January 23, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Walimu wamkaba koo Lusinde

Spread the love

CHAMA cha Walimu Tanzania (CWT) tawi la shule ya sekondari Mvumi Makulu, Dodoma, kimetoa siku tatu kwa mgombea ubunge wa jimbo la Mtera Livingston Lusinde (CCM), kuomba radhi kutokana na kitendo chake kuwatukana walimu na kuwadhalilisha. Anaandika Dany Tibason, Mtera … (endelea).

Kwa mujibu wa mwenyekiti wa kikao cha makubaliano, Sospeter Langiboli siku ya Jumamosi Oktoba 3, mwaka huu Lusinde akiwa katika mkutano wa hadhara aliwashambulia walimu wa wilaya ya Chamwino kwa madai kwamba hawana akili na wanatakiwa kurudi darasani upya.

“Katika mkutano wa kampeni uliofanyika eneo la tangamano Mvumi Makulu, Lusinde akiwa jukwaani alitushambulia walimu kwa madai kwamba sisi hatuna akili kwamba ni wajinga na tunatakiwa kurudi darasani kujifunza upya.

“Kama hiyo haitoshi Lusinde anasema kuwa sisi walimu hatuna akili na hatujitambui, ndiyo maana hata serikali haituthamini kwa sababu ya ujinga wetu,” alieleza Langiboli.

Akitoa ufafanuzi zaidi Langiboli, amesema kitendo cha Lusinde kuwashambulia walimu na kudai kwamba yupo tayari kuwapeleka shule kimewafanya kudharauliwa na wanafunzi pindi wanapokuwa madarasani.

Amesema kwa sasa walimu wa shule ya msingi ya Mvumi Makulu pamoja na walimu wengine katika wilaya ya Chamwino wanamtaka Lusinde kuitisha mkutano wa hadhara ili kuwaomba walimu hao radhi na endapo hata fanya hivyo, hatua zaidi zaitachukuliwa dhidi yake.

Aidha, Langiboli amesema CWT tawi la shule ya sekondari ya Mvumi Makulu, umemwandikia barua Mkurugenzi wa halmashauri ya Chamwino, katibu wa CWT wilaya ya Chamwino kuhusu malalamiko hayo.

Wengine waliyopatiwa nakala ya barua ya malalamiko ni hayo ni Mwenyekiti wa Bodi pamoja na Afisa Elimu Kata ya Mvumi Makulu.

Mwanahalisi Online ilibahatika kupata moja ya nakala ya barua zilizopelekwa kwa watajwa wote ambapo kikao cha walimu wapatao 21 walikubaliana kwamba Lusinde aitishe mkutano wa hadhara kwa ajili ya kuwaomba radhi.

Kwa upande wake, Katibu wa CWT wilaya ya Chamwino, James Puya alikiri kupokea barua hiyo kutoka kwa uongozi wa shule ya sekondari ya Mvumi Makulu.

Mbali na kukubali kupokea barua hiyo pia amelaani kitendo cha Mgombea ubunge huyo kutumia majukwaa ya kisiasa kuwashambulia walimu.

Amesema kitendo hicho ni utovu wa nidhamu na ni jambo la kuwavunja moyo walimu na kuwafanya washindwe kuwafundisha wanafunzi.

Puya amesema barua hiyo ya malalamiko pamoja na muktasari wa kikao cha walimu hao inamtaka Lusinde aitishe mkutano wa hadhara na kuwaomba radhi.

Naye Mkuu wa Shule hiyo, Mohamad Ally Mohamed, amesema kitendo cha mgombea ubunge kuwashambulia walimu ni kitendo ambacho kinalenga kuwakatisha tamaa walimu na kuwafanya washindwe kufanya kazi zao kwa moyo mmoja.

Kwa historia Lusinde ni kati ya wana CCM ambao wanasifika sana kwa matusi na lugha chafu bila kujali anayemtunaka au kumkashifu ni mtu wa rika gani.

error: Content is protected !!