October 6, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Wajasiriamali 825 wanaufaika na mkopo Morogoro

Spread the love

KATIKA kuunga mkono juhudi za wajasiriamali na kuhakikisha wanajikwamua kiuchumi na kujiongezea kipato, Halmashauri ya Morogoro imetoa mkopo wa Sh  milioni  340 kwa   vikundi  63 vya wajasiriamali  vyenye jumla ya wanaufaika 825. Anaripoti Victor Makinda, Morogoro … (endelea).

Hayo yameelezwa jana tarehe 27 Februari, 2022 na Afisa Maendeleo ya Jamii, Halmashauri ya Morogoro, Florance Mwambene, wakati wa hafla ya kukabidhi hundi kwa vikundi vya wajasiriamali iliyofanyika kijijini Fulwe kata ya Mikese Halmashauri ya Morogoro.

Akifafanua mchanganuo wa mikopo hiyo Mwambene alisema kuwa jumla ya Sh milioni 340 zimetolewa  kwa vikundi 63  ikiwa ni  vikundi 35 vya wanawake,  23  vijana na vikundi vitano vya watu wenye ulemavu.

Mwambene amesema kati ya wananchi 825 walionufaika na mkopo huo wa asilimia 10 zilizotengwa  kutokana na mapato ya ndani ya Halmashauri hiyo  kwa ajili ya kuwawezesha wajasiriamali kwa uwiano wa asilimia 4 wanawake 4 vijana na asilimia 2 watu wenye ulemavu.

Amesema kuwa wanawake waliopata mkopo huo ni 487, vijana 281 na watu wenye ulemavu 32.

Mwambene aliongeza kusema kuwa mkopo huo tayari ulishawekwa kwenye akaunti za kila kikundi mwishoni mwa Mwezi Disemba 2021.

Awali akizungumza kwenye halfa hiyo, iliyowajuimsha wawakilishi wa vikundi vya wajasiriamali, Maafisa Maendeleo ya jamii, maafisa Ugani na wadau wa maendeleo wa halmashauri hiyo, Mwakilishi wa Mkuu wa Wilaya ya Morogoro ambaye ni Afisa Tawala ofisi ya Mkuu wa Wilaya ya Morogoro,  Hilaly Sagara, amesema Halmashauri hiyo itaendelea kutoa mikopo kwa wajasiriamali ili kuwawezesha kukua kiuchumi na kuondokana na umaskini wa kipato.

”Tutaendelea kutenga fedha kwa ajili ya kuwawezesha wajasiriamali kwa kwa kuwa tunaamini kuwa njia pekee ya kujikwamua kiuchumi ni kuwa na  vikundi vya uzalishaji vilivyowezeshwa,” amesema Sagara.

Pia Sagara amewaonya wanasiasa wanaoingilia mchakato wa mikopo hiyo kuacha mara moja kwa kuwa mikopo hiyo haitolewi kisiasa.

”Nimeelezwa hapa kuwa baaadhi ya wanasiasa wanaingilia michakato ya mikopo hii ama kwa kutoa upendeleo kwa baadhi ya vikundi au kujinuifa wao, ninawataka kuacha mara moja tabia hiyo kwa kuwa mikopo hii haitolewi kisiasa au kwa ajili ya kunufaisha mtu binafsi bali inatolewa kwa ajili ya kuwanufaisha wananachi wote kujikwamua na umaskini” amesema Sagara.

Naye Kiongozi wa Miradi wa Shirika la Kikristu la Tanganyika la Kuwahudumia Wakimbizi (TCRS), Rehema Samwel akizungumza kwa niaba ya wadau wa Maendeleo wa Halmashauri hiyo, amesema kuwa shirika lake litaendelea kushirikiana na wananchi na uongozi wa Halmshauri hiyo katika kuhakikisha linaendelea kuwawezesha wananchi kujikwamua katika lindi la umaskini.

”Dhima yetu kubwa ni kusaidiana na serikali kuwawezesha wananchi kujikwamua na umaskini kwa kushiriki shughuli mbali mbali za ujasiriamali na kilimo.

“TCRS tunafurahi kuona kuwa kati ya vikundi vya wajasiriamali ambavyo tuliviwezeshwa kuundwa na kuvipatia elimu ya ujasiriamali katika Halmashauri ya Morogoro, vikundi 23 vimekidhi vigezo vya kupatiwa mikopo na vinaendelea vizuri,” amesema.

Akizungumza kwa niaba ya wanufaika wa mkopo huo, Katibu wa Kikundi cha Vijana wajasiriamali cha Bosi kuku cha Kijijini Mlilingwa, Yohana Baliki, ameishukuru Halmashauri ya Morogoro kwa kutoa mikopo kwa vijana kwani imewawezesha kujipata ajira na kujiongezea kipato.

error: Content is protected !!