June 26, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Waislam wasiyumbishwe kuhusu Lowassa

Spread the love

SHEIKH Khalifa Hamisi, muislam maarufu nchini ambaye siku hizi anajitokeza kuzungumzia masuala ya kisiasa akijitambulisha kuwakilisha Taasisi ya Imam Bukhar, ametakiwa kuacha kuwagawa Waislam kwa kauli za kichochezi wakati huu wanapokabiliwa na kupigakura ya kuchagua viongozi. Anaandika Jabir Idrissa … (endelea).

Kupitia tamko la Kamati ya Masheikh na Maimam wa Mkoa wa Dar es Salaam, Alhaji Sheikh Saidi Erico amesema kwamba Sheikh Khalifa amepotosha ukweli wa mambo na kitendo chake cha kumshambulia Askofu Josephat Gwajima kinaelekeza tu Waislam kutomchagua Edward Lowassa anayewakilisha Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa).

Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam jana, Alhaji Sheikh Erico aliyejitambulisha kama Mwenyekiti wa kamati hiyo ya masheikh na maimam wa Dar es Salaam, amesema Waislam kuelekezwa kutosikiliza au kuwachukia Wakristo kama Askofu Gwajima si jambo sahihi na si halali.

Akigusia suala la Lowassa kuwa mgombea urais aliyepitishwa na Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Alhaji Eriko amesema Lowassa hana ubaya aliowatendea Waislam kwa kuwa hata hiyo memorandamu anayotajwa kusaini alipokuwa Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu, aliisaini kwa agizo la Rais ambaye alikuwa ni mzee Ali Hassan Mwinyi ambaye ni Muislam.

Sheikh Eriko amesema kwa utaratibu wa majukumu serikalini, waziri anaweza kufanya lolote la kuagizwa na Rais aliyemteua, kwa hivyo huyo rais ndiye angebebeshwa mzigo na siyo Lowassa.

Amesema Lowassa amesaidia Waislam kwa michango mbalimbali ya kujenga misikiti hasa mkoani Arusha, na hakuna jambo baya alilowafanyia binafsi Waislam la kumfikisha kustahili kuonekana ni mtu mbaya.

Memorandamu aliyosaini Lowassa ilikuwa ni ya kuwezesha serikali kutoa fedha za kugharamia watumishi wa Kikristo wakiwemo madaktari walio kwenye hospitali zinazomilikiwa na Kanisa ambazo zilipewa hadhi na serikali kuhudumia umma pale palipokosekana hospitali za serikali.

“Mimi nasema Waislam wasiyumbishwe na Khalifa wakati huu wa uchaguzi. Waislam wawe huru kupiga kura kwa mtu ambaye wao wenyewe wataona atasaidia; sasa Waislam wako ndani (gerezani) wengi tu lakini Khalifa hatujamsikia anazungumzia hao watu, masheikh wamekamatwa na kuwekwa ndani.

“… Wengine wamepigwa risasi, mtawala si Mkristo ni Muislam, hata mimi ninayezungumza nilishawahi kukamatwa nikawekwa ndani miezi sita na yeye Khalifa mwenyewe alikamatwa akawekwa ndani nikakaa naye jela wakati huo rais ni Mwinyi muislam… Sheikh Ponda amepigwa risasi na akakamatwa na kuwekwa gerezani, mbona Khalifa hajayasema haya akalaumu kiongozi aliyepo ambaye ni Muislam Rais Kikwete,” amesema Sheikh Eriko.

Alhaji Eriko amesema kwamba Askofu Gwajima pamoja na kuwa ni Mkristo, amesaidia wananchi wa Salasala jimboni Kawe, ana akatoa msaada kwa Waislam kwa kuchimba visima sita kwenye misikiti ambavyo waumini wanatumia kwa haja mbalimbali ikiwemo kuweka udhu kwa ajili ya kusali.

Amesema kwamba mfano mzuri wa Waislam kusaidiwa na wasiokuwa Waislam upo katika historia ya maisha ya Mtume Muhammad (S.A.W) ambaye mambo yalipokuwa magumu kwenye mji wa Makkah, nchini Saudi Arabia, aliwaamuru Maswahaba – rafiki wasaidizi wake katika kueneza Uislam – waende kwa Mfalme wa Habash kunakoitwa sasa Ethiopia kupata hifadhi.

Amesema kama ilikuwa ni dhambi kuomba hifadhi kwa asiyekuwa Muislam basi kiongozi mkuu wa Uislam asingewashauri wasaidizi wake kufanya hivyo. Kutokea mtu anayejisema kuwa ni Muislam akatoa ushauri unaopingana na kile alichokiamini na kukielekeza kiongozi mkuu wa Uislam ndio dhambi na jambo lisilokubalika.

Alhaji Sheikh Eriko amesema kitendo cha Sheikh Khalifa kuhamasisha Waislam wamchukie Askofu Gwajima kwa kudai ameoteshwa kitu dhidi ya Waislam, hakina maana kwa sababu kwa asili katika Uislam ndoto anayoota mwanadamu, haina nafasi yoyote.

Alhaji Eriko amemkumbusha Sheikh Khalifa kurejea matendo yake yaliyompeleka kukichukia Chama Cha Mapinduzi (CCM) kwenye miaka ya 1990 kufikia hatua ya kushawishi walio wanachama wa chama hicho wahame na zikakusanywa kadi vigunia viwili lakini baadaye zilipotea na akaja akaanza kukipigia kampeni chama hichohicho.

Hata msimu huu wa uchaguzi, amesema Sheikh Eriko, Khalifa amekuwa akishawishi Waislam kuchagua wagombea wa CCM katika uchaguzi mkuu hatua inayoonesha anatumia wadhifa anaojipa kuyumbisha Waislam kitu kilicho haramu kuwagawa watu.

Skeikh Khalifa amelaumiwa kwa kuendekeza kuizungumzia amani bila ya kutanguliza haja ya watawala kuzingatia kuwapatia wananchi haki zao ndipo wahimizwe kudumisha amani

error: Content is protected !!