October 1, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Wajumbe UVCCM wapokonywa simu mkutanoni

Spread the love

WAJUMBE wa Baraza la Vijana la Chama Cha Mapinduzi (UVCCM) jijini Dodoma, wamepokonywa simu zao za mkononi, wakati wa mkutano wa kura za maoni kutafuta mgombea ubunge viti maalum kundi la vijana. Anaripoti Mwandishi Wetu, Dodoma … (endelea).

Leo Alhamisi tarehe 30 Julai 2020, wajumbe wa UVCCM kwenye mikoa wanafanya kura za maoni, kupendekeza wagombea ubunge viti maalum kundi la vijana katika Uchaguzi Mkuu utakaofanyika Jumatano tarehe 28 Oktoba 2020.

Katika hali isiyo ya kawaida, wajumbe hao wamepokonywa simu zao kabla ya shughuli ya upigaji kura kuanza. Jambo ambalo halijawahi kushuhudiwa katika kura za maoni zilizopita ndani ya CCM.

Wilfred Mgonela, Katibu wa Hamasa na Chipukizi UVCCM mkoani Dodoma amesema, uchaguzi huo una mvutano mkubwa, ndio maana wameamua kuchukua hatua hiyo.

Mgonela amesema, baada ya upigaji kura kumalizika, wajumbe hao watarudishiwa simu zao.

“Tumeamua kufanya hivi ili kudhitibi taarifa zisizorasmi, wakimaliza kupiga kura watarudishiwa simu zao.”

“Tumemua kufanya hivi kwa maana, tunabadilika kila wakati. Siku hazifanani, uchaguzi umekuwa wa mvutano sana, tunaamini kufanya hivi tutafanya uchaguzi wa huru na haki,” amesema Mgonela.

Joel Makwaia, Katibu wa UVCCM mkoani Dodoma na msimamizi wa uchaguzi huo amesema, wamewanyang’anya wajumbe hao simu zao za mkoni kwa ajili ya kudhibiti kampeni za chini kwa chini, wakati upigaji kura ukiendelea.

“Sisi ni vijana na tuna uzoefu na wa shughuli za vijana hasa kwenye matukio ya uchaguzi, hatutaki kuona mjumbe anamtumia ujumbe mwenzake twende na fulani. Msimamo huu hapana,” amesema Makwaia.

Makwaia amesema, hatua hiyo inalenga kutoa nafasi kwa watia nia wote kutoa kampeni zao kisha kuchaguliwa na wajumbe kulingana na sifa zao.

“Tunataka tutoe fursa wagombea wote wajieleze kwa wajumbe na kila mjumbe atumie akili yake mwenyewe kumchagua, sio kushawishiwa na mtu kwa njia ya meseji. Ndio maana tumechukua simu za watu wote,” amesema Makwaia.

Awali, wajumbe hao walitaka kugoma kupokonywa simu, lakini wasimamizi wa uchaguzi huo waliwataka kutekeleza agizo hilo, na mwisho wa siku wakakubali kukabidhi simu zao.

Akizungumzia mgomo huo wa awali, Makwaia amesema hatua hiyo inadhihirisha kwamba kuna baadhi ya wajumbe walikuwa na nia ovu.

“Ukishaona wajumbe wanagoma, inaonesha tunalotaka kufanya ni jema kuondoa mizengwe. Mtu anagoma maana yake ni kwamba ana jambo lake anataka kufanya,” amesema Makwaia.

Katibu huyo wa UVCCM mkoani Dodoma amesema, uongozi wa umoja huo umejipanga kudhibiti vitendo vya rushwa ili kuunga jitihada za Rais wa Tanzania, John Pombe Magufuli za kutokomeza vitendo vya rushwa.

“Suala la rushwa ni ushenzi tu, naweza kusema watu wanaelekezwa waache rushwa lakini wanaendelea.”

“Na nawaasa wajumbe mtu kama alitoa rushwa msimchague, tuchague mtu sahihi, aliyetoa rushwa asichaguliwe, sisi vijana tunatakiwa kuunga mkono Rais Magufuli, tukiwa sehemu ya rushwa sio vizuri,” amesema Makwaia.

Kwa mujibu wa Makwaia, watia nia katika kura hizo wako 28 wakitafuta nafasi moja, ambapo wajumbe wa mkutano huo wako 40.

error: Content is protected !!