July 6, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Wakulima Njombe walia na bei za pembejeo

Spread the love

 

WAKULIMA wa Mkoa wa Njombe, wamefikisha kilio cha bei kubwa za pembejeo serikalini, wakitaka ipungue. Anaripoti Mwandishi Wetu, Njombe … (endelea).

Wakulima hao wamefikisha kilio hicho jana tarehe 20 Julai 2021, katika mkutano wao na Mbunge wa Njombe Mjini, Deodatus Mwanyika, uliofanyika mkoani humo.

Wakulima hao wamesema kuwa, kwa sasa wananunua pembejeo za kilimo kwa bei kati ya Sh. 85,000 hadi 100,000, kwa mfuko mmoja.

Wamedai kuwa, bei hiyo inawaingizia hasara katika kilimo chao, kwani iko juu kuzidi bei za mazao. Huku wakitolea mfano zao la viazi, ambalo wanadai kwa sasa linauzwa kwa Sh.18,000 kwa gunia.

Akijibu malalamiko hayo, Mwanyika  amesema bei hiyo imepanda kutokana na uhaba wa pembejeo na mbolea katika nchi zinazozalisha.

Mbunge huyo amesema, wakulima wa Tanzania wanategemea mbolea kutoka nje ya nchi, hivyo kukosekana kwake kuna athiri kilimo chao.

Amesema kupanda kwa bei za pembejeo sio mpango wa Serikali, kama ambavyo baadhi ya watu wanadhani, bali ni kutokana na uhaba wa mbolea katika nchi zinazozalisha.

Mwanyika amewataka wananchi kuwa wavumilivu kwani, Serikali inalishughulikia suala hilo kwa haraka zaidi na kabla ya msimu wa kilimo haujanza, huenda litakua limeshughulikiwa.

Amewaahidi wananchi kwamba, atafuatilia suala hilo kwa karibu na kupata majibu ya mara kwa mara kutoka  Serikalini, ili kujua muafaka wake.

Mwanyika ameendelea kufanya ziara ya kukutana na wananchi wa jimbo hilo na mpaka sasa ameshafanya ziara katika Kata za Matola na Makowo, tarehe 23 Julai 2021, anatarajiwa kufanya  ziara katika Kata ya Luponde.

error: Content is protected !!