January 23, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Waislam watwangana msikitini

Baadhi ya waumini wa dini ya kiislamu msikiti mkuu wa Ijumaa Gongoni mjini Tabora, uliwahi kukumbwa na vurugu siku za nyuma

Spread the love

WATU wawili waumini wa dini ya Kiislamu, wamejeruhiwa katika vurugu zilizoibuka kwenye Msikiti wa Hidayah kata ya Kitangiri jijini Mwanza. Anaandika Mwandishi Wetu … (endelea).

Kufuatia vurugu hizo, Jeshi la Polisi Mkoa wa Mwanza, limelazimika kutumia mabomu ya machozi kuwatawanya waumini hao huku wawili wakitiwa mbaroni.

Vurugu hizo zilianza saa moja usiku wa kuamkia Mei 15 mwaka huu, kufuatia kijana mmoja kujitokeza mbele ya Msikiti huo akitaka kusoma barua ilidaiwa kuchochea fujo.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza, Kamishna Mwandamizi Msaidizi, Charles Mkumbo, amesema vurugu hizo zilizuka jioni wakati waumini hao wakiswali, ndipo ghafla alitokea kijana mmoja ambaye hakufahamika akitaka kusoma barua.

Mkumbo amesema baada ya waumini hao kumkataza kusoma barua hiyo, lilitokea kundi la vijana wengine na kuingia kwenye Msikiti huo wakiwa na mapanga na marungu na kuanza kufanya fujo katika msikiti huo.

“Baada ya kuona vurugu hizo zinaendelea, tulilazimika kutumia nguvu ya ziada kupiga mabomu ya machozi kuwatawanya na kufanikiwa kutuliza ghasia hizo. Watuhumiwa wanatarajiwa kufikishwa mahakamani pindi upelelzi utakapokamilika,” amesema Mkumbo.

Mmoja wa waumini, Kawawa Kiumba, ameliambia MwanaHALISIOnline kuwa, kufuatia mapigano hayo,  Serikali inapaswa kuingilia kati kumaliza mgogoro uliopo kati ya Haswali Suna na Suni Jamaa wanaotaka kuleta uvunjifu wa amani.

Amesema serikali inapaswa kuingilia kati mgogoro huo kutokana na kuwepo baadhi ya watu wachache wanaotumia mwanya huo kujinufaisha wao wenyewe badala ya kumwabudu Mwenyezi Mungu.

“Mimi nadhani hao vijana waliofanya fujo walikodishwa ili kuonekana kuna mgogoro, na hiyo yote kuna matajiri wachache ambao wameshindwa kuwaunganisha waumini hawa na badala yake wanakuwa chachu ya fujo,” amesema Kiumba.

Mwenyekiti wa Mtaa wa Medical Research, Patroba Maginga, amesema kitendo cha vurugu hizo kinasababisha wananchi kuathirika na kuacha kufanya shughuli za kimaendeleo ambazo zinawaingizia kipato. 

Hata hivyo, amesema vurugu hizo haziwaathiri waumini pekee bali na wananchi wengine, hivyo ni vyema serikali ikaingilia kati ili kutafuta muafaka wa jambo hilo kabla tukio halijajirudia.

error: Content is protected !!