July 5, 2022

Uhuru hauna Mipaka

‘Wajawazito hawajifungulii vituoni’

Wanawake wakwa wodini baada ya kujifungua hospitalini

Spread the love

SERIKALI imesema vifo vingi vinavyotokana na uzazi vinasababishwa na wajawazito kutojifungulia katika vituo vya afya. Anaandika Dany Tibason, Dodoma … (endelea).

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Uratibu na Bunge), Jenister Mhagama ametoa kauli hiyo, alipokuwa akijibu swali la nyongeza la Mbunge wa Viti Maalum, Suzan Lyimo (Chadema).

Lyimo katika swali lake alitaka kujua ni kwanini Serikali imeshindwa kupambana na vifo vitokanavyo na uzazi, kwamba badala ya kushuka hadi kufikia 133 kwa vizazi 100,000, vimekuwa 432 kwa vizazi hai 100,000.

Pia, alitaka kujua ni kwanini serikali imeshindwa kuwa na malengo ambayo yangefanikisha kufikia malengo ya milenia.

Akijibu swali hilo, Mhagama amesema pamoja na serikali kupambana na vifo hivyo, lakini bado akina mama wengi hawaendi katika vituo vya afya kwa ajili ya kujifungua.

Awali katika swali la msingi la mbunge wa Viti Maalum, Anastazia Wambura (CCM), alitaka kujua serikali imefikia wapi katika utelelezaji wa malengo ya maendeleo ya milenia katika kuboresha afya za wazazi na kupunguza vifo vya akima mama kutoka 529 kwa kila vizazi hai 100,000 mwaka 1990 hadi vifo 133 kila vizazi hai 100,000 ifikapo Desemba 2015.

Katika kujibu hilo, Naibu Waziri wa Habari, Vijana Utamaduni na Michezo, Juma Nkamia kwa niaba ya Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii, amesema kuwa juhudi hizo zimeonekana kuzaa matunda kidogo.

Amesema kuwa takwimu za sensa ya watu na makazi ya mwaka 2012, zinaonesha kwamba vifo vitokanavyo na uzazi vimeshuka hadi 432 kwa kila vizazi hai 100,000.

Nkamia amesema kulingana na takwimu za Shirika la Afya Duniani (WHO), nchi nyingi ikiwemo Tanzania, hazitaweza kufikia lengo namba tano ya maendeleo ifikapo mwaka 2015.

Kwamba, kutokana na hali hiyo kuna ulazima wa kujipanga upya katika maono ya mwaka 2020.

error: Content is protected !!