August 16, 2022

Uhuru hauna Mipaka

‘Aliyekwapua’ Sh. 51.6 milioni NMB matatani

Spread the love

GODWIN Muganyizi (44), wakili wa kujitegemea hapa nchini pamoja  na wenzake watatu, wamepandishwa kizimbani katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu kujibu tuhuma za kuitapeli Benki ya NMB, Shilingi 51, 640, 000/-,  anaandika Faki Sosi.

Katika kesi hiyo, washitakiwa wengine ni Maseke zenge (50), Augustine Paschal Mrema (55) ambaye ni mhasibu na Ahmadi Kambona ambaye ni ofisa wa kampuni ya udalali ya Unyangala Auction Mart.

Akisoma mashtataka yao, Nassoro Katuga, Wakili wa Serikali mbele ya Amillius Mchaura, Hakimu Mkazi katika mahakama hiyo, amesema kosa la kwanza linalowakabili watuhumiwa hao ni kula njama ya kutenda kosa.

Inadaiwa kuwa watuhumiwa hao, walitenda kosa hilo siku isiyojulikana na sehemu isiyojulikana jijini Dar es Salaam.

Watuhumiwa hao pia wanadaiwa kutenda kosa la kughushi hukumu ya Mahakama ya Hakimu Mkazi Mkuu Kisutu, tarehe 22 Agosti mwaka 2014 iliyoelekezwa kwa Benki ya NMB tawi la Azikiwe na Jamhuri, ili kujipatia fedha kwa njia ya udanganyifu.

Watuhumiwa hao wanatuhumiwa kughushi amri ya mahakama ya kuitaka benki hiyo kulipa kiasi cha Sh. Milioni hamsini na moja, laki sita na elfu arobaini (51,640,000/-).

Watuhumiwa wote wamekana mashtaka hayo na dhamana yao ilikuwa wazi, wakitakiwa kudhaminiwa na wadhamini wawili watakaosaini hundi ya Sh. 10 Milioni kila mmoja, hata hivyo wadhamini wao hawakuwepo mahakamani siku ya leo na hivyo watuhumiwa kurejeshwa rumande.
Kesi hiyo itatajwa tena tarehe 13 Oktoba, mwaka huu.

error: Content is protected !!