January 23, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Wakurugenzi Jiji la Mwanza kukiona cha moto

Spread the love

SERIKALI mkoani Mwanza imewapa wiki moja wakurugenzi wa halmashauli ya Jiji la Mwanza na manispaa ya Ilemela mkoani hapa kuhakikisha wanakarabati na kujenga barabara ambazo ni sugu na mbovu. Anaandika Moses Mseti, Mwanza … (endelea).

Agizo hilo lilitolewa jana na Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Magesa Mulongo, wakati wa kikao kilichowakutanisha wakurugenzi, wakuu wa wilaya, makatibu Tawala na kamati ya ulinzi na usalama mkoa, juu ya mipango mkakati kwa wanafunzi waliochaguliwa kuingia kidato cha kwanza mwakani.

Mulongo amesema kuwa mkurugenzi wa Jiji la mwanza na manispaa ya Ilemela wanapaswa kuhakikisha miundombinu ya barabara katika maeneo yao inakuwa rafiki ili shughuli za kimaendeleo ziweze kufanyika kiurahisi na haraka.

Amesema kuwa viongozi hao wanapaswa kutafuta vifaa ikiwamo greda za kukarabati barabara ambazo ni kolofi zikiwamo barabara ya mwaloni kwenda Kirumba na ile barabara ya Igombe isiyokuwa na rami ambayo ni mbovu sana.

“Nawapa wiki moja wakurugenzi wa Nyamagana (Jiji) na Ilemela kuhakikisha mnakarabati na kujenga barabara ambazo ni kolofi, nyie hapa mjini hatuwezi kusema mnalima, kazi yenu ni miundombinu tu,” amesema Mulongo.

Amesema kuwa kutokana na Serikali ya awamu ya tano kuhitaji maendeleo ya vitendo haina budi viongozi hao kuacha kufanya kazi zao kwa vitendo ili kumsaidia Rais Dk. John Magufuli katika kupambana na tatizo la umaskini kwa Watanzania.

Pia amesema baada ya wiki moja aliyoitoa ikimalizika hatasita kuanza ufuatiliaji wa kina juu ya agizo lake kama limefanikiwa ama halijafanikiwa na kwamba kama litakuwa bado hatua nyingine zitafuata kuhakikisha miundombinu ya Mwanza inakuwa ya uhakika.

Katika hatua hiyo amewaonya wazazi na walezi watakaoshindwa kuwapeleka wazazi wao shuleni mwakani na kwamba watakaobainika hatua kali za kisheria zitachukuliwa juu yao.

Alidai kuwa hivi sasa hakuna mzazi wala mlezi yeyote yule atakaeweka kisingizio chochote kwani michango na ada zimeondolewa hivyo wazazi wanapaswa kuwapeleka watoto wao shule.

Hata hivyo Jiji la Mwanza katika kipindi hiki cha mvua hali ya miundombinu ya barabara imekuwa ni kero kubwa sana kwa wakazi wa Jiji hilo licha ya jitihada za ukarabati kufanyika.

error: Content is protected !!