August 8, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Wakulima watakiwa kuwa makini na mbegu

Shamba la mahindi

Spread the love

WAKULIMA nchini wamesisitizwa kununua mbegu kwenye maduka yaliyosajiliwa huku wakihakikisha ubora wa mbegu wanazonunua kwa kuwa na lebo ya TOSCI ili kuweza kupanda mbegu bora na kuvuna mazao yanayoendana na hekari wanazolima na kuondokana na baa la njaa, anaandika Christina Haule.

Mkurugenzi wa Taasisi ya Kudhibiti ubora wa mbegu Tanzania (TOSCI) iliyopo chini ya Wizara ya Kilimo na Mifugo, Patrick Ngwediagi amesema licha ya TOSCI kuendelea na mapambano dhidi ya wauzaji wa mbegu feki lakini pia jamii nayo inapaswa kuwa makini ili kuweza kuepukana na changamoto ya kukosa mazao bora.

Aidha aliwahimiza wazalishaji wa mbegu kuzalisha kwa kufuata taratibu, kanuni na sheria zilizopo ili kumuwezesha mkulima kupata mbegu bora itakayomuwezesha kuzalisha mazao bora na kuleta tija kwake na Taifa kwa ujumla.

Amesema kwa kuzingatia sheria ya mbegu ya mwaka 2003 iliyorekebishwa mwaka 2014 na kanuni za mbegu ya mwaka 2007 iliyorekebishwa mwaka 2016 wazalishaji mbegu wanaweza kuzalisha mbegu bora na kukidhi matakwa ya Taifa.

Ngwediagi amesema, mbegu zinapaswa kuuzwa kwenye maduka yaliyokubalika huku zikiwa zimethibitishwa na TOSCI na yeyote atakayekamatwa akiuza mbegu isiyothibitika atachukuliwa hatua ikiwemo kufungiwa biashara yake na yeye kupandishwa kizimbani kukabiliana na mashataka kwa mujibu wa sheria.

Akizungumzia msimu wa kilimo, mbegu na wakulima wa vijijini ambako utaratibu wa mbegu kwenye maduka maalum haupo, Mkurugenzi huyo aliwashauri wakulima wa maeneo kama hayo kuhakikisha wanapata mafunzo ya mpango maalum wa kuzalisha mbegu uitwao QDS unaotolewa ngazi ya wilaya.

Amesema, kufuatia kuwajali zaidi wakulima wakiwemo wa vijijini, TOSCI iliwaelimisha wataalamu wa kilimo wa kila wilaya namna ya upatikanaji wa mbegu bora, elimu ambayo maofisa hao nchi nzima kwa sasa wamekuwa wakiitoa katika maeneo yao.

error: Content is protected !!