July 7, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Wajumbe feki wa BMK wambeba Sitta

Mjumbe wa Bunge Maalum la Katiba, Hamid Jongo

Spread the love

WAJUMBE wa Bunge Maalum la Katiba, wanaojiita kutoka taasisi za kidini, wamepata ujira mpya. Wanamtetea kwa nguvu zote, Samwel Sitta, mwenyekiti wa Bunge Maalum la Katiba.

Katika mradi wao huu, wamekana Bunge Maalum, kutengeneza rasimu mpya. Wamekana kujadili “rasimu mbadala” iliyoandaliwa na Chama Cha Mapinduzi (CCM).

Wamekana kwenda nje ya Rasimu ya Pili ya Katiba iliyowasilishwa bungeni na Mwenyekiti wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, Jaji Joseph Warioba.

Akizungumza na waandishi wa habari wiki iliyopita, Sheikh Hamid Jongo na Askofu Amos Muhagachi, wamesema Bunge Maalum la Katiba linafanya kazi zake zote kwa misingi ya sheria na taratibu.

Viongozi hao wa kidini wamefika mbali zaidi. Wametetea uhalali wa bunge hilo kisheria na kisiasa. Wamekana ubaguzi. Wamekana kuvunjwa kwa kanuni na wamejibia madhehebu ya kidini yanayotaka bunge hilo kusitishwa.

Ni jambo la kusikitisha kuona viongozi wa madhehebu ya kidini wamekana ukweli. Nani asiyejua kwamba mjadala ndani ya Bunge Maalum umehama kutoka kujadili Rasimu ya Jaji Warioba, hadi rasimu ya Asha –Rose Mingiro? Nani asiyejua kuwa Bunge Maalum linajadili kitu tofauti na maoni ya wananchi?

Nani asiyejua kuwa Sitta na kamati yake ya uongozi wanatenda kinyume na Sheria ya Mabadiliko ya Katiba, Sura Na. 83; na wanaendeshaji shughuli za bunge hilo bila kufuata kanuni?

Nani asiyejua kuwa idadi ya wajumbe kutoka upande wa pili wa Muungano – Jamhuri ya Zanzibar – haijatimia na haiwezi kutimia bila UKAWA kurejea bungeni?

Madai kuwa bunge lina idadi pungufu ya wajumbe, hayajatolewa na taasisi za kidini. Hayajatolewa na vyombo vya habari; wala hayajatolewa na UKAWA.

Madai kuwa Bunge Maalum la Katiba halijatimiza akidini, yametolewa na wajumbe wenzenu. Yametolewa na Sitta na Werema.

Siyo mara moja wala mbili, Werema amesikika akisema, ni muhimu kukabadilishwa kanuni za bunge hilo ili kuodoa kifungu kinachotambua wajumbe walioko bungeni; badala ya utaratibu wa sasa wa sheria kutambua wajumbe wote.

Kama yote haya yanafahamika, tamko la viongozi wa madhehebu ya kidini lililomalizikia kwa maneno, “BAKWATA KIKRISTO,” limelenga nini? Wamelipwa na nani kukana ukweli huu?

Lakini kuna hili pia: Kama Bunge Maalum linaendeshwa kwa kufuata kanuni na sheria; na linajadili rasimu ya Tume ya Rais ya Mabadiliko ya Katiba, kipi kilichosababisha Mwanasheria Mkuu Visiwani kujiuzulu?

Ninyi watumishi wa Mungu, kuweni wa kweli. Mtangulizeni mungu mbele badala ya fedha.

Mmedai kanuni za bunge zinafuatwa kwa usahihi. Lakini mnaweza kuonyesha kwa ufasaha kifungu cha sheria au kanuni inayotoa mamlaka kwa mwenyekiti wa Bunge Maalum kupokea maoni?

Mmezungumzia madai ya wajumbe wa kundi la 201 kupewa rushwa na kwa maelezo yenu, hii ni kashfa mnayosambaziwa na vyombo vya habari.

Lakini ukweli unabaki palepale. Tamko hili limesheheni ukakasi na linawafanya wananchi wengi kulitia shaka. Ni muhimu mkatubu; vinginevyo mnaweza kuliangamiza taifa kwenye matatizo.

Mwandishi wa makala, Edna J. Lugano ni msomaji wa MwanaHALISI Online. Anapatikana kwa simu Na. 0755 298 781, imeil: edinalugano@yahoo.com

error: Content is protected !!