October 26, 2021

Uhuru hauna Mipaka

Wahitimu wa vyuo hawakidhi soko la Ajira

Spread the love

ASILIMIA 50% ya wahitimu kutoka vyuo vikuu hawakidhi mahitaji ya soko la Ajira katika nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki hali inayopelekea wengi kutoajiriwa katika sekta binafsi na zile za serikali. Anaandika Ferdinand Shayo, Arusha … (endelea).

Kwa mujibu wa utafiti uliofanywa na Baraza la Vyuo Vikuu vya Afrika Mashariki (IUCEA) pamoja na Baraza la Biashara la Afrika Mashariki (EABC ) mwaka 2013 hadi mwaka 2014 uliohusisha waajiri kutoka mashirika binafsi na yale ya serikali, wengi walilalamikia juu ya wahitimu wanaozalishwa na vyuo kutokidhi haja ya soko la ajira.

Katibu Mkuu wa Baraza la Vyuo vikuu vya Afrika Mashariki, Profesa Mayunga Nkunya amesema kuwa changamoto zilizoainishwa katika utafiti huo na waajiri ni pamoja na wahitimu kutoweza kutumia maarifa waliyoyapa kuleta tija katika maeneo ya kazi, kuwa na elimu ya nadharia kuliko ya vitendo pamoja na kukosa ujasiri wawapo kazini.

Profesa Mayunga amesema hayo wakati akizungumza na waandishi wa Habari juu ya Kongamano kubwa la kuwakutanisha waajiri, wafanyabiashara na wanafunzi wa vyuo litakalofanyika nchini Uganda Oktoba mwaka huu lengo ni kujadili mambo muhimu ambayo yanaweza kusaidia kuboresha elimu ya vyuo iweze kukidhi matakwa ya soko la ajira.

Mayunga amesema kuwa badala ya waajiri kulaumu wanayo nafasi ya kushiriki katika kutoa mawazo ambayo yatasaidia katika kuwaandaa wahitimu waweze kuleta matokeo yanayotarajiwa katika jamii.

“Waajiri wengi hulalamikia mitaala yetu kuwa haiendani na hali halisi ya soko mingine imeangalia mahitaji ya miaka ya nyuma na si sasa hiyo ni changamoto ambayo inapaswa kupatiwa ufumbuzi wa kudumu,” Amesema Profesa Mayunga

Mkurugenzi Mkuu wa Baraza la Biashara la Afrika Mashariki (EABC), Lilian Awinja amesema kuwa kutokana na ugunduzi wa mafuta na gesi unaoendelea katika ukanda wa Afrika Mashariki vyuo vikuu vina jukumu la kuwaandaa wahitimu wawe na ujuzi unaohitajika katika sekta hiyo badala ya kuchukua wataalamu kutoka nje.

error: Content is protected !!