SHIRIKA la Chakula la Umoja wa Mataifa (WFP), limetangaza kuwa zaidi ya wakimbizi laki mbili waliopo nchini Tanzania, wataanza kupokea nusu ya mpango wa chakula kuanzia kesho Alhamisi, 1 Juni 2023. Anaripoti Mwandishi Wetu … (endelea).
Mkurugenzi wa WFP nchini Tanzania, Sarah Gordon-Gibson, ameeleza kuwa mgao wa chakula kwa wakimbizi Tanzania, umepunguzwa kwa kasi tangu mwaka 2020.
Taarifa ya Sarah ilinukuliwa na shirika la utangazaji la Ujerumani (DW), jana Jumanne.
Mpango wa Chakula Duniani, WFP limesema kuwa zaidi ya wakimbizi 200,000 nchini Tanzania watapokea nusu tu ya mgao wa chakula kuanzia mwezi ujao kwa sababu ya ukosefu wa pesa za wafadhili.
Wakimbizi watakaoathirika na uhaba huo wa chakula, asilimia 70 wanatoka nchini Burundi na asilimia 30 iliyosalia wanatokea Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo (DRC).
Kwa muda mrefu sasa, mataifa hayo mawili, yamekuwa yakikabiliwa na vita vya wenyewe kwa wenyewe, huku hali ikiwa mbaya zaidi nchini DRC, kufuatia kuibuka upya kwa makundi ya waasi, yanayoongozwa na wanamgambo wa M23.
Kwa mujibu wa WFP, kuanzia Juni mwaka huu, mgao utapungua kwa asilimia 50, hali inayoweza kuwaacha maelfu ya wakimbizi wakihangaika kukidhi mahitaji yao ya chakula.
Shirika hilo limesema, kunahitajika takribani kiasi cha dola za Marekani 21 milioni (zaidi ya Sh. 50 bilioni), kukabiliana na upungufu wa chakuka.
Sarah amesema shirika hilo lina wasiwasi mkubwa kwamba upunguzaji huo wa chakula, utawalazimisha wakimbizi kuingia katika mazingira magumu zaidi.
Leave a comment