January 28, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Wakulima wajeruhi mifugo 200 Morogoro

Spread the love

UHASAMA kati ya wakulima na wafugaji unaendelea kukomaa mkoani Morogoro ambapo zaidi ya mifugo 200 imejeruhiwa kwenye Kijiji cha Kambara wilayani Mvomero. Anaandika Christina Raphael.

Kundi lililofanya uharibifu huo linatambulika kwa jina la ‘Mwamo’ ambapo limejeruhi mifugo hiyo kwa kuikatakata kwa mapanga likidai kulipiza kisasi cha kuliwa mazao yao.

Mifugo iliyojeruhiwa ni pamoja na mbuzi, kondoo na ndama ambapo kundi hilo la wakulima lilivamia nyumbani kwa mfugaji na kufanya uharibifu huo.

Mwandishi wa habari hizi alishuhudia mifugo hiyo ikiwa imejeruhiwa wilayani humo huku wafugaji wa jamii ya kimasai akiwemo mmiliki wa mifugo hiyo Christina Nuru wakilalamikia tukio hilo na kusema kuwa kitendo hicho ni cha kinyama na kinaashiria kuwaingiza kwenye umaskini.

Daniel Olimwinisi ambaye ni mfugaji wa jamii ya kimasai ameiomba serikali kutoa tamko kali ili kukomesha hali hiyo kwa kuwa inatishia usalama wa mifugo yao na kuhatarisha hali ya usalama.

Mwigulu Nchemba, Waziri wa Kilimo, Mifugo na Uvuvi amefika katika eneo la tukio ambapo alionesha kusikitishwa na unyama uliofanywa na wakulima huku akionya hatua ya watu kutumia sheria mkononi.

Baada ya kuona uhalifu huo Mwigulu aliitisha mkutano na kijiji ambapo wengi waligoma kuitikia kwa madai kuwa, Betty Mkwasa, Mkuu wa Wilaya hiyo anachangia kuendelea kwa migogoro.

Hata hivyo wanakijiji wachache walijitokeza ambapo Mkwasa alisema, hahusiki kwenye mgogoro huo kwani anachojua yeye ni kuwa inachochewa na wanasiasa.

error: Content is protected !!