January 28, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Walimu Arusha waidai Serikali bil 4, waipa wiki mbili

Spread the love

CHAMA cha Walimu mkoa wa Arusha (CWT-Arusha) wamelalamikia serikali na kuitaka kutekeleza kwa wakati madeni yao la zaidi ya Sh. 4 billioni kwani yamekuwa kikwazo katika ufanisi wa kazi hali ambayo inapelekea kushusha kiwango cha elimu nchini. Anaandika Ferdinand Shayo, Arusha … (endelea).

Akizungumza na waandishi wa habari, Mwenyekiti wa CWT mkoa wa Arusha, Mwalimu Juvin Kuyenga amesema walimu wa mkoa wa Arusha wanadai madeni makubwa sana hali inayosababisha kuvunjika moyo katika utendaji wa kazi.

Mwalimu Kuyenga ametaja madeni hayo katika halmashauri mkoani Arusha ni Jiji la Arusha wanadai Sh. 987,689,00, Arumeru Sh. 2,996,607,848.21, Karatu Sh. 423,983,820, Longido Sh. 171,112,680, Ngorongoro Sh. 169,000,000, na Monduli Sh. 135,832,000.

Amesema madeni haya yanatokana na madai mbalimbali ikiwa ni pamoja na malimbikizo ya mishahara, mafunzo, uhamisho, matibabu na likizo na mapunjo ya mshahara, kitu ambacho kimekuwa kero na kusababisha walimu kuzichukia kazi zao.

Amesema kuwa walimu wamekuwa wakibaki kwenye daraja moja kwa muda mrefu kati ya walimu 12,319 waliopo Arusha walimu 5,364 wamegota kwenye madaraja yao na bado hawajafunguliwa pamoja na serikali kutoa waraka wa kufungua madaraja tangu Julai 2014.

“Posho ya madaraka kwa viongozi wa elimu, wakuu wa shule, wakuu wa vyuo kutokana na waraka wa seriakali uliotolewa mwaka jana posho hiyo ilitakiwa ianze kutolewa kuanzia Julai mwaka huu, lakini hadi sasa bado haijanza ,” amesema Mwalimu Kuyenga.

Walimu Kuyenga ameilalamikia serikali kuchelewesha malipo kwa wastaafu, kwani kuna walimu 67 waliostaafu Januari lakini hajalipwa mafao yao hali inayosababisha waishi katika mateso.

“Tunaidai serikali sababu tunapowasiliana na hawa wa mifuko ya hifadhi za jamii inasema serikali bado haijawarejesha michango ya walimu, danadana hizi zinawafanya walimu kuona haki zao zinanyonywa kwani utasababisha ufanisi kuwa mdogo makazini,” amesema Mwalimu Kuyenga.

Kwa upande wake Katibu wa CWT mkoa wa Arusha, Mwalimu Hassan Saidi amesema chama hicho kimetoa wiki mbili kwa waajiri wa halmashauri zilizopo mkoa wa Arusha kuwarudisha majumbani walimu waliostaafu na wanaostaafu na wasipofanya hivyo watawachukulia hatua za kisheria.

Mwalimu Saidi, amewataka wagombea wa urais kutazama vipaumbele muhimu vya walimu badala ya kujinadi kuwapa kompyuta mpakato (laptop) wakati wana mahitaji ya msingi zaidi ya hayo ikiwa ni pamoja na mishahara isiyokidhi mahitaji ya walimu na kurejeshwa na kwa posho ya kufundishia kwa walimu.

error: Content is protected !!