January 25, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Wakurugenzi wanne MSD wapigwa ‘stop’

Spread the love

UMMY Mwalimu, Waziri wa Afya, Maendeleo, Jinsia na Watoto amewasimamisha kazi wakurugenzi wanne wa Bohari Kuu ya Dawa nchini (MSD) kwa shutuma za ubadhirifu wa Sh. 1.5 bilioni, anaandika Regina Mkonde.

Waliosimamishwa ni Heri Mchunga, Mkurugenzi wa Manunuzi; Cosmas Mwaifwani, Mkurugenzi wa Kanda na Huduma kwa Wateja; Joseph Tesha, Mkurugenzi wa Fedha na Mipango pia Misanja Muja, Mkurugenzi wa Ugavi.

Waziri huyo amemtaka Laurean Bwanakunu, Mkurugenzi Mkuu wa MSD kuwapa barua za kuwasimamisha kazi wakurugenzi hao ili kupisha uchunguzi.

Ummy ametoa agizo hilo leo jijini Dar es Salaam wakati akipokea vifaa tiba kwenye jengo jipya la mama na mtoto lililopo katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili.

Amesema, hatokubali kuachishwa kazi wala kuwafumbia macho watumishi wa sekta ya afya watakaobainika kufanya makosa hasa ubadhirifu wa fedha na mali za umma.

“Wakuu wa Wilaya, Mikoa, Wakurugenzi na Katibu Mkuu wa Afya waache kukaa ofisini na kusafiri nje, wazunguke nchi nzima kwenye hospitali zao ili wakaangalie kama huduma zinazotolewa ni bora, kama si bora watoe taarifa ili tuzitatue changamoto hizo,” amesema na kuongeza;

“Sitalala hadi nipate taarifa kutoka kwa Katibu Mkuu wa Afya ya Maendeleo ya Huduma za Afya nchini kote, kila hospitali ihakikishe ina vitanda vya kutosha na vifaa tiba, kama kuna changamoto zozote zibainishwe mapema ili wizara ijue inazitatuaje.”

Ummy pia amepokea vifaa tiba vyenye thamani ya Shilingi 88,793,000 kutoka kwa Bwanakunu ikiwa ni utekelezaji wa agizo la Rais John Magufuli alilolitoa kwenye mkutano wa wazee wa Dar es Salaam tarehe 13 Februari mwaka huu.

“Nimepokea vitanda 120, mashuka 480, vitanda vya kuzalia wajawazito 10, vitanda vya kulalia watoto njiti 10 na magodoro 120 kutoka MSD, ikiwa ni utekelezaji wa agizo la Rais la kutaka jengo lililokuwa likitumiwa na watumishi kubadilishwa na kuwa hodi ya akina mama na watoto,” amesema

Tarehe 10 Februari mwaka huu Rais Magufuli alifanya ziara ya kushtukiza Muhimbili na kutembelea wodi namba 39 na kukuta magodoro yakilazwa sakafuni huku majitaka kutoka chooni yakielekea kwenye magodoro hayo.

Rais Magufuli alitoa agizo ndani ya siku mbili jengo hilo la ghorofa tatu lililokuwa likitumiwa na watumishi, watumishi hao kuondolewa na kufanywa wodi ya akina mama na watoto.

 

error: Content is protected !!