June 30, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Walimu wagoma TIU

Spread the love

Na Faki Sosi

WALIMU wa Chuo cha Kimataifa cha Tanzania (TIU) kilichopo Kimara Stop-Over, Dar es Salaam, wamegoma kuingia darasani kwa muda wa mwezi mmoja kutokana na kutolipwa malimbikizo ya mishahara yao pamoja na kutopewa mikataba ya kazi.

Madarasa yamefungwa, walimu wamo ofisini. Walimu waliozungumza na MwanaHALISI online wamesema kuwa madai yao ni mkataba wa kisheria wa makubaliano ya kazi, ambao wamenyimwa kwa muda mrefu, kutolipwa malimbikizo ya mishahara ya miezi saba, kukatwa kodi bila kuingiziwa fedha hizo kwenye mfuko wa hifadhi ya jamii na kutotambulika kuwa wao ni wafanyakazi.

Mpayu Irenistina, mwalimu chuoni hapo tangu 2014, amesema walimu wamegoma kwa kuwa hawajajua hatima yao. Wapo wasiolipwa mishahara. Hata inapolipwa, si kwa wakati.

Amesema walichukua hatua za awali kufanya vikao na uongozi wa chuo, lakini vikao havijazaa matunda. Tayari wamepeleka malalamiko yao kwenye baraza la usuluhishi.

Salome Ponela, mhadhiri kwenye chuo hicho ambaye anadai mshahara wa miezi mine, bado hajajua kama atalipwa, kwani mkuu wa chuo amekuwa kigeugeu katika suala la malipo.

Ernest Kayumba, rais wa wanafunzi, amesema walimu wao wamegoma kwa sababu ya kutolipwa mishahara, na kwamba hali hii itaathiri wanafunzi wanaomaliza muhula, wanaopaswa kufanya mitihani ya kumaliza ngazi ya stashahada ili wapate nafasi ya kujiunga na vyuo vikuu.

Amesema kuwa alifanya jitihada za kukaa na uongozi wa chuo, akapewa ahadi kuwa walimu wangeingia darasani.

Profesa Askofu Israel Wandamba, mkuu wa chuo hicho, hakupatikana. Alipoulizwa kuhusu suala hilo, Dk. Samwel Msava, makamu mkuu wa chuo, alisema, “nipo msibani, nitafute saa mbili usiku.”

error: Content is protected !!