Monday , 5 June 2023
Home Habari Mchanganyiko Wakili kumfikisha mahakamani DPP Biswalo
Habari MchanganyikoTangulizi

Wakili kumfikisha mahakamani DPP Biswalo

Peter Madeleka, Wakili wa Mahakama Kuu ya Tanzania
Spread the love

 

PETER Madeleka, Wakili wa Mahakama Kuu na mmoja wa watu walioshitakiwa kwa ‘utakasishaji fedha’, ameapa kumfikisha mahakamani, aliyekuwa Mkurugenzi wa Mashitaka (DDP), Biswalo Mganga. Anaripoti Mwadishi Wetu, Dar es Salaam … (endelea).

Anasema, DDP huyo wa zamani, alitumia vibaya mamlaka yake, ikiwamo kanuni za sheria ya Majadiliano ya Makubaliano (Plea Bargain), kuweka maelfu ya watu gerezani na kisha kuwalazimisha kulipa mabilioni ya fedha kwenye akaunti yake Benki Kuu ya Tanzania (BoT).

Akaunti hiyo maalumu ambayo DPP ameifungua, haina vote na haikaguliwi na Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), kwa kuwa haijaidhinishwa kwa mujibu wa sheria ya Bunge.

Alisema: “Baadhi ya aliyotenda Biswalo akiwa DPP, ni kinyume na Katiba na sheria inayounda ofisi ya DPP na mamlaka yake. Si siri, watu wengi wameumizwa, kutokana na kubambikizia watu kesi na kisha kupora fedha zao.”

Madeleka alisema: “Katika kipindi cha uongozi wake, mabilioni ya fedha za wanyonge, zimechukuliwa kwa mwavuli wa kesi za utakatishaji. Ni lazima aburutwe mahakamani, ili awajibike kwa aliyotenda akiwa katika ofisi ya umma.”

MwanaHALISI Online, limemtafuta Biswalo kwa njia ya simu kuhusu tuhuma dhidi yake ikiwemo baadhi kutaka Rais Samia Suluhu Hassan asimwapishe, amesema “siwezi kukujibu chochote kwa mtu ambaye simwoni, kama unahitaji mahojiano na mimi, tuonane uso kwa uso.”

Alipoelezwa wapi anaweza kupatikana alisema, “mtanitafuta nitakapopatikana.”

Kwa mujibu wa Madeleka, alisota mahubusu mbalimbali, likiwamo gereza kuu la Arusha, Kisongo, ambako alikaa kwa miezi 11 na siku 13, akituhumiwa kwa utakasishaji wa Sh.2 milioni.

Aidha, Madeleka ambaye kabla ya kuwa wakili, alikuwa ofisa wa Jeshi la Polisi, aliwekwa mahabusu Dar es Salaam, kwa miezi saba, akituhumiwa kwa uhujumu wuchumi wa Sh.1.4 bilioni.

Mbali na yeye kusota gerezani, mkewe ambaye alikuwa ofisa wa Uhamiaji, alisota gerezani kwa muda huo huo wa mumewe.

Biswalo aliteuliwa kuwa DPP na aliyekuwa Rais, Jakaya Kikwete, tarehe 3 Oktoba 2014. Aling’olewa Jumatano iliyopita ya tarehe 11 Mei 2021, na Rais Samia Suluhu Hassan, kwa kumteua kuwa Jaji wa Mahakama Kuu.

Katika kipindi cha utumishi wake, akiwa mkurugenzi wa mashtaka, hasa kipindi cha utawala wa awamu ya tano wa Hayati Rais John Pombe Magufuli, Biswalo alilaumiwa kwa kutumia madaraka yake vibaya.

Miongoni mwa wanaomtuhumu Biswalo kwa matumizi mabaya ya madaraka, ni pamoja na aliyekuwa Rais wa Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS), Fatma Karume, aliyesema kuwa Jaji huyo mpya, hakustahili uteuzi huo.

Aliyekuwa Mkurugenzi wa Mashtaka Tanzania (DPP), Biswalo Mganga

Fatma alisema, katika kipindi chote hicho, kumekuwa na malalamiko dhidi ya ofisi ya DPP ikiwamo ucheleweshaji kesi na matumizi ya Sheria ya Plea Bargain, ambapo baadhi ya watu walidai kugubikwa na urasimu katika utekelezwaji wake.

“Alitumia vibaya nafasi yake kama DPP na badala ya kupewa adhabu, kapewa zawadi ya ujaji na Rais Samia, hii si haki. Biswalo anastahili kuwa Jaji nchi hii kwa lipi alilofanya?” Alihoji Fatma ambaye ni mtoto wa Rais mstaafu wa Zanzibar, Amani Abeid Karume.

Mwingine anayedai kuwa Biswalo alitumia madaraka yake vibaya, na hivyo kustahili kufikishwa mahakamani, ni mwanasheria na mbunge wa zamani Singida Mashariki (Chadema), Tundu Lissu.

Akiandika kwenye ukurasa wake wa Twitter, huku akiambatanisha Sheria ya Taifa ya Huduma za Mashtaka, Lissu amesema: “Alistahili kufukuzwa kazi chini ya sheria hii, si kupewa hadhi ya Jaji wa Mahakama Kuu yetu.”

Akizungumza kwa uchungu, Madeleka alisema: “Matendo haya na mengine yaliyofanywa na Biswalo, hayawezi kuvumilika kwenye macho ya sheria. Nitakwenda mahakamani, ili kuweka rekodi sawa na kuwa fundisho kwa wengine.”

Rais wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan

Madeleka alisema, utaratibu wote uliokuwa unatumika kuhusu Plea Bargain, haukuwahi kuzingatia sheria na Katiba ya nchi. Aliongeza: “Ule ulikuwa uhalifu tu kama uhalifu mwingine.”

Alisema, kitu chochote kama kilikuwa kinafanyika nje ya taratibu na sheria zilizopo, si halali kwa mujibu wa sheria. Kama DPP alikuwa anachukua fedha za watu na kuagiza kuwekwa kwenye akaunti yake, bila kufuata utaratibu ulioelekezwa kwenye sheria, alikuwa anafanya uhalifu kama mtu mwingine yeyote.”

Alipoulizwa kama anaweza kumfikisha mahakamani mtu mwenye wadhifa wa Jaji wa Mahakama Kuu, Madeleka alisema: “Namfikisha mahakamani kama Biswalo, na kwamba kwa mujibu wa Katiba, DPP na hata Jaji, hana kinga ya kushtakiwa.”

Alitolea mfano wa Jaji mmoja nchini, ambaye alipandishwa kizimbani akituhumiwa kumgonga mwenda kwa miguu kwa gari.

Aidha, Madeleka alisema: “Jambo haliwezi kuwa halali kwa sababu eti limefanywa na DPP, hata kama limevunja sheria. Jambo linakuwa halali kwa sababu sheria imetamka jambo hili ni halali.

“Kama linafanyika kinyume na utaratibu, haijalishi amelifanya nani. Haijalishi ana hadhi gani kwa sasa na kateuliwa na nani. Ni kwa sababu Ibara ya 26 (1) (2) ya Katiba inasema: “Kila mtu ana wajibu wa kufuata na kutii Katiba ya nchi na sheria za Jamhuri ya Muungano, bila kujali cheo chake,” alisema.

Akizungumzia utaratibu wa Plea Bargain, Madeleka alisema, mfumo huo si mgeni duniani. Kwamba mataifa mbalimbali yanao, kwa lengo la kuhakikisha haki inapatikana haraka na kupunguza msongamano wa mahabusu magerezani.

Alisema Biswalo alisababisha mrundikano mkubwa wa mahabusu magerezani, kinyume na malengo ya Bunge, wakati wa kupitisha sheria ya Plea Bargain.

Aliongeza kuwa, kila kosa ambalo hapo awali lilikuwa linajitegemea, sasa linaonekana ni uhujumu uchumi. Mtu ameiba fedha, hizo fedha zinaonekana ni kutakasa fedha, ambalo ni moja ya makosa ya uhujumu uchumi, na kusababisha ongezeko la watu magerezani.

Alisema, kwa takwimu za Desemba 2019, wakati wa maadhimisho wa sherehe za Uhuru wa Tanzania Bara, Hayati Rais Magufuli alisema mahabusu katika magereza nchini, walikuwa 18,000, kati yao asilimia 90 ni wenye makosa ya uhujumu uchumi yasiyo na dhamana.

Shekhe Ponda

Katibu wa Shura ya Maimamu nchini, Sheikh Ponda Issa Ponda, alisema, uteuzi wa Biswalo kuwa Jaji wa Mahakama Kuu, haukustahili kwa namna yoyote ile.

Sheikh Issa Ponda, Katibu wa Taasisi na Jumuiya za Kiislamu

Shekhe Ponda alisema: “Wananchi wamekuwa na malalamiko kwa muda mrefu ya ukandamizaji wa haki za binadamu, katika utendaji na mfumo wa sheria nchini. Katika hilo, utendaji wa DPP, ni ushahidi tosha wa tatizo hilo. Magereza yamefurika kwa madai ya DPP kutafuta ushahidi dhidi yao.”

Ponda ambaye ni mkosoaji mkubwa na mpinga matukio ya ukiukwaji wa haki za binadamu na mtetezi wa Amani, alisema chini ya ofisi yake, DPP amesababisha maumivu kwa wananchi wengi.

Alisema: “Watu wanakaa magerezani kwa siku moja mpaka miaka 10 au zaidi, kwa uamuzi wa DPP. Lakini utafiti unaonesha madai hayo ya DPP ni uongo.”

Shekhe Ponda ambaye alipata kushitakiwa mara kadhaa na kulazimika kukaa gerezani kwa kunyimwa dhamana, mwaka 2013, alipigwa risasi na polisi na kusomewa mashitaka akiwa mahututi kitandani Muhimbili.

Alitolewa hospitali na kupelekwa gerezani akiwa taabani na akapelekwa gerezani hadi aliposhinda mwaka 2015.

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Articles

Habari Mchanganyiko

Tunduma watenga 60 milioni kujenga machinjio ya kisasa

Spread the loveHALMASHAURI ya mji Tunduma Imetenga kiasi cha Tshs Miloni 60...

Habari Mchanganyiko

Bilioni 17 kujenga bandari kavu Tunduma

Spread the loveHALMASHAURI ya mji Tunduma iliyopo wilayani  Momba mkoani Songwe imepatiwa...

Habari Mchanganyiko

Bandari ya Kigoma kuongezewa uwezo wa kutoa huduma zake

Spread the love  SERIKALI kupitia mamlaka ya Bandari nchini (TPA), imewekeza takribani...

Habari MchanganyikoTangulizi

Kifo cha mwanafunzi UDOM: Tume yamsafisha naibu waziri

Spread the loveTUME ya Haki za Binadamu na Utawala Bora nchini (THBUB),...

error: Content is protected !!