August 12, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Wala rushwa kunaswa ‘kiulaini’

Spread the love

WALA na watoa rushwa nchini wamepatiwa dawa. Ni baada ya kuzinduliwa kwa Kampeni ya Longa na Takukuru itakayomwezesha raia yoyote kumnasa mla rushwa, anaandika Regina Mkonde.

Kampeni hiyo inatoa fursa kwa wananchi kutoa taarifa za wala na watoa rushwa kupitia njia ya kutuma ujumbe na kupiga simu. Mtu anayepiga atatumia namba *113# bila malipo na kwa njia ya ujumbe mfupi wa maneno atatumia namba 113 bila malipo.

Kampeni hiyo imezinduliwa kutokana na serikali hupoteza mapato kutokana na baadhi ya watumishi wa halmashauri na taasisi zenye dhamana ya kukusanya kodi kuchukua rushwa kwa wafanyabiashara wasio waaminifu.

Hayo yamesemwa leo na Samia Suluhu, Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania wakati akizindua kampeni hiyo iliyoandaliwa na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) jijini Dar es Salaam.

“Rushwa huikosesha serikali mapato kwa sababu baadhi ya watumishi huchukua hongo kutoka kwa wafanyabiashara wasio waaminifu hivyo wafanyabiashara huishia kulipa kodi kidogo tu kwa serikali,” amesema.

Suluhu ameitaja Halmashauri ya Manispaa ya Kinondoni kuwa moja kati ya halmashauri zilizokithiri watumishi wa aina hiyo na kwamba, vile vile katika halmashauri nyingi nchini hakuna kumbukumbu za majina ya wafanyabiashara wanaolipa kodi.

“Ndani ya halmashauri zetu hakuna kumbukumbu za majina ya wafanyabiashara wa mabango ya matangazo ya barabarani na kama zipo basi ni za mabango machache na si yote,” amesema.

Amesema, licha ya kutokuwepo kwa kumbukumbu za majina ya wafanyabiashara wanaolipa kodi katika baadhi ya halmashauri, bado zipo nyingine zinazofuta majina ya wafanyabioashara wenye madeni makubwa na kuwasajiri na kuwa kama wafanyabiashara wapya.

“Vile vile wapo baadhi ya watumishi wa umma kwenye halmashauri zetu ambao wanawafuta wafanyabiashara katika kitabu cha orodha ya wafanyabiashara wenye madeni makubwa na kuwafanya wateja wapya,” amesema na kuongeza.

“Wafanyabiashara wanapotaka leseni wanaambiwa kuwa vitabu vya leseni vimeisha wakati vipo kwa lengo la kupata rushwa ndipo watoe leseni.”

Aidha, Suluhu amesema kuwa, kuna baadhi ya wafanyabiashara wasiotoa stakabadhi kwa lengo la kutokatwa kodi huku wakitoa masharti magumu kwa wateja ili wafanye maamuzi ya kununua bidhaa bila ya kudai risiti.

“Kuna wafanyabiashara hawataki kutoa stakabadhi na kuwaambia wananchi kauli zinazowakatisha tamaa ili wakubali kununua bidhaa bila ya kudai stakabadhi na kwamba, kama mwananchi anakutana na changamoto hiyo atumie namba za Takukuru kutoa taarifa ili wachukuliwe hatua,” amesema.

Amesema, serikali ikikosa fedha haitaweza kutekeleza mipango yake ya maendeleo ya kijamii na kiuchumi na haitakuwa imara bali itaishia kuwa ombaomba na kukubali masharti yoyote hata yale yanayohatarisha ustawi wa nchi na watu wake.

“Bado tunayo mapungufu mengi katika karibu kila sekta, ya elimu, afya, maji, kilimo, viwanda na miundombinu, hivyo tukicheka na wala rushwa hatutafanikisha lolote kati ya tuliyoyaahidi,” amesema Samia.

Suluhu ametoa agizo kwa wakurugenzi na wasaidizi wote katika mikoa wa Takukuru kushughulikia taarifa za kweli za wala rushwa ili kuwapa moyo wananchi kwa kujua kuwa taarifa wanazotoa zinafanyiwa kazi.

error: Content is protected !!