamu mbalimbali zilizopita.

Amesema kuwa kutokana na madeni ya walimu kuwa ya muda mrefu yamekuwa yakiongezeka kila siku na kuwafanya walimu kuendelea kulalamika bila kilio chao kutatuliwa na uongozi uliokuwepo madarakani.

“Wakati huu serikali inaenda kutekeleza utoaji wa elimu bure kwa wanafunzi wa kuanzia shule ya msingi hadi kidato cha nne tunamuomba Rais wetu Dk. Magufuli kuhakikisha madeni ya walimu yote yanalipwa ili kuweza kuwaongezea ari ya kufanya kazi walimu ambao kwa kiasi kikubwa walikata tamaa,” amesema Mlugu.

Aidha amesema kuwa katika wilaya yake anayoiongoza walimu wanadai jumla ya Sh. 88,060,474 ambazo ni fedha za likizo, uhamisho, posho ajira mpya, nauli na zile za wastaafu na zinginezo.

“Ni madeni ya muda mrefu sana ambayo tunayapigia kelele kila siku lakini serikali haitaki kusikia, kuna wengine wamekwenda likizo toka mwezi Juni mwaka huu lakini hadi leo hii tunamaliza mwaka hawajalipwa fedha zao,” amesema Mlugu.

Naye mwalimu Iddi Nahato, amesema kuwa pamoja serikali kulipa madeni hayo lakini pia itatakiwa kuboresha mishahara ya walimu pamoja na kuwapatia motisha ili kuweza kuongeza ufanisi kazini.

Nahato amesema kuwa serikali ya awamu ya tano chini ya Rais Mgufuli inatakiwa kuwa na ubunifu kwa walimu ili kuweza kuondoa manung’uniko ambayo yamekuwepo kila siku kwa walimu hali iliyokuwa kwa kiasi fulani inachangia kushuka kwa elimu.

“Kuwepo na utaratibu hata wa kuwapatia vyeti au motisha fulani walimu wanajituma na kuonyesha jitihada katika utumishi wao ili kuamusha moyo wa kujituma zaidi lakini pia suala la madeni limalizwe serikali ilipe walimu wote wanaoidai,” amesema Nahato.

Kwa upande wake mwalimu Lydia Ndyetabula, amesema kuwa Rais Magufuli awatumia viongozi wake aliowachagua katika wizara ya Elimu kuchunguza suala la madeni na kiini chake ili kuweza kuliondoa kabisa.

“Kaulimbiu ya Rais inasema hapa kazi tu basi na sisi walimu tufanye kazi siyo kudai haki bila kutimiza wajibu wetu lakini pia niwaombe wazazi kupitia elimu bure iliyoanzishwa na serikali wasiendele kuwaficha watoto wao wawapeleke shule kwani elimu ni bure kwa wote sasa,” amesema Ndyetabula.

error: Content is protected !!