July 7, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Waheshimiwa Wassira, Chikawe wanaishi dunia gani wenzetu?

Stephen Wassira
Spread the love

KAULI  za mawaziri wawili wa Rais Jakaya Kikwete, Mathias Chikawe, waziri wa Sheria na Katiba na yule wa Ofisi ya Rais Uratibu, Stephen Wassira zimetufunza kwamba kwa Mtanzania kuondoka kijijini kwao na kuhamia mjini hakumfanyi yeye kuwa mtu wa mjini hata kama angeishi mjini miaka 50.

Hebu wewe kawasikilize wanavyosema. Wassira kanukuliwa akisema kwamba muswada wa mabadiliko ya sheria ya mabadiliko ya katiba uliopitishwa hivi karibuni na Bunge eti ni halali sana tena mzuri kwa sababu kanuni zote zilifuatwa katika kuupitisha. Wassira hasemi kama kanuni hizo ni nzuri au mbaya.

Kwa upande wake Waziri Chikawe anadai kwamba muswada ulipitishwa unapaswa kutiwa sahihi na Rais Jakaya Kikwete haraka iwezekanavyo la sivyo kutatokea vurugu! Kwa busara ya Mheshiwa Chikawe katiba mbovu iliyopatikana bila kuwashirikisha Wazanziabari ni bora kuliko maandamano ya kuipinga.

Jinsi alivyokuwa akiongea kibabe kwenye runinga majuzi, Mheshimiwa Wassira alinikumbusha methali ya kwetu inayohamasisha ubabe pasipo sababu ya msingi. Kwetu sisi tunaotoka Mara tunajua methali isemayo: omonto achere isiko leo omoteme nomotihache na ng’ana yangekogambwa.

Methali hiyo inamaanisha kwamba mtu akija uwanjani kwako unayo haki ya kumpiga na gongo kubwa na jambo lolote lisitokee au kukupata. Lakini ni vema kweli au ni haki mtu aliyekuja uwanjani kwako kupigwa na mpigaji asihojiwe kwa sababu ni kwake? Pamoja na kuishi mjini bado Wassira anataka ya vijijini kwao Mara ndiyo yafuatwe ya kupiga na motihache bila kutumiai busara kuhoji mtu huyo kafuata nini kwako?

Lakini hiyo ndiyo busara ya CCM na viongozi wake akina Chikawe na Wassira. Sielewi wanaishi dunia gani wenzetu. Wao wanaona ni halali kabisa kupitisha kitu kibovu na kukitumia hata kama kuna  fursa ya kufanya marekebisho kama hayo ambayo wapinzani wanataka yafanyike kwa kumwomba Rais asiusaini muswada huo kuwa sheria.

Wassira na Chikawe wanadai sheria kanuni na taratibu za Bunge zilizingatiwa na kufuatwa na wabunge wa walioupitisha muswada huo unaolalamikiwa. Hebu tujiulize, ni sheria zipi, kanuni zipi na taratibu zipi zilizingatiwa na kufuatwa? Ni sheria, kanuni na taratibu halali na nzuri au zile halali lakini mbaya?

Mabwana Wassira na Chikawe wanapaswa kuelewa kwamba hata makaburu wa Afrika Kusini walikuwa na katiba, sheria, kanuni na taratibu halali lakini mbaya zilizopitishwa na Bunge la makaburu wenyewe bila kushirikishwa Wafrika, Waasia na watu wenye rangi mchanganyiko waitwao Coloureds.

Katiba, sheria, kanuni na taratibu za makaburu zilikuwa halali kwa sababu zilipitishwa kisheria lakini zilikuwa mbaya kwa sababu ziliwabagua wananchi wengine wan chi hiyo hiyo moja. Ni sheria na kanuni hizo hizo zilizopiga marufuku Mwafrika kumwoa Mzungu au kuogelea naye bichi moja!

Chikawe na Wassira wanafahamu na kama hawafahamu basi wanapaswa kufahamu kuwa katiba, sheria, kanuni na taratibu zinazotumika bungeni ni halali lakini mbaya siyo halali na nzuri kwa sababu zilipitishwa na unge la maccm waliokuwa bize kuhakikisha utawala wao na kula yao inadumu daima.

Kwa hiyo kaka yangu Wassira anapaswa kuyaacha ya kule kwetu ya mtu kupigwa na gongo kwa sababu tu kafika uwanjani mwa mtu bila kwanza kuhoji huyo mtu kafuata nini uwanjani kwa watu. Napinga hili huku nikijua fika kwamba huo ndio msimamo wa maccm kupiga tu mradi tu mtu kakaidi hata kama anayo haki ya kukaidi.

Inapopitishwa kanuni au sheria inayosababisha upendeleo kwa maccm halafu ikapingwa na wapinzani lakini maccm yakatumia wingi wao bungeni kuipitisha wapinzani wanayo haki ya kukaidi kwa sababu ni kanuni mbayahata kama imepitishwa kihalali kabisa tena kidemokrasia. Si tunasema wengi wape.

Chikawe na Wassira wanafahamu au wanapaswa kufahamu kwamba mahali penye wezi wengi kuliko idadi ya watu wema kutapitishwa sheria, kanuni na taratibu zinazotoa nafuu kwa wezi na kwamba sheria, kanuni na taratibu hizo zitakuwa halali lakini mbaya.

Mabwana Chikawe na Wassira wanafahamu au wanapaswa kufahamu kwamba kuwapo na demokrasia si lazima kuwapo na haki kama vile ambavyo wezi wakitumia wingi wao kuhalalisha wizi haitakuwa na maana kwamba kuna haki mahala hapo.

Nilipokuwa india miaka ya mwisho ya tisini kulitokea mzozo baina ya wanaume na wanawake kwamba wanaume wanakunywa pombe na kufanya fujo pamoja na kuchelewa nyumbani, basi wanawake wakatumia wingi wao kupitsha sheria inayopiga marufuku unywaji pombe katika jimbo la Haryana.

Matokeo ya sheria hiyo ni kwamba viwanda vya pombe jimboni Haryana viliuza pombe yao katika majimbo mengine kama vile uttar Pradesh, bihar, Punjab na mengine. Hii haikuwa sheria nzuri hata kama ilipitishwa kihalali kabisa tena kidemokrasia kwa wananchi wengi kama asilimia 47 hivi walikosa haki.

Chikawe na Wassira wajua au wanapaswa kujua kwamba sheria, kanuni na taratibu za bunge letu la Anna Makinda na Job ndugai ni halali kabisa lakini mbaya. Ni halali kwa sababu zilipitishwa kwa kufuata utaratibu unaotakiwa lakini ni mbaya kwa sababu zinapendelea maccm na hivyo zitasababisha kupatikana katiba mbaya vilevile.

Kwa mfano Wassira alinukuliwa akisema kuwa Mwenyekiti wa CHADEMA, Freeman Mbowe, anapaswa kufuata kanuni na kwamba akiwa mwanasiasa lengo lake ni kuingia madarakani akishinda na hivyo akishinda atatka wananchi wake wafuate kanuni.

Swali kwa Mheshimiwa Wassira ni kwamba wananchi wake huko bunda wanamwambia Bunge linatenda haki kwa wabunge wote? Hapa Chikawe na Wassira watuambie kama maccm yakiomba mwongozo maamuzi hutolewa kirahisi ni kwa nini mwongozo ukombwa na wapinzani maamuzi yasitolewe?

Na hapa Wassira na Chikawe wafahamu hoja siyo kutenda haki bali ni bunge kutenda haki na lionekane linatenda haki? Haiwezekani Bunge linalowalazimisha wabunge (soma wapinzani) kufuata kanuni lakini lenyewe lisifuate kanuni hizo kwa kutotoa maamuzi ya miongozo inayoombwa na wapinzani.

Mwisho wa mambo kinachoonekana hapa ni kwamba maccm yanakorofisha watu na kulazimisha waliokorofishwa wajibu kwa namna inayowafurahisha. Eti mtu akupige kofi na baadaye akuelekeze namna ya kujibu. Hawataki ujibu kwa kupiga kofi kama ulivyopigwa wewe bali ufuate kanuni iliyotungwa na hao wapigaji makofi.

Kinachoonekana hapa ni kwamba Wassira, Chikawe, Spika Makinda na Naibu wake Ndugai, wanaudhi watu wanakera watu na kukashifu watu halafu wanataka watu wanaoudhiwa, kukerwa na kukashifiwa wajibu kwa namna ambayoChikawe, Wassira, Makinda na Ndugai wanataka.

Yaani akina Mbowe, James Mbatia na wapinzani wengine walie au wapinge au wabishe kwa namna ambayo akina Chikawe, Wassira, Makinda na Ndugai wanataka au kupendelea. Wewe unipige ngumi lakini hutaki nikupige bali unataka nikushitaki eti ndiko kufuata kanuni hata kama nafahamu kuwa mashitaka yanapelekwa kwa nyani.

Heria, kanuni na taratibu za akina Makinda, Ndugai na mWassira na Chikawe hazistahili kufuatwa katika hali ya kawaida na ikibidi zitapingwa hata kama italazimika watu wengine kufungwa kwa sababu watakuwa wanapigania jambo lenye mustakabali mwema kwa Watanzania kama vile ambavyo akina Mandela walifungwa kwa kupigania  mambo yenye mustakabali mwema kwa Afrika Kusini.

error: Content is protected !!