Thursday , 28 March 2024
Home Habari Mchanganyiko Wakazi Keko Akida wamlilia Rais Samia
Habari Mchanganyiko

Wakazi Keko Akida wamlilia Rais Samia

Spread the love

 

WAKAZI 106 wa mtaa wa Akida, Keko Machungwa wilayani Temeke, Dar es Salaam nchini Tanzania, wamemwomba Rais Samia Suluhu Hassan aingilie kati mchakato wa urasimishaji ardhi kwenye eneo hilo, kwa madai kuwa wapo watendaji wa ardhi mkoani hapa wanakwamisha. Anaripoti Suleiman Msuya, Dar es Salaam … (endelea).

Akizungumza kwa niaba ya wenzake, Zainabu Milinga (78), alisema wakazi wa mtaa wa Akida, wameitikia mwito wa Rais Samia anayetaka wananchi kurasimisha maeneo yao ila mchakato huo unahujumiwa.

Milinga alisema wananchi wamekusanya fedha na kuweka kwenye akaunti maalumu kwa ajili ya urasimishaji, ila katika mazingira ya kutatanisha, Manispaa imewaambia Kamishina wa Ardhi wa Mkoa wa Dar es Salaam, amezuia mchakato huo kuendelea.

“Sisi hatuna imani na Kamishina wa Mkoa, kwani taarifa tulizonazo ni kwamba yeye ndiye kikwazo, tunaomba Rais Samia aingilie kati, kwani tuko tayari kurasimishiwa eneo letu, kinyume na hapo, tutaamini kuwa kuna mchezo mchafu,” alisema.

Zainabu alisema pia zipo taarifa kuwa eneo hilo ni shamba la familia ya marehemu Akida, jambo ambalo si sahihi, kwa kuwa yeye alizaliwa hapo mwaka 1944 na mama yake alifia hapo na kuzikwa mwaka 1964 akiwa na umri wa miaka 50 na hakukuwa na mashamba bali nyumba.

“Hapa mimi nimeishi miaka 78 sasa tangu zamani hakukuwa na mashamba ni nyumba na watu wengi wameuziwa na marehemu Akida, hivyo taarifa za kuwapo familia inadai ni eneo lao si kweli,” alisema.

Alisema katika wanachohisi kuwapo mchezo mchafu, wapo baadhi ya wajukuu wa familia ya Akida ambao wamekuwa wakiwashawishi kuungana ili wapate fedha, jambo ambalo yeye haliungi mkono.

Katibu wa Tume ya Upimaji Ardhi katika eneo hilo, Henry Mwisongo alisema jambo la kushangaza, ni eneo kudaiwa kuwa la familia, huku baadhi ya wakazi wakiwa na hati za kumiliki ardhi.

Mwisongo alisema kilio chao ni Rais Samia kutoa maelekezo kwa Wizara ya Ardhi, kuhakikisha changamoto hiyo inakwisha na wao wanapata haki yao.

Daniel Mgalilwa ambaye ni mlemavu, alisema iwapo eneo hilo lilikuwa la familia hiyo, wasingechangishwa fedha za kulirasimisha.

“Mimi niliuziwa hapa mwaka 1978, yaani nina miaka zaidi ya 40 naishi hapa, sijawahi kusikia mtu akidai kuwa ni eneo la familia ya Akida. Tunaomba Serikali kupitia Rais Samia na Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, waingilie kati tupate haki yetu,” alisema.

Akizungumzia sakata hilo, Kamishina Msaidizi wa Ardhi wa Mkoa wa Dar es Salaam, Rashid Kayera alisema ofisi yake inafanyia kazi mgogoro huo, na leo watakutana na familia ya Akida kupata ufumbuzi.

Kayera alisema Serikali imejipanga kwa urasimishaji wa maeneo yote ya Dar es Salaam, ila kigezo kikubwa kinachotumika ni uhalali wa mmiliki.

“Eneo la Akida linalolalamikiwa lilipimwa mwaka 1951 na kupewa namba 161/3 na 161/4 na kumilikishwa kwa watu tofauti, ila baadaye likamilikiwa na familia ya Akida, hivyo hati namba 15120 ndiyo inawatambua.

“Baada ya eneo kupimwa, ofisi hii inawatambua Mzee, Mariam, Salum, Idd na Salama Mohammed Akida, hawa ndio nawatambua kama wamiliki,” alisema.

Kayera alisema mwaka 2010 Serikali ilitwaa eneo hilo na kuilipa familia ya Akida zaidi ya Sh bilioni tatu, ambayo ni nusu ya eneo lote, hivyo familia ilikuwa inadai nusu nyingine, jambo linalokwamisha upimaji kwa wananchi wanaolalamika.

“Tumekaa nao na kuwaeleza, kuwa ili warasimishiwe, ni lazima mgogoro huo umalizike, kinyume na hapo hawana haki ya kurasimishiwa. Ila leo tutakutana na familia ya Akida kupitia vielelezo,” alisema.

Kamishna alisema katika eneo hilo, nyumba 50 kati ya 99 ndizo zinatambuliwa, hivyo kutaka wananchi kuacha upotoshaji wa kinachoendelea.

Msimamizi wa Mirathi wa Familia ya Akida, Mzee Akida, alisema hawana nia ya kudhulumu wakazi wa eneo hilo, kwa kuwa ni ndugu zao, bali wanachodai ni haki yao ya kisheria.

Mzee alisema wanawasiliana na Wizara kuhakikisha zaidi ya Sh bilioni 3 anachodai kinalipwa na eneo hilo linakuwa huru kwa anayetaka kulitumia.

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Articles

BiasharaHabari Mchanganyiko

Wafanyabiashara, wawekezaji China waridhia kuwekeza bil. 800 katika sekta 5 nchini

Spread the loveUJUMBE wa wafanyabiashara na wawekezaji wakubwa kutoka Jimbo la Changzhou...

Habari Mchanganyiko

Bil. 4.42 kumaliza uhaba maji kata 2 Musoma Vijijini

Spread the loveWANANCHI wa kata za Busambara na Kiriba, Jimbo la Musoma...

BiasharaHabari Mchanganyiko

Soko nepi za watoto lashuka, watu wazima lapaa

Spread the loveKiwanda cha kutengeneza nepi cha Japan kimetangaza kuwa kitaacha kutengeneza...

Habari Mchanganyiko

NMB yafuturisha Dar, Majaliwa azitaka Serikali za Mitaa, Taasisi zijifunze kwao

Spread the loveBENKI ya NMB imewafuturisha wateja wake walio kwenye Mfungo wa...

error: Content is protected !!