June 30, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Wakubwa waendeleza majadiliano Z’bar

Spread the love

VIONGOZI wakuu wa kisiasa Zanzibar wameendelea kukutana kwa faragha katika jitihada za mwisho za kuokoa mvurugiko wa amani kutokana na hatua ya kufuta uchaguzi mzima wa Oktoba 25. Anaandika Jabir Idrissa, Zanzibar … (endelea).

Maalim Seif Shariff Hamad, mwanasiasa anayepigania haki yake ya kuongoza Zanzibar baada ya kuchaguliwa na wananchi katika uchaguzi huo aliingia Ikulu jana na kutoka baada ya saa nne za majadiliano.

Katika majadiliano ya jana, idadi ya viongozi waliokutana iliongezeka, baada ya kushuhudiwa Dk. Salmin Amour Juma, rais mstaafu wa awamu ya tano, naye akiingia na kushiriki majadiliano.

Jumatatu mapema wiki hii, majadiliano hayo yaliyofanyika Ikulu ya Zanzibar, yalimshirikisha rais aliyepo Dk. Ali Mohamed Shein, na marais wastaafu Ali Hassan Mwinyi (1984/85) na Amani Abeid Karume (2000/2005).

Mbali na hao, pia alikuwepo Makamu wa Pili wa Rais, Balozi Seif Ali Iddi, ambaye pia alishiriki majadiliano ya jana.

Awali jana asubuhi, kulienea taarifa mjini hapa kuwa Dk. Mohamed Gharib Bilal, aliyewahi kuwa Waziri Kiongozi kwa miaka mitano ya mwisho ya uongozi wa Dk. Salmin, alialikwa kushiriki kikao hicho.

Hata hivyo, mwandishi wa habari hizi amejiridhisha kuwa Dk. Bilal, ambaye amestaafu karibuni umakamu wa rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, hakuonekana katika kikao cha jana kilichoanza saa tatu asubuhi.

Mwandishi ameshuhudia rais mstaafu Karume akitoka kiasi cha saa 7 mchana jana, sambamba na Maalim Seif, lakini viongozi wengine walibakia ndani Ikulu.

Haifahamiki hasa kinachozungumzwa katika majadiliano ya viongozi hao ni nini hasa, ingawa vyanzo vya ndani ya serikali na CCM vinasema ni kujenga maridhiano ya uongozi utakavyokuwa.

“Kuna kazi muhimu inafanyika kwa sasa. Kujenga maridhiano ya namna Zanzibar itakavyoongozwa baada ya Tume ya Uchaguzi kutangaza matokeo ya kura za urais zilizobaki,” chanzo ndani ya Ikulu kimesema.

Mtoa taarifa huyo alipoulizwa kama maridhiano maana yake ni kuendelezwa kwa muundo wa Serikali ya Umoja wa Kitaifa (SUK), alisema “ndivyo ilivyo, kinachohakikishwa ni kuwa misingi ya Sheria na Katiba ya Zanzibar inazingatiwa na kufuatwa.”

Hatua ya viongozi wakuu wa Zanzibar kujadiliana kwa faragha hapa imeamsha upya mijadala kwenye mitaa ya mji huku kila mtu akibashiri vyake.

Hali hii inachangiwa na usiri wa vikao hivyo; kwa kuwa si wasaidizi wa Rais Dk. Shein wala wa Maalim Seif wanaoeleza kwa uwazi lengo la majadiliano yanayofanyika.

Maofisa wa Ikulu ya Zanzibar ndio hata kuthibitisha kuwa kunafanyika kikao hawaoni kama ni jambo muhimu kwa wananchi.

Waandishi wawili wa habari jana waliingia ndani Ikulu na kukutana na maofisa wa Idara ya Mawasiliano ya Rais, lakini hawakupata jibu la maana kwa maofisa waliokutana nao.

Waandishi hao ni Salma Said wa Mwananchi Communication Ltd (MCL) na Kulthum Ali wa Shirika la Utangazaji Tanzania (TBC) aliyepo Zanzibar.

Wasaidizi wa Maalim Seif ambaye pia ni Katibu Mkuu wa Chama cha Wananchi (CUF), angalau wanathibitisha kuwa kiongozi huyo anashiriki majadiliano hayo. Hawana maelezo zaidi kwa kuwa wote hawaingii kumsindikiza Maalim Seif kwenye vikao hivyo.

Maalim Seif amekuwa akihangaika kiupigania haki yake ya kuiongoza Zanzibar baada ya kushinda uchaguzi, lakini ikaja hatua ya Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC), Jecha Salim Jecha akafuta uchaguzi wote.

Jecha alifuta uchaguzi Oktoba 28 mchana wakati akiwa ameshatangaza matokeo ya kura za urais za majimbo 31 kati ya majimbio 54 ya Zanzibar.

Aliufuta uchaguzi kwa tangazo alolitoa kupitia Shirika la Utangazaji Zanzibar (ZBC) ambalo lilirushwa baada ya kurekodiwa mahali kusikojulikana, yeye akalisoma tu baada ya kulisaini.

Hakuna uthibitisho kuwa tangazo hilo liliandaliwa kwa umoja wa Tume ya Uchaguzi kwa kuwa baadhi ya makamishna wameshajitokeza na kusema hakuna kikao kilichojadili na kuhitimisha kutolewa kwa tangazo hilo.

Jecha alichukua hatua hiyo katika kile kinachoaminika hapa kuwa “shinikizo” la viongozi wakuu wa CCM Zanzibar, baada ya kuona chama hicho kimepoteza mamlaka ya kuongoza nchi kwa njia ya kura za wananchi.

Oktoba 26 asubuhi, Maalim Seif alitangaza mbele ya waandishi wa habari kuwa alikuwa amepata kura nyingi na kuelekea kushinda na kutaka Tume isicheleweshe utangazaji wa matokeo kwa kuwa kura zilishahesabiwa na matokeo kusainiwa vituoni na kila mhusika wa uchaguzi kama sheria inavyoelekeza.

Alieleza kuwa alikuwa amepata asilimia 52.87 ikiwa ni zaidi ya kura 200,000 dhidi ya asilimia 47.13 kiasi cha kura 178,000 zs Dk. Shein.

Kinyume cha maelezo ya Jecha kuwa uchaguzi ulikuwa na ukiukwaji mkubwa wa sharia, waangalizi wa asasi za ndani na wa kimataifa walisema awali kuwa uchaguzi ulikuwa safi kuliko ulivyokuwa mwaka 2010.

Kumekuwa na matamko mbalimbali ya kutaka Mwenyekiti Jecha afute tamko lake na kurudi kukamilisha kazi ya kuhakiki kura zilizobakia, na kumtangaza mshindi wa uchaguzi huo.

Tume ya Haki za Binaadamu Tanzania (THUU) ambayo ni asasi huru chini ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano imefika Zanzibar na kukusanya taarifa mbalimbali kuhusiana na mgogoro huo na kusema itatoa taarifa yake haraka iwezekanavyo kuhusu namna ya kutatua mgogoro wa uchaguzi Zanzibar.

Lakini kuna hali ya kushangaza kwamba viongozi wa CCM wanaonekana kumuunga mkono ingawa wanashindwa kueleza Jecha alitoa tangazo lake kwa mamlaka gani kwa kuwa Sheria ya Uchaguzi Zanzibar, Na. 11 ya mwaka 1984 haitoi mamlaka ya Mwenyekiti wala Tume kufuta uchaguzi.

Uchaguzi unaweza kufutwa na Msimamizi wa jimbo katika eneo ambako kuna uthibitisho uchaguzi ulivurugika kiasi cha kutovumilika kuendelea.

Wakati viongozi wakubwa wakiendeleza majadiliano ya faragha, jana asubuhi vifaru viwili vya Jeshi la Ulinzi Tanzania Zanzibar (JWTZ) vilishuhudiwa vikiranda mjini hapa na kuingia eneo la Bwawani Hoteli ambako kulikuwa na kituo cha kutangazia matokeo ya kura za urais. Kituo hicho kilizingirwa na askari wa jeshi hilo siku ile ambayo Mwenyekiti Jecha alishinikizwa na kutoa tangazo nje ya kituo hicho.

Vifaru hivyo vilipita barabara ya Darajani hadi Bwawani, na baada ya muda mfupi kukutwa vikirejea kupitia barabara ya Mlandege, kwendea kambi kuu ya Bavuai, Migombani, nje kidogo ya mji.

Inasemekana kuna maandalizi ya kuiwezesha Tume ya Uchaguzi kurudi kituoni Bwawani kwa ajili ya kutangaza matokeo ya mshindi wa urais, leo au kesho.

error: Content is protected !!