KUELEKEA Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2020, Mwita Waitara ambaye ni Mbunge wa Ukonga pia Naibu Waziri wa Ofisi ya Rais Tamisemi, ameanza kupiga yowe. Anaripoti Regina Mkonde … (endelea).
Waitara aliyehamia CCM na ‘kukabidhiwa’ jimbo hilo baada ya kuondoka Chadema amesema, anachezewa mchezo mchafu jimboni humo huku akidai, Chadema ndio wanaoratibu.
“…halafu pale kuna watu zaidi ya milioni 1, kuchukiwa na mtu mmoja sio ajabu. Tuko kwenye mapambano, ngoja tukutane kwenye sanduku la kura,” amesema.
Waitara ametoa kauli hiyo baada ya kuwepo mvumo kwamba ametelekeza jimbo, hata hivyo amedai kwamba hakuna mtaa ambao hajaupitia.
Jana tarehe 6 Oktoba 2019 baadhi ya wakazi wa Ukonga, mbele ya Paul Makonda, Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam walimtuhumu Waitara kwamba hatoshi, na kuwa ametelekeza jimbo sambamba na kuhonga bia watu wanaoenda kumlalamikia changamoto za jimbo lake.
Akizungumza na MwanaHALISI Online kuhusu tuhuma hizo leo tarehe 7 Oktoba 2019, Waitara ameziita ‘ni siasa za majitaka’ akidai zinachochewa na wafuasi wa Chadema.
“Sijawahi kukutana na mtu kama huyo, ninachoona ni kwamba alikuwa mtu wa Chadema na aliongozwa na mwenyekiti wa jimbo. Bahati nzuri nilikuwa mbunge wa Ukonga kupitia Chadema kwa hiyo tunajuana. Na anapozungumzia kuna diwani wa Chadema, na ndio napita kuelekea nyumbani kwangu,” amesema Waitara na kuongeza:
“Na si kweli kwamba sijaonekana jimboni. Na kama kuna mtu ana ushahidi wa kutosha aeleze nilikutana naye kwenye hoteli gani? Hivi nikimkamata aisaidie polisi amenilisha maneno si itaonekana namuonea?”
Amedai tuhuma zinazoelekezwa kwake si za kwali “mambo yote ni ya uongo, hanifahamu, hajawahi kuja ofisini kwangu akanikosa sababu mimi Ukonga napatikana. Hakuna mtaa ambao sijawahi pita.”
Waitara amedai kuwa, tuhuma hizo zimeibua kwa kuwa joto la uchaguzi limepamba moto, na kuwa anawasubiri katika sanduku la kura.
“Kazi ya mbunge ni kuwasemea wananchi na ninasema kwenye vikao. Haya ni mambo ya kutengeneza, na sasa hivi joto la uchaguzi limepanda. Watu wanataka uenyekiti wa mtaa na wanajua Chadema watapata shida,” amesema Waitara na kuongeza:
“Kama kuna mtu ana hoja zake mimi nipo, atumie ustaarabu alete hoja zake. Zaidi ya hapo hizo ni siasa za majitaka. Halafu pale kuna watu zaidi ya milioni 1, kuchukiwa na mtu mmoja sio ajabu. Tuko kwenye mapambano, ngoja tukutane kwenye sanduku la kura.”
Hata hivyo amedai, wakati mwingine hutumia fedha zake kwa ajili ya maendeleo jimboni mwake.
“Na hiyo barabara haikuwa hivyo, mimi niliizibua sana usiku na mchana kwa kutumia gharama zangu. Haikuwa hivyo. Daladala hazikuwepo, tumepambana sisi sasa hivi daladala zinapita. Na fedha kwa ajili ya ujenzi zipo kwenye akaunti zimetengwa, kama haijatengenezwa ujue kuna sababu za msingi,” ameeleza Waitara.
Leave a comment