December 1, 2021

Uhuru hauna Mipaka

Wakulima wa korosho Lindi, Mtwara washauriwa kujiwekea akiba NBC

Spread the love

 

MKUU wa Wilaya ya Lindi, Shaibu Ndemanga amewashauri wakulima wa zao la korosho katika mikoa ya Lindi na Mtwara kujiwekea akiba sambamba na kufungua akaunti za akiba kwa ajili ya watoto hatua ambayo ametaja kuwa itawasaidia kujenga nidhamu ya matumizi ya fedha ili kujikwamua na umaskini. Anaripoti Mwandishi Wetu, Lindi … (endelea).

Akizungumza mwishoni mwa wiki mkoani humo wakati wa hafla fupi ya kukabidhi ya zawadi mbambali kwa wakulima wa korosho mkoa wa Mtwara walioibuka washindi wa droo ya tatu ya   kampeni ya ‘Vuna Zaidi na NBC Shambani’Bw Ndemanga alisema licha ya wakazi wa mikoa hiyo kupata fedha nyingi kupitia kilimo cha mazao ya korosho na ufuta bado wamekuwa na changamoto za kifedha hususani katika masuala muhimu ikiwemo ada za watoto kutokana na ukata mkubwa unaotokana na wao kutojiwekea akiba.

“Kwa kuwa muda ambao tunapata fedha zitokanazo na kilimo huwa hauendani na muda wa kulipa ada za watoto wetu kumekuwa na ufujaji mkubwa wa fedha kwa matumizi yasiyo na tija sana. Ni kutokana na changamoto hiyo ndio sababu nawaomba sana mjenge utamaduni wa kujiwekea akiba ili isaidie muda sahihi ukifika,’’ alisema

Aliwashauri wakulima hao kufungua akaunti hizo kupitia benki ya NBC kutokana na ukaribu uliopo baina ya wakulima hao na benki hiyo huku akitolea mfano wa akaunti ya NBC Shambani iliyobuniwa mahususi kwa ajili ya wakulima.

“Kwa kuwa jitihada hizi za NBC zimeonesha kuunga mkono juhudi  za wakulima na serikali katika kuboresha kilimo cha korosho katika mikoa ya Mtwara na Lindi ni vema pia tuendeleze ushirikiano huu pia  hata kwenye akaunti nyingine zikiwemo za akiba na watoto wetu ili kuimarisha zaidi uhusiano wetu na zaidi tukiamini kwamba akufaaye kwa dhiki ndio rafiki wa kweli‘’ aliongeza.

Zaidi, aliwataka wakulima hao kutumia ipasavyo zawadi mbalimbali walizozipata wakulima hao kupitia kampeni hiyo ikiwemo pikipiki, baiskeli, pampu za kupulizia dawa  mikorosho ili viweze kuwasaidia katika kujiongezea uzalishaji wa mazao yao sambamba na kujiandaa vema kwa ajili ya msimu ujao.

Kwa upande wake Meneja wa Benki hiyo Kanda ya Kusini Bi Zubeider Haroun alisema kupitia droo hiyo ya pili benki ilitoa zawadi za aina mbalimbali ikiwemo pikipiki, baiskeli, pampu za kupulizia dawa  mikorosho, guta (Toyo),  pamoja na zawadi za nyingine  ikiwemo kanga, mabegi ya shule na madaftari kwa wakulima mmoja mmoja na AMCOS katika mikoa ya Mtwara na Lindi.

“Kampeni hii inalenga kusaidia jitihada  zilizowekwa na serikali za kuongeza uzalishaji wa korosho kutoka tani 280,000 zinazozalishwa sasa hadi kufikia tani 700,000  ifikapo mwaka 2025 sambamba na kuwahamasisha wakulima wa korosho kufanya kazi kwa bidii ili kuongeza uzalishaji.’’

“Naendelea kuwahamasisha wakulima waendelee kupitishia fedha zao kupitia benki akaunti ya NBC Shambani ili wawe kwenye nafasi kujishindia zawadi lukuki katika droo zinazofuata,’’ alisema Bi Zubeider

Kwa upande wao washindi wa droo hiyo waliishukuru benki ya NBC kwa kuandaa kwa kampeni hiyo kwa kuwa imekuwa na msaada mkubwa kwao.

“Mbali na zawadi mbalimbali ambazo tumefanikiwa kupata kupitia kampeni hii ya Vuna Zaidi na NBC Shambani’’  tunashukuru pia tumepata hamasa  na elimu ya kutosha kuhusu kilimo cha zao hili kibiashara zaidi.’’ Alisema Bw Mustafa Kuwasi mkulima wa korosho mkoa wa Lindi.

error: Content is protected !!