July 5, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Waislam watoa pole kifo cha Dk. Mengi

Spread the love

BARAZA la Waislamu Tanzania (BAKWATA), limetoa pole kwa familia ya Dk. Reginald Abraham Mengi kutokana na kifo cha Mzee Mengi, kilichotokea Dubai, Falme za Kiarabu tarehe 2 Mei 2019. Anaripoti Mwandishi Wetu…(endelea).

Baraza hilo limeeleza kuwa, Dk. Mengi ambaye aliyekuwa Mwenyekiti wa Kampuni za IPP, atakumbukwa kutokana na hulka yake ya kutobagua watu kwa misingi ya dini.

Akizungumza na wanahabari jijini Dar es Salaam tarehe 3 Mei 2019, Mufti Abubakar Zubeir, Sheikh Mkuu wa Tanzania amesema, BAKWATA litamkumbuka Dk. Mengi kwa msaada wake alioutoa katika ujenzi wa misikiti hapa nchini.

Mufti Zubeir amesema, baraza hilo limepokea kwa masikitiko makubwa kifo cha Dk. Mengi, kwa kuwa alikuwa sehemu ya msaada kwa jamii.

Ameeleza kuwa, enzi za uhai wake Dk. Mengi alitoa msaada kwa watu wa dini zote, na kwamba atakumbukwa kwa kuwajali wagonjwa, masikini na watu wasiojiweza.

“Enzi za uhai wake Dk. Mengi alikuwa akiwajali wagonjwa na masikini na hakuwa mtu wa kujikweza, aliwapenda sana na kuwasaidia wasiojiweza,” amesema Mufti Zubeir.

Mwili wa Dk. Mengi unatarajiwa kuwasili nchini Jumatatu ya tarehe 6 Mei 2019 ukitokea mjini Dubai alikopoteza maisha, kisha utaagwa siku ya Jumanne kwenye viwanja vya Karimjee jijini Dar es Salaam, baada ya ratiba hiyo, mwili wake utasafirishwa siku ya Jumatano kuelekea mkoani Kilimanjaro kwa ajili ya mazishi siku ya Alhamisi ya terehe 9 Mei 2019.

error: Content is protected !!