June 26, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Wajane wapaza sauti

Katibu Mkuu wa Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia na Watoto, Anna Maembe (mwenye mawani) akiongoza maandamano ya Siku ya Wajane Duniani

Spread the love

LEO ikiwa ni kilele cha Maadhimisho ya Siku ya Wajane Duniani, Chama Cha Wajane Tanzania (TAWIA) kimewataka wadau mbalimbali kujitokeza na kuwasaidia wajane. Anaandika Sarafina Lidwino … (endelea).

Mwenyekiti wa TAWIA, Rose Sarwatt wakati akisoma risala yake mbele ya mgeni rasmi Katibu Mkuu Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia na Watoto, Anna Maembe amewasihi wadau wa mikopo ikiwa ni pamoja na benki kuwakopeshe wajane mikopo isiyo na riba ili kuwainua kiuchumi.

Katika maadhimisho hayo Maembe alimwakilisha Naibu Waziri wa Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Angela Kairuki.

Sarwatt amesema, “tunaomba wamiliki wa mashule mbalimbali ambazo walikuwa wakisoma watoto kabla ya kuondokewa na wazazi wasiwafukuze wanafunzi baada ya kukosa ada kwani kwa kufanya hivyo kunawaharibu watoto kisaikolojia.”

Sarwatt ametoa wito kwa wadau mbalimbali kujitokeza kuwasaidia wajane hao kwani mbali na kupiga hatua, bado wana changamoto zinazowakabili ikiwemo kukosa ofisi ya kudumu na pesa za kuwaendeleza kiuchumi wajane hao.

Maadhimisho hayo kitaifa yamefanyika leo Jijini Dar es Salaam katika Viwanja vya Mnazi Mmoja ambapo yamehudhuriwa na wajane mbalimbali kutoka mikoa tofauti nchini.

Akizungumza katika maadhimisho hayo Maembe amesema, serikali imefarijika uwepo wa siku hiyo.

Maembe amesema, licha ya uwepo wa TAWIA bado serikali inawajibu wa kuweka sera, sheria na mikakati ya kuhakikisha wajane na watoto yatima wanapata haki zao za msingi.

“Tunazo sheria chache nzuri kama sheria ya mtoto ya mwaka 2009 na Penal Code. Lakini tunazo sheria chache ambazo ni kandamizi kwa makundi haya,” amesema Maembe.

Pia, mila za baadhi ya makabila nchini zinazofanyika katika jamii zetu zinakandamiza na kunyanyasa wajane.

Hata hivyo Maembe amewaambia wajane kuwa, sheria zote zinazowabana wajana zitarekebishwa ili ziwe rafiki kwao na watoto wao.

“Pia lazima sisi wote tuungane na kupiga vita mila potofu kama za kurithi na kutakasa wajane, huu ni unyanyasaji wa kijinsia,” amesema.

Na kwamba TAWIA izidi kutoa elimu kwa jamii na kuomba msaada wa kiushauri na sheria ili kukomesha mila hizi.

Aidha Maembe amesema, serikali ipo tayari kufanya kazi na kushirikiana na TAWIA ili kuandaa maandiko mbalimbali ya kuelimisha ikiwa ni pamoja na kuwatambulisha kwa wadau mbalimbali wapenda maendeleo.

error: Content is protected !!