October 3, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Wakili amfuata Lissu urais Chadema

Wakili Gaspar Nicodemus Mwanalyela, akizungumza baada ya kukabidhiwa fomu ya kugombea Urais katika Uchaguzi Mkuu 2020 kwa tiketi ya Chadema

Spread the love

GASPAR Mwanalyela, Wakili wa Mahakama Kuu Tanzania, amechukua fomu ya kuomba kuteuliwa kugombea Urais wa Tanzania, kupitia Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema). Anaripoti Regina Mkonde, Dar es Salaam … (endelea).

Mwanalyela amechukua fomu hiyo ikiwa ni siku mbili baada ya Tundu Lissu, Makamu Mwenyekiti wa Chadema kuchukua fomu hiyo.

Wakili huyo amekabidhiwa fomu hiyo leo Jumatano tarehe 8 Julai 2020 na Reginald Munisi, Mkurugenzi wa Uchaguzi Chadema katika Makao Makuu ya chama hicho wilayani Kinondoni, jijini Dar es Salaam.

Wakili huyo amekuwa mwanachama wa tatu wa Chadema kuchukua fomu tangu uchukuaji fomu ulipoanza tarehe 19 Juni 2020. Zoezi hilo linatarajiwa kuhitimishwa tarehe 4 Julai 2020.

          Soma zaidi:-

Lissu ambaye pia ni Mwanasheria wa Chadema, ndio alikuwa wa kwanza kuchukua fomu hiyo tarehe 4 Julai 2020, kupitia wakala wake David Jumbe. Dk. Mayrose Majinge alikuwa wa pili, alichukua fomu jana tarehe 7 Julai 2020.

Wakili huyo amesema, ameamua kugombea ili kurudisha matumaini kwa wananchi walio na hofu na wenye kukata tamaa.

Amesema, atafuata nyayo za Baba wa Taifa, Hayati Julius Nyerere, za kuanzisha vijiji vya ujamaa na kujitegemea na kwamba, atakwenda mbali zaidi kwa kuanzisha vijiji vya watalaamu.

“Baba wa Taifa alianzisha vijiji vya ujamaa na kujitegemea. Tunapaswa kutengeza vijiji vya watalaamu wa madaktari, teknolojia na kilimo. vijiji hivi ni muhimu kuongeza ugunduzi na uvumbuzi.

“Suala la vijiji vya ujamaa na kujitegemea vilivyoanzishwa na Mwalimu Nyerere, nabadilisha ili tuwe na muundo mzuri wa urithishanaji taaluma tutalijengea Taifa mustalabali mwema,” amesema.

Wakili Gaspar Nicodemus Mwanalyela, akizungumza baada ya kukabidhiwa fomu ya kugombea Urais katika Uchaguzi Mkuu 2020 kwa tiketi ya Chadema

Pia amesema, endapo atateuliwa na Chadema kugombea urais na kisha kuchaguliwa na wananchi kuwa Rais wa Tanzania, atahakikisha Katiba ya wananchi inapatikana, pamoja na kutoa elimu ya uraia kwa wananchi ili wajue haki na majukumu yao katika Taifa.

“Ahadi yangu ni kutoa elimu juu ya kutambua haki na wajibu wao, sababu mtu hawezi kudai haki asiyofahamu na kutekeleza wajibu asiojua.

“Hili litaenda sambamba na upatikanaji Katiba ya wananchi, kwa sababu ndani ya Katiba, mkataba wa kijamii unapatikana maana yake tukiwa na Katiba ya hovyo, taifa litakua la hovyo,” amesema Wakili Mwanalyela.

Amesema, endapo atafanikiwa kuwa Rais wa Tanzania, ataufumua mfumo wa ulinzi na usalama, elimu, biashara, kilimo, teknolija ili sekta hizo ziendane na mabadiliko ya sasa.

Amewataka wananchi kushiriki uchaguzi huo pasi na kukata tamaa.

“Nimeisikia wananchi wengi wakiwa wamekata tamaa, hata wengine wakipata mashaka wataingiaje kwenye uchaguzi huu.

“Wapo wanaodhani hautakuwa wa maana na mantiki. Fursa hii ni adhimu, tuache woga tuingie ili tuendelee kudumu katika mustakabali wetu mwema,” amesema Wakili Mwanalyela.

Baada ya zoezi hilo kufungwa, kitachofuata ni vikao vya uchujaji, ambapo tarehe 22 Julai 2020, Kamati Kuu ya Chadema itapendekeza jina la mgombea urais, kisha tarehe 29 Julai 2020, mkutano mkuu wa Chadema utapitisha jina la mgombea wa urais wa Tanzania.

error: Content is protected !!