June 30, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Wakamatwa kwa kutishia kuuwa kwa bastola

Spread the love

 

JESHI la Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam, linawashikilia watu wanne, kwa tuhuma za kutishia kuuwa watu kwa kutumia silaha aina ya bastola, wanazozimiliki kihalali. Anaripoti Mwandishi Wetu, Dar es Salaam…(endelea).

Hayo yamesemwa leo Jumatano, tarehe 4 Agosti 2021 na Kamanda wa Jeshi la Polisi la kanda hiyo, ACP Jumanne Muliro, akizungumza na wanahabari jijini Dar es Salaam.

Kamanda Muliro ametaja mtuhumiwa wa kwanza ni, Isack Robert Wile, maarufu kama Wambura, aliyekamatwa akiwa katika Baa ya 99 Vibes, iliyopo Sinza mkoani Dar es Salaam.

Ambapo anadaiwa kutoa bastola yake aina ya Browing, yenye namba za usajili TZCAR 72791 na kuanza kutishia watu huku akiwa amelewa.

Mtuhumiwa wa pili ni, Rashid Idd Mshana, aliyekamatwa baada ya kusambaa kwa video inayomuonesha akitishia watu kwa bastola aina ya Browning.

“Jeshi la Polisi lilifanya upelelezi na kufanikiwa kumkamata mtuhumiwa huyo, akiwa na silaha bastola yenye namba AP 06929TZCAR 113729, ikiwa na risasi 10 ndani ya magazine, inayomilikwa na kaka yake anayefahamika kwa jina la Mussa Rashid Mshana,” amesema Kamanda Muliro.

Kamanda Muliro amemtaja mtuhumiwa wa tatu ni, Mussa Rashid Mshana, anayetuhumiwa kwa kosa la uzembe baada ya kumuachia silaha mdogo wake Rashid , ambaye pia alikamatwa baada ya kujirekodi akitishia watu kwa kutumia silaha hiyo.

Ibrahim Shaibu, naye ni mtuhumiwa wa nne katika kosa hilo, aliyekamatwa tarehe 1 Agosti 2021, ambaye anadaiwa kutishia kumuuwa jirani yake, Chacha Mwita, walipokuwa wanagombania mipaka.

“Tarehe 1 Agosti 2021 majira ya saa 12:00 jioni, maeneo ya Vijibweni Kigamboni, alimtishia kumuua kwa silaha jirani yake aliyefahamika kwa jina Chacha Mwita, walipokuwa wanagombania mipaka ya kiwanja katika maeneo yao,” amesema Kamanda Muliro.

Kamanda Muliro ameongeza “mtuhumiwa alikamatwa akiwa na silaha bastola aina ya Luger, yenye namba A1365 ikiwa na risasi 06 ndani ya magazine , ambayo anaimiliki kihalali.”

Kamanda Muliro amesema silaha za watuhumiwa hao zinashikiliwa na Jeshi la Polisi Kanda “ na taratibu za kisheria zitafuatwa ikiwa ni pamoja na kuwafutia umiliki wa silaha hizo.”

error: Content is protected !!