Sunday , 19 May 2024
Home Gazeti Habari za Siasa Waitara aanza mbio za kutaka kumng’oa Heche
Habari za SiasaTangulizi

Waitara aanza mbio za kutaka kumng’oa Heche

Mwita Waitara, Naibu Waziri wa TAMISEMI na Mbunge wa Ukonga. Picha ndogo John Heche. Mbunge wa Tarime Vijijini
Spread the love

MBUNGE wa Ukonga (CCM), Mwita Mwaikabe Waitara, ameanza kampeni za “kumdhoofisha” na hatimaye kumng’oa, hasimu wake mkuu kisiasa, mbunge wa Chadema katika jimbo la Tarime Vijijini, John Heche. Anaripoti Yusuph Katimba … (endelea).

Taarifa kutoka ndani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) na baadhi ya marafiki wa karibu na mbunge huyo, pamoja na Waitara mwenyewe zinasema, tayari mwanasiasa huyo ameamua kugombea ubunge katika jimbo la Heche.

Waitara ambaye alijiunga na CCM akitokea Chadema katikati ya mwaka huu, amekuwa kwenye “kazi maalum ya kuishughulikia Chadema na baadhi ya wabunge wake.”

Miongoni mwa wabunge ambao wanatajwa kuwa Waitara amejipa kazi ya kuwashughulikia, mbali na Heche, ni Ester Bulaya, mbunge wa Bunda na Esther Matiko (Bunda).

Kabla ya kujiunga na CCM, Waitara alikuwa mmoja wa wanachama na viongozi wa kuaminika ndani ya Chadema. Aliwahi pia kuwa mkuu wa idara ya sera na utafiti, makao makuu ya chama hicho.

Aidha, mbali na Chadema kumsimamisha kugombea ubunge katika jimbo la Ukonga (2015), Waitara alipata nafasi ya kugombea ubunge wa Tarime (2010) na uenyekiti wa serikali ya mtaa wa Kivule, jimboni Ukonga, wilayani Ilala, mkoani Dar es Salaam mwaka 2014.

“Nikweli kwamba Mwita Mwaikabe Waitara, anakwenda Tarime Vijini mwaka 2020. Huu ndio mkakati wetu kama chama cha siasa na ndio malengo ya Waitara mwenyewe,” ameeleza kiongozi mmoja mwandamizi wa chama hicho katika jimbo la Tarime.

Maelezo ya kiongozi huyo yanashabihiana moja kwa moja na maelezo ya katibu wa mbunge huyo ambaye amegoma kutajwa jina lake. Anasema, “hata baadhi ya viongozi wa CCM katika jimbo la Ukonga, tayari wameanza kutafuta mgombea mwingine wa kuziba nafasi yake.”

Anasema, lengo la mpango huo ni kuhakikisha chama hicho kinakomboa majimbo yake yote ya mkoa wa Mara katika uchaguzi unaotarajiwa kufanyika mwaka kesho.

Anasema, “mheshimiwa Waitara anakubalika sana katika eneo lile la Tarime. Chama kinajua jambo hilo na hivyo, kimeamua akasimame Tarime Vijijini ili asaidie kugomboa majimbo ya Bunda na Tarime Mjini.”

Anaongeza, “naye amemua kubeba jukumu hilo kwa sababu ya kukisaidia chama chake na kutaka kuwaonyesha Chadema kuwa yeye bado ni hazina kisiasa katika eneo hilo.”

Tayari CCM kimelikomboa jimbo la Serengeti mkoani humo baada ya aliyekuwa mbunge wa Chadema, Mwalimu Chacha Ryoba, kukimbia chama hicho mwishoni mwaka jana na kujiunga na CCM.

Kwa sasa, Mwalimu Ryoba, ni mbunge wa jimbo hilo kupitia CCM.

Mtoa taarifa wa MwanaHALISI Online anasema, pamoja na mpango huo wa CCM, kilichomsukuma Waitara kwenda kugombea ubunge Tarime, ni ugomvi wake na Heche na Chadema.

Waitara na Heche wamekuwa na uhasama mkubwa wa kisiasa tangu wanasiasa hao wawili walipokuwa wote Chadema.

Taarifa zinasema, hata kuondoka kwake ndani ya chama hicho na kujiunga na CCM, amekuwa akikuhusisha na Heche.

Mwanasiasa huyo amenukuliwa mara kadhaa akimtuhumu Heche kuwa amechangia kwa kiasi kikubwa kumgombanisha na mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe na baadhi ya viongozi wengine anaodai kuwa ni wafuasi wa mwenyekiti huyo.

Kwa mujibu wake, Heche ambaye ni mwenyekiti wa Chadema Kanda ya Victoria, alikuwa anamlisha maneno Mbowe ili yeye aendelee kutawala siasa za Mara na kuonekana ni mtu muhimu kwenye jamii wa Wakurya.

Alirejea maelezo haya mara kadhaa, hasa katika kipindi cha kampeni za uchaguzi mdogo jimboni Ukonga. Heche alilazimika kwenda Ukonga kujibu madai hayo.

Katika maelezo yake, Heche alikana kuwa alihusika katika kumsababishia Waitara kuondoka Chadema. Alisema, “kilichomkimbiza ni njaa yake ya kutaka madaraka kwa haraka.”

Hata hivyo, Waitara alitajwa mara kadhaa kuwa miongoni nwa wanachama waliokuwa wakisuka mkakati wa kumng’oa Mbowe, tangu Zitto Kabwe, alipokuwa Chadema.

Uhasama wa kisiasa wa Waitara na Heche, ulianza mwaka 2010, baada ya wanaisasa hao wawili, kujitosa kwenye kura za maoni kuwania ubunge wa Tarime.

Wakati huo, Heche alikuwa diwani wa Kata ya Tarime Mjini. Waitara alishinda na hivyo akafanywa kuwa mgombea. Hakushinda.

Vyanzo vya taarifa vinasema, “kuanzia hapo, kukawa na ugomvi wa ndani kwa ndani. Ugomvi ulipoa pale Waitara alipoamua kugombea Ukonga. Hivyo hatua yake ya kurudi Tarime, ni kuendeleza ugomvi huo wenye lengo la kumfuta kisiasa Heche.”

Wachambuzi wa mambo ya kisiasa wanasema, iwapo Waitara atagombea ubunge katika jimbo hilo, basi jimbo hilo litakuwa moja ya majimbo ambayo yatakuwa kwenye ushindani mkubwa.

Waitara ambaye kwa sasa, ni naibu waziri katika ofisi ya Rais (TAMISEMI), mwanzoni mwa wiki hii alikuwa jimboni humo kwa kisingizio cha mapumziko ya mwisho wa mwaka.

Lakini kinachoitwa, “mapumziko ya mwisho wa mwaka,” kilisheheni mbwebwe za kisiasa.

Miongoni mwa mbwembwe hizo, ni mapokezi makubwa yaliyopambwa na bendera na sare za chama chake hicho kipya; yaliyoongozwa na mkuu wa wilaya hiyo, Glorious Luoga.

Kwa mujibu wa ripoti za vyombo vya habari, msafara wa Waitara ulikuwa na ulinzi mkubwa wa askari polisi walikuwa wamebeba silaha za moto na mabomu ya machozi.

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Articles

Habari MchanganyikoHabari za Siasa

CCM yamteua Pele kuwa mgombea ubunge Kwahani

Spread the loveKamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya Chama Cha Mapinduzi (CCM)...

Habari MchanganyikoHabari za Siasa

Ujenzi kituo cha kupoza umeme Chalinze wafikia asilimia 93.7

Spread the loveKamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini imeeleza...

Habari MchanganyikoHabari za SiasaTangulizi

Wakili Mwabukusi anusurika kufungiwa, asema hatarudi nyuma

Spread the loveWAKILI Boniface Mwabukusi amesema kuwa hatorudi nyuma kuwatetea Watanzania na...

Habari MchanganyikoHabari za Siasa

RC Chongolo atangaza ‘vita’ kwa wanaovusha wageni kinyemela

Spread the loveKATIKA kulinda usalama wa nchi kupitia mpaka wa Songwe, Mkuu...

error: Content is protected !!