June 14, 2021

Uhuru hauna Mipaka

Waitara ampandia Rais Magufuli

Spread the love

MWITA Waitara, Mbunge wa Jimbo la Ukonga, Dar es Salaam amesema, marufuku ya vyama vya siasa kufanya mikutano ya hadhara nchini inatokana na kukosekana kwa fikra pevu miongoni mwa viongozi, anaandika Regina Mkonde.

Waitara ambaye pia ni Mwenyekiti wa Uongozi Maalum wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) Mkoa wa Dar es Salaam amesema hayo leo katika kipindi cha ‘Tuongee Asubuhi’ kinachorushwa na Kituo cha Televisheni cha Star TV.

“Anachofanya Rais Magufuli ni kuzuia siasa za Chadema ili tusijiimarishe huku yeye akisuka mipango ya CCM kusikika peke yake pia anadhibiti vyombo vya habari vinavyoandika ukweli, hii ni siasa ya kitoto,” amesema na kuongeza;

“Maamuzi yaliyofanyika si ya haki, Magufuli amezuia mikutano ya Chadema anaruhusu ya CCM tu, mwanzo alikataza mikutano ya hadhara lakini alipoona chama chake kitahitaji kufanya mikutano akaruhusu wabunge kufanya kwenye maeneo yao, jambo hili si sawa.”

Waitara amesema kuwa inashangaza kuona hata tamko la kuwataka wabunge na madiwani peke yao kufanya siasa katika Kata na Majimbo yao likikiukwa kwa kuwaruhusu viongozi wakuu wa CCM kufanya mikutano lakini viongozi wa upinzani wakizuiliwa.

“Christopher Ole Sendeka ni msemaji wa CCM na siyo Mbunge, amefanya mkutano mkoani Arusha na polisi walimlinda wala hawakumzuia, lakini ukiacha hilo vyama visivyo na wabunge au madiwani vitajijenga vipi na kupata wabunge wapya bila mikutano?” Amehoji.

Katika hatua nyingine, Waitara amesisitiza adhima ya Chadema kufanya mikutano na maandamano nchi nzima kuanzia Septemba Mosi mwaka huu ili kupinga viashiria vya udikteta ambavyo vimeanza kuonekana katika serikali ya awamu ya tano.

“Kufanya mikutano ya hadhara ni haki ya kikatiba na kisheria kwa vyama vyote vya siasa, na UKUTA upo pale pale kwasababu hii ni nchi ya vyama vingi, kama Chadema hatufanyi mikutano ya maendeleo watuache, waitishe ya kwao na watushitaki kwa wananchi,” amesema.

error: Content is protected !!