RAIS wa Tanzania Samia Suluhu Hassan ametoa wito kwa walimu wote nchini kuacha kufundisha kwa mazoea na badala yake wajifunze mbinu mpya za kufundisha. Anaripoti Mwandishi Wetu, Zanzibar … (endelea).
Mkuu huyo wa nchi ametoa wito huo leo Jumanne tarehe 10 Januari, 2023 wakati wa ufunguzi wa skuli ya Msingi ya Mwanakwerekwe ikiwa ni maadhimisho ya miaka 59 ya Mapinduzi Matukufu ya Zanzibar.
Mbali na walimu pia Rais Samia amesisitiza haja ya kufanya mabadiliko ya mitaala ya elimu ili wanafunzi waweze kuchukua masomo machache yatakayowasaidia kuwa na ujuzi wa kutosha kuliko kuchukua masomo mengi ambayo mwishoni humchanganya.
“Jack of all master of none,” Rais Samia ametumia nahau hiyo ya Kiingereza kuonesha namna mwanafunzi anayebeba masomo mengi asivyoweza kumudu somo lolote.
Pia Rais Samia ametoa wito kwa wazazi na walezi kuwa makini na matumizi ya simu ya watoto wao na kuhakikisha kuwa wanazitumia katika kujifunza zaidi kuliko masuala ya burudani.
Shule hiyo ambayo imepewa jina la Dk. Samia itakuwa na uwezo wa kuchukua wananfunzi 1,300 na imejengwa kwa Sh 4 bilioni ikiwa ni matumizi ya fedha za nafuu ya Uviko-19.
Rais Samia amejitolea kuwa mlezi wa shule hiyo pamoja na iliyopo jirani na hiyo ya Dk. Magufuli ambapo amesema itafunguliwa akaunti maalum na kwa kuanzia ameweka Sh 20 milioni kwaajili ya kuhudumia shule hizo mbili.
Amesisitiza walimu kuhakikisha uzuri wa jengo hilo la ghorofa, unaendana na kile kitakachozalishwa hapo kwa maana ya matokeo mazuri ya wanafunzi.
Leave a comment